Lissu arejesha nguvu ya upinzani

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

KUPIGWA risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye anaendelea matibabu Nairobi, nchini Kenya kunaonekana kuuimarisha nguvu ya upinzani nchini. RAI linachambua.

KUPIGWA risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye anaendelea matibabu Nairobi, nchini Kenya kunaonekana kuuimarisha nguvu ya upinzani nchini. RAI linachambua.

Septemba 7, mwaka huu iliripotiwa kuwa Lissu ameshambuliwa kwa risasi zaidi ya 20 nyumbani kwake, Area E, mkoani Dodoma na watu wasiojulikana.

Kupigwa risasi kwa Lissu, mbali ya kuushangaza umma wa Watanzania, lakini pia kumeibua mjadala mzito na mkali ambao umeendelea kushika hatamu kwenye mitandao ya kijamii.

Mbali ya kuibua mjadala mzito kwenye mitandao ya kijamii, lakini pia tukio la Lissu ndilo tukio lililoripotiwa na kutangazwa sana na vyombo vingi vya habari vya Kitaifa na Kimataifa, huku vingi vikiendelea kufuatilia maendelea ya afya yake.

Hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kutajwa na kuandikwa sana kwa jina la Lissu pamoja na chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) sanjari na upinzani kwa ujumla.

Mbali na Chadema na upinzani kwa ujumla kutajwa na kuripotiwa sana nje na ndani ya nchi, lakini pia tukio hilo limeonesha kuuimarisha zaidi upinzani tofauti na ilivyokuwa kabla, ambapo hali ya kisiasa hasa kwa upinzani ilikuwa tete kutokana na kupigwa marufuku kwa siasa za majukwaani.

Lakini pia katika siku za hivi karibuni tukio hilo ambalo linatajwa kuwa na sura ya mauaji limeonekana kufifisha jina la Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kipo kwenye maandalizi ya Mkutano wake Mkuu.

Tukio hilo linasababisha wanasiasawa upinzani kutazamwa kwa jicho la huruma na idadi kubwa ya Watanzania, wakiamini kuwa huenda kuna uonevu unatekelzwa dhidi yao.

Tukio hilo pia linaonekana dhahiri kuwapa hoja na ujasiri baadhi ya wanasiasa wa upinzani, ambao sasa kwa kutumia mitandao ya kijamii na vyombo vya Habari wameamua kusema bila hofu wala woga tofauti na ilivyokuwa awali, ambapo ni Lissu pakee ndiye aliyekuwa akionekana kuwa na uwezo wa kukosoa Serikali.

Katika kipindi kifupi cha wiki mbili tayari wabunge zaidi ya watano wa upinzani wameweza kupaza sauti zao wakikosoa na wakati mwingine kuinyooshea kidole Serikali au Bunge.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Ubungo, Saeed Kubenea, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ni miongoni mwa wabunge waliopaza sauti zao kukosoa mihimili ya dola ama dola kwa ujumla.

Hatua hiyo imewasababishia baadhi yao kuingia matatani kwa kukamatwa na jeshi la polisi ama kuhojiwa na mamlaka za Bunge kutokana na kauli zao.

Aidha, tukio hilo la Lissu linaonekana kupoteza kabisa hoja na mijadala ya makinikia na ripoti za Bunge za madini ya Tanzanite na Almasi kutokana na watu wengi kuhamishia fikra zao kwenye suala la kushambuliwa kwa Rais huyo wa chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).

Mbali na kufifishwa kwa hoja hizo za madini, lakini pia sakata la Lissu limepunguza kasi ya kauli za tambo na majigambo ya kisiasa aliyokuwa nayo Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa wa CCM, Humphrey Polepole.

Tukio hilo pia linaonekana kubeba upekee kwani ndilo lililoweza kuwasukuma viongozi mbalimbali wa nafasi za juu za taasisi za Serikali kuzungumza, jambo ambalo ni aghalabu kufanyika kwa baadhi yao kutokana na unyeti wa nafasi zao.

Viongozi ambao wanatajwa kuwa nadra kuzungumzia masuala yanayohusu siasa na wanasiasa kuliangana na nafasi zao ni Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na Usalama na Jaji Mkuu.

Hata hivyo, kupitia tukio hilo la Lissu, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo na Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Juma kwa nyakati tofauti walilizungumzia.

Pamoja na mambo mengine, sakata hilo la Lissu linatajwa kuwaunganisha zaidi Watanzania kwani bila kujali dini zao wamesimama pamoja ili kumwombea mwanasiasa huyo anayetajwa kutokuwa na hofu katika kutetea jambo lolote analoliamini.

Hivi karibuni pande mbili za dini zenye waumini wengi nchini kwa maana ya Ukristo na Uslamu walisimama pamoja kwa kila upande kwa nafasi yake kuendesha maombi na dua.

Kiu ya waumini hawa ni kuona Lissu anarejea katika hali yake ya kawaida na kuendelea na majukumu yake kama ilivyokuwa awali.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.