Serikali isiubeze mchakato wa Katiba Mpya

Rai - - HOJA YA WIKI - NA MOSES NTANDU Mwandishi wa Makala hii ni Mwandishi na Mtafiti katika Kituo cha kutoa Taarifa Tanzania (TCIB) anapatikana kwa namba 0714 840656 na Baruapepe mosesjohn08@yahoo.com.

TANZANIA ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo kwa miaka mingi zimekuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine barani humu, na hata nje ya Bara hili kwa mfumo bora wa kiutawala na hata hulka ya umoja na mshikamano toka kupata uhuru.

Hii ni kutokana na misingi imara iliyowekwa na wazee wetu waliopigania uhuru na kuliongoza Taifa hili wakiongozwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere. Wazee hawa walisimama kidete kutetea na kusimamia masilahi ya taifa hili kwa maadili ya hali ya juu.

Kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ninaweza kudiriki kusema kuwa kumekuwa na kuyumba kwa maadili kwa baadhi ya viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza taifa letu katika nafasi tofauti za kiutawala.

Kuyumba huku kwa nidhamu ya kimaadili kwa baadhi ya viongozi wetu kumesababisha kuwa na mdororo wa maendeleo ya kiuchumi na hata kisiasa, kwani kumeonekana na pia kumekuwa na kutoaminiana kwa viongozi wa kisiasa, jambo ambalo limekuwa likikwamisha mambo mengi sana mema ya kitaifa hasa yale yanayogusa maslahi ya umma.

Miongoni mwa jambo kubwa ambalo limegharimu fedha nyingi za umma na bado liko katika sintofahamu kubwa kutokana na kutoaminiana na kuyumba kwa umoja wa kitaifa, ni zoezi la kuandikwa na kuanza kutumika kwa Katiba mpya hapa Tanzania. Katika hali ya kawaida kuna haja ya msingi ya kuwepo na katiba mpya kutokana na wakati na hali halisi ya kiutawala, kwani tumekuwa tunatumia katiba ambayo iliandaliwa miaka 40 iliyopita.

Licha ya katiba yetu tuliyonayo ambayo ni ya mwaka 1977 kufanyiwa marekebisho mara kadhaa, bado inaonesha kuna haja ya kuja na mfumo bora zaidi utakaoendana na kasi na hali halisi ya kiutawala, katika hali ya kawaida kuna mabadiliko mengi yaliyokwishatokea ya mfumo wa utawala, uchumi na hata masuala mengi ya kijamii ambayo yanahitaji mfumo mpya wa katiba ambao utaendana na hali halisi ya sasa.

Julai 26 mwaka huu niliandika makala juu ya upatikanaji wa katiba mpya nikieleza ahadi ya chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015, ikiahidi kwamba hadi kufikia mwaka 2020 itakuwa imekamilisha mchakato wa uandikaji wa katiba mpya na kuanza kutumika kabla ya kufikia uchaguzi mkuu ujao hapo mwaka 2020.

Ahadi hii imeainishwa katika ilani ya uchaguzi ya chama hicho kinachoshika dola kwa sasa hapa nchini, katika sura ya saba kwenye kipengele cha G na H imesema kuwa chama kitahakikisha kinafanya yafuatayo;- “(g) Kukamilisha mchakato wa kutunga katiba mpya na kuanza kuitekeleza kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba na (h) kuendelea kuimarisha mfumo wa kujitathmini kiutawala bora (APRM) na kutekeleza mapendekezo yaliyomo katika ripoti zake za mara kwa mara.”

Katika ilani ya chama imekwenda mbali na kuonesha utayari wa chama kukubali mfumo bora wa kujitathmini katika mfumo wa kiutawala, yaani demokrasia na mfumo wa utawala bora ambo ni hulka ya chama na Tanzania kwa ujumla wake toka taifa kuwa huru.

Hili ni jambo jema sana kuainishwa katika ilani hii ya chama, lakini hali ikoje katika utekelezaji wake? Hivi karibuni Mkurugenzi mtendaji wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Hebron Mwakagenda, aliainisha kuwa kwa hali ya kawaida matumaini ya utekelezaji wa mchakato huu yameanza kufifia kutokana na majukumu makubwa ya kitaifa yanayotakiwa kutekelezwa tuelekeapo 2020.

