Joto la Katiba mpya laanza kupanda

Rai - - MBELE - NA GABRIEL MUSHI

JOTO la uhitaji wa Katiba Mpya limeanza kuonekana kushika kasi katika siku za karibuni baada ya kuibuka kwa baadhi ya viongozi wa dini, wasomi na wanasiasa, wote wakitaka kurejeshwa kwa mchakato huo. RAI linachambua.

Mchakato wa Katiba Mpya ulianza wakati wa Serikali ya awamu ya nne kwa kupita katika hatua kadhaa ikiwemo ya kukusanya maoni na kuitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba, hata hivyo mchakato huo haukufikