Serikali, TFF wajifunze kwa kilichotokea Kenya

Rai - - MBELE - NA AYOUB HINJO

RASMI Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani ‘CHAN’, haitofanyika tena nchini Kenya kutokana na sababu kadhaa za kiufundi ambazo kimsingi unaweza kusema wazi ni uzembe. Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF

RASMI Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani ‘CHAN’, haitofanyika tena nchini Kenya kutokana na sababu kadhaa za kiufundi ambazo kimsingi unaweza kusema wazi ni

uzembe.

Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF ilipanga fainali zijazo kufanyika Januari mwakani nchini Kenya, lakini katika hali ya kushtua mabosi hao wa soka barani humu wamebadili muandaaji na sasa zinasubiri kupewa nchi nyingine. Maamuzi ya CAF kuinyang’anya Kenya uenyeji wa michuano hiyo ulifikiwa siku chache baada ya jopo la wakaguzi wake kutua nchini humo na kufanya ukaguzi hapo Septemba 11 mwaka huu.

Hatua hiyo ya CAF imetokana na ukweli kuwa maandalizi kwa upande wa ukarabati wa viwanja ambavyo vingetumika kwa fainali hizo zinazoshirikisha jumla ya mataifa 16 havijakidhi viwango vinavyotakiwa kwa mujibu wa shirikisho hilo.

Sababu nyingine inatajwa ni hofu ya kutokea machafuko ya kisiasa kufutia vuguvugu la marudio ya uchaguzi nchini humo.

Inaaminika sababu za kisiasa ni moja kati ya vitu vilivyowafanya wakenya kushindwa kufanya maandaliai pamoja na ukarabati wa viwanja na badala yake kuelemewa na vuguvugu la kisiasa lililohusisha uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8 mwaka huu na baadaye kufutwa na Mahakama ya Juu nchini humo na kuagiza urudiwe tena ndani ya siku 60.

Siku chache zilizopita, Rais wa Shirikisho la Soka Nchini Kenya, Nick Mwendwa alikaririwa akikanusha taarifa zilizodai kwamba Kenya iko mbioni kupokwa nafasi ya kuandaa Michuano ya CHAN iliyopangwa kufanyika kuanzia Januari 12 hadi Februari 4 mwakani.

Katika taarifa hiyo kiongozi huyo alisema kwamba maandalizi kwa ujumla yakiwemo marekebisho ya viwanja kadhaa ambavyo ndivyo vilivyotarajiwa kutumika kwa fainali hizo yanaendelea vizuri na kwamba walitarajia kukamilisha ndani ya kipindi kifupi toka wakati huo.

Kauli ya kuwatoa hofu wakenya ilitolewa na kiongozi huyo pia siku moja kabla CAF kushusha rungu lake kwa Kenya na kuwaacha mashabiki na wadau wa soka nchini humo wasijue la kufanya kwani kutokana na hatua hiyo ni wazi hata nafasi yao ya kushiriki michuano hiyo kama mwenyeji nayo imeota mbawa.

Kenya kunyang’anywa nafasi hiyo ni wazi kwamba imepoteza pia fursa ya kujitangaza kimataifa kupitia sekta mbalimbali kama vile utalii na utamaduni ambazo zinagusa ukuaji wa uchumi moja kwa moja ambao ni moja kati ya vyanzo vya mapato makubwa ya taifa hilo.

Kenya imepoteza fursa nyingine kubwa ya kujifunza elimu ya uendeshaji wa biashara ya soka, kwa kuzalisha vijana wadogo. Elimu hiyo ingekuwa njia sahihi kwao kuelekea mageuzi ya soka

ambayo wameshaanza kupitia uzalishaji wa wachezaji kama Victor Wanyama na wengineo.

Mwaka 2015, nchi ya Morocco ilitengua uteuzi wao wa kuandaa michuano ya Mataifa ya Afrika, AFCON sababu ya kuhofia kwa uenezwaji wa virusi wa ebola.

Nchi hiyo ilichaguliwa kuandaa michuano hiyo mwaka 2011, huku ikizipiku nchi za DRC Congo na Afrika Kusini. Lakini walishindwa kuandaa kutokana na ugonjwa huo, kushika kasi Magharibi na Kaskazini mwa Afrika.

Hata hivyo tukio hilo la Kenya linaacha somo kubwa sana kwa Tanzania ambayo nayo ina kibarua kizito na cha kihistoria mwaka 2019 kwa kutakiwa kuandaa Fainali za AFCON kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17.

Ikiwa imebaki takribani mwaka mmoja na nusu swali la kujiuliza ni je tupo Tanzania iko tayari kuaandaa fainali hizo? Je maandalizi yameshaanza au vyombo husika vinasubiri muda ukaribie ndipo waanze maandalizi ya zima moto?

Kwa takribani mwaka unakaribia sasa Tanzania imekuwa bize kuhangaika kuangalia ni namna gani wataweza kutengeneza kikosi na kusahau kuwa kama hawatafanikwia katika maandalizi ya miundombinu hasa viwanja na hatoli basi nafasi hiyo inaweza kuyeyuka kama ilivyokuwa kwa majirani zao Kenya.

Uwanja wa Taifa, Uhuru, Kaitaba na Nyamagana ni viwanja bora ambavyo viko nchini. Licha ya viwanja hivyo kuwa na sehemu nzuri ya kuchezea, bado vingine vimekosa vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo, zahanati pamoja na miundombinu mingine muhimu kwa afya ya mchezo huo.

Inawezekana muda sio rafiki sana kwa sasa kutokana na ugumu halisi wa maandalizi hayo ikiambatana na upatikanaji wa fedha kutoka kukamilisha zoezi, lakini sasa TFF inapaswa kuishirikisha Serikali ili kuangalia ni namna gani kwa pamoja wanaweza kukamilisha kwa wakati mtihani huo.

Ikumbukwe tu ni vigumu kwa Tanzania katika siku zijazo kupewa haki ya kuandaa fainali za wakubwa kama haikuwahi kufanya hivyo katika fainali kama hizo katika ngazi za vijana, hivyo nafasi hiyo inabaki kuwa sehemu ya mchakato muhimu kama nchi kuelekea ndoto za kuandaa Afcon hapo baadaye.

Mwanzo mzuri wa uandaaji wa wa michuano hii kikamilifu ndio mwanzo wa kuaminika katika uandaaji wa michuano mikubwa ya Mataifa ya Afrika. Hii ni nafasi ya kipekee sana kwa Tanzania katika Nyanja zote kimichezo na kiuchumi.

Kilichotokea Kenya kiwe somo kwa Tanzania pengine zaidi ikichukuliwa Afrika Kusini kama somo tosha kwani baada ya kuwa mwenyeji wa Afcon mwaka 1996 ilikuwa rahisi kwao kupewa nafasi ya kuandaa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 na sasa bado wanaendelea kunufaika na fursa hiyo.

TFF na Serikali wanapaswa kuanza sasa lakini pia wakijifunza kitu kuhusiana na uzembe wa Kenya na wakati huo huo Afrika Kusini kama sehemu ya kujifunza klupitia mafanikio yao.

Kikosi cha Serengeti Boys

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.