Mwakagenda anasema: “Sasa matumaini yameanza kufifia kwani katika mazingira yaliyopo kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kumebaki fursa finyu sana ya kuandaa bajeti ya dharura na kuipitisha katika kipindi hiki cha mwaka 2017.

Hii maana yake ni kwamba ili tuweze kupata katiba mpya kuna nguvu kubwa ya ziada inahitajika na pamoja na serikali kujihimu kwa dhati katika kutekeleza mchakato huu, vinginevyo itakuwa ni ahadi hewa kwani utekelezaji wake utakuwa mgumu sana kwa muda uliosalia kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Naye Mwenyekiti wa Jukata ambaye pia ni Mchambuzi na Mtafiti wa Masuala ya Kisiasa barani Afrika na kwingineko duniani, Deus Kibamba, amebainisha na kufafanua jambo hili katika mahojiano yangu naye ambapo anajibu swali moja kuu ambalo sote tunapaswa kujiuliza ambalo linaweza kuonesha mwelekeo wa mchakato huu muhimu hapa nchini.

Swali;- Unadhani mchakato wa kuandikwa katiba mpya kwa kipindi kilichobakia kuelekea 2020 unaweza kufanyika na tukaweza kupata Katiba mpya na ikaanza kutumia kabla ya kumalizika kwa mhula huu wa kwanza wa awamu ya tano?

Kibamba anajibu;Mchakato wa Katiba Mpya kwa sasa unamtegemea sana Rais John Pombe Magufuli. Hii ni kwa sababu mbili. Kwanza, kikatiba, kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Tanzania ya mwaka 1977, Rais ndiye kila kitu. Ana madaraka makubwa sana. Anaweza kuanzisha na kuua au kufuta michakato, taasisi au idara.

Hilo lenyewe ni sehemu ya mjadala wa katiba. Rais abaki na madaraka kiasi gani? Je, Rais mwenyewe anaweza kufanya mambo gani, hawezi kufanya mambo gani kikatiba? Kenya imefanikiwa sana katika hili, Tanzania bado Rais ana uwezo wa kufanya lolote na kwa wakati wowote (blank cheque).

Kwamba mchakato unaweza kuanzishwa tena, kutokea wapi (upya kabisa? lilipoishia Bunge Maalum la Katiba? Au ilipoishia Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Warioba?) Yote hayo ni maamuzi ya rais. Rais anaweza kuamua kuwa kwa mfano tuendelee na kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa. Rais pia anaweza kuamua kuwa hapana watu wengi wanaonekana kuiguna Katiba inayopendekezwa.

Tuanzie na Rasimu ya Warioba, Rais pia anaweza kutumia busara akasema Watanzania wameonekana dhahiri kugawanyika kati ya wanaotaka tuanzie kwa Warioba ambao ni wengi sana na wale wanaotaka tuanzie kwa Katiba Pendekezwa ya akina Chenge na Mzee Samuel Sitta (marehemu).

Katika hili anaweza kusema sawa naona tuanzie katikati ya hizo rasimu mbili. Akaunda Timu ya Wataalamu wa Masuala ya Katiba, Sayansi ya Siasa, Mifumo ya Utawala na Sheria, wanaofikia kama 10 hivi wakafanya kazi ya kuoanisha rasimu hizo mbili kuona yanayolalamikiwa kutupwa kutoka Rasimu ya Warioba ili yarejeshwe ndipo tuendelee.

Juu ya kwamba ataamua kufanya lolote katika uwezo na nafasi zilizopo na nilizotaja hapo juu au nyingine yoyote, hiyo sasa iko mikononi mwa Rais na washauri wake, kama anao. Jukwaa la Katiba Tanzania limejaribu kumshauri afanye mpango wa kuuanzisha tena mchakato kwa kuanza na nafasi ya Timu ya Wataalamu.

Hivyo ndivyo hali halisi ilivyo katika uwezekano wa kuendelezwa kwa mchakato wa katiba mpya, vinginevyo itatubidi kusubiri hadi baada ya uchaguzi mkuu ujao wa 2020 ili kuangalia uwezekano huo kuwepo kwa awamu ijayo ya utawala huu wa awamu ya tano.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.