WAKATI WENZETU WANAKWENDA SAYARI NYINGINE, SISI TWENDE VIJIJNI

Rai - - MBELE - VICTOR MAKINDA

Jambo linalonifurahisha na kunipa moyo ni kwamba wasomaji wengi wa RAI walio mijini na vijijini wamekuwa wakinipigia simu na kunitumia jumbe mbalimbali kunipongeza kwa makala haya ya vijijini na nimekuwa nikipokea mialiko mingi ya kwenda vijijini kujione hali halisi. Tuendelea na makala hii ya safari ya kijijini.

Wapo wanaonitaka kwenda maeneo ya vijiji wanavyoishi kushuhudia changamoto zinazowakabili lakini pia wapo wanaonitaka kwenda katika vijiji vyao kuona namna walivyoweza kupambana na hali halisi ya maisha na ugumu wa maisha kijijini na kufanikiwa kuwasaidia wanavijiji wenzao kuondokana na baadhi ya kero zilizokuwa zinawakabili kwa miaka nenda rudi.

Katika simu za mialiko nilizopokea wiki hii moja ilitoka kwa Askofu John Masawe wa kanisa na PAG mkoa wa Maorogoro. Askofu Masawe alinialika kwenda katika kijiji cha Msufini, kata ya Mvomero, Tarafa ya Mvomero, Wilayani Mvomero mkoani Morogoro. Safu ya Ukweli Ulivyo, ilifunga safari mpaka kijijini Msufini, Wilayani Mvomero.

Askofu Masawe alianza kunieleza kwa kina jinsi ambavyo amekuwa msomaja nguli wa RAI tangu mwishoni mwa miaka ya 90. Kupitia safu hii ya Ukweli Ulivyo, anatuma pongeza zake za dhati kwa waaandishi na wahariri wa gazeti hili kongwe pendwa la RAI. Anasema kuwa ameelimika mno na makala za RAI, zinazoigusa jamii pana katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Lengo hasa la mwaliko wake lilikuwa ni kunieleza namna ambavyo amepambana na changamoto nyingi ngumu na namna alivyoweza kuzivuka huku akisukumwa na dhamira yake ya dhati ya kuisaidia jamii inayoishi kijijini hususani katika kijiji cha Msufini na wilaya ya Mvomero kwa ujumla wake.

“Nilifanya utafiti wa kina na kubaini hali halisi ya maisha ya wananchi vijijini. Binafsi nimezaliwa na kukulia kijijini katika maisha duni. Nilichobaini kuwa maisha ya wananchi wa vijijini yanakabiliwa na changamoto nyingi katika nyanja za elimu, afya na shughuli za kilimo. Watoto yatima waishio vijijini hawana usaidizi na uangalizi wa kutosha. Maradhi kama vile Ukimwi yamewaacha wengi wakiwa katika hali ya umaskini wa kipato huku wakikabiliwa na maradhi. Pia yatima wanaoachwa na wazazi waliokufa kwa ugonjwa wa ukimwi wanahangaika sana. Watoto yatima kwa ujumla wake wanahitaji uangalizi mkubwa husuasani waishio vijijini kwani asasi nyingi za kiraia zimejikita mijini.

Huku vijijini haziji na hata zikija basi ni kwa kupita tu na kwa muda mfupi. Ndipo wazo la kuanzisha asasi ya Tanzania Movement Organization (TMO) iliponijia. Lengo kuu likiwa ni kuisaidia jamii inayoishi kijijini hasa hasa jamii yenye kipato cha chini.” Anaanza kusimulia Askofu Masawe.

Mwaka 2012 ndipo taasisi hii ilipoanza kufanya kazi. Sikuona sababu ya kuendesha shughuli za taasisi hii mjini ambako asasi nyingi zimejikita. Kwa kuwa nilikusudia kuiiinua jamii inayoishi kijijini niliisajili asasi na kujikita katika Kijiji cha Msufini wilayani Mvomero kijiji ambacho kipo nyuma sana kimaendeleo na kinakaliwa na wananchi wengi wenye kipato cha chini licha ya kijiji hiki kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba na ifaayo kwa kilimo cha nafaka, mboga mboga na matunda.

Katika kijiji hiki na tarafa ya Mvomero kwa ujumla, hakukuwa na huduma ya msingi ya kuwasaidia waathirika wa ukimwi. Asasi ya TMO iliwaangazia hao kwa kuanzia. Tukaanzisha mpango maalumu ya kuwasidia waaathirika wa ukimwi kwa kuwapa mitaji ya shughuli za kijasilamali, kilimo na ufugaji. Na kugawa chakula kwa jamii yote nyakati za njaa.Waathirika wengi wamenufaika na miradi hiyo na baadhi imewasaidia sana kuongeza muda wao wa kuishina kipato. Kwani licha ya kwamba serikali inatoa dawa bure za kurefusha maisha kwa waathirika, lakini ugumu wa maisha na hali duni ya kipato na lishe bora huwafanya baadhi ya waathirika kufa haraka. Serikali inajitahidi kwa kiasi kikubwa kusaidia jamii ya waathirika lakini mashirika binafsi, watu binafsi wenye uwezo ni muhimu kuwekeza nguvu zao kwa waathirika wa janga la ukimwi hususani waishio vijijini kwani uduni wa maisha ya kijijini ni adha kubwa kwa waathirika na wagonjwa wa ukimwi na jamii kwa ujumla. Askofu Masawe anaendea kusema kuwa licha ya kusaidia waathirika na wagonjwa wa Ukimwi vijijini kiuchumi, pia asasi ya TMO, iliona kuwa kuna haja na sababau kubwa kuwaangazia watoto yatima hususani ambao wazazi wao wamekufa kwa ugonjwa wa ukimwi kwa kuwawezesha kupata elimu. “Janga la Ukimwi limeacha baadhi ya familia zikiwa yatima na hazina uwezo wa kupata elimu. Hii ilikuwa ni kikwazo kikubwa sana nafsini mwangu. Nikaona licha ya kuwasaidia wagonjwa na waathirika wa ukimwi, ni vema pia TMO, ikaanzisha shule ya awali na Msingi, kijijini Msufini, ili iweze kutoa elimu kwa jamii iishio kijiijini hapa na wilaya ya Mvomero kwa ujumla.

Hii nilizingatia kuwa watoto wengi wa waathirika wa Ukimwi na watoto wa watu walio na kipato cha chini huku vijijini hawana fursa ya kupata elimu bora kama ambayo watu wenye uwezo huipata. Nikaona ni vema tuwe na shule ya Awali na Msingi ili watoto walioachwa na wazazi wao kwa ama ugonjwa wa ukimwi au kwa sababu nyingie, tuwasaidie kupata elimu bora ya mchepuo wa kingereza. Hapa Tukaanzisha shule ya msingi Nazareth, hapa hapa kijijini Msufini, Mvomero. Tunaishukuru serikali tumepata ushirikiano wa kutosha na hata kufanikiwa kusajili shule yetu mapema mwaka huu. Kwa sasa shule ipo darasa la nne ikiwa ni pamoja na elimu ya awali.

Lengo letu sio kufanya biashara ya elimu, lah hasha! Lengo letu ni kuhakikisha kuwa watoto wote wanaotoka katika familia za kimaskini katika vijijini vya wilaya ya Mvomero na mahali pengine Tanzania wanapata elimu bora ya awali na Msingi huku wazazi wakichangia viasi vidogo mno kulingana na uwezo walioa nao. Si lazima pesa hata kama mzazi anayo mahindi, mpunga, mbuzi, kuku bata, kwetu sisi huo nimchango, lengo ni kuhakikisha kuwa jamii ya kifukara ya kiTanzania iishio vijijini ipate elimu bora.

Serikali yetu ya awamu ya tano, ina kaulimbiu ya hapa kazi tu, sasa haiwezekani kufanya kazi kwa ufanisi pasipo na elimu bora. Tunachokifanya sisi ni kuhakikisha kuwa tunamsaidia Rais wetu kuhakikisha elimu bora yenye viwango inatolewa kwa watu wa madaraja yote ya jamii ya watanzania ili tuweze kuwaandaa vijana kuiishi kauli mbiu ya hapa kazi tu kivitendo.” Anaongeza kusema Askofu Masawe.

WITO WAKE KWA JAMII

Askofu Masawe anaiasa jamii ya kwa ujumla wake kufanya kazi bila kuchoka ili kukifikia kilele cha mafanikio, kwani bila kujituma kufanya kazi kamwe jamii ya kitanzania haiwezi kupiga hatua za maendeleo na kuondokana na adha ya kunyanyaswa na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.

“Kazi pekee ndio inayoweza kutukomboa watanzania mikononi mwa maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini kama anavosema Rais Magufuli kuwa Hapa Kazi tu.

“Pia ninatoa wito kwa serikali kuendelea kwenda vijijini kama ambavyo makala zako ndugu mwandishi unavyoziandika kwani sisi tuliojitoa na kuishi huku vijijini tunaziona changamoto nyingi mno zinazowakabili wananchi. Serikali pamoja na kuweka msisitizo wa kazi ni lazima ihakikishe kuwa inashuka vijijini ambako maelfu ya watanzania walipo na ambako bado kuna changamoto nyingi,” anasema.

Binafsi nimezaliwa na kukulia kijijini katika maisha duni. Nilichobaini kuwa maisha ya wananchi wa vijijini yanakabiliwa na changamoto nyingi katika nyanja za elimu, afya na shughuli za kilimo. Watoto yatima waishio vijijini hawana usaidizi na uangalizi wa kutosha. Maradhi kama vile Ukimwi yamewaacha wengi wakiwa katika hali ya umaskini wa kipato huku wakikabiliwa na maradhi

Wazazi na wanafunzi wa Shule ya kutwa ya Awali na Msingi ya Nazareth wakipata chakula katika sherehe za ufunguzi wa shule hiyo

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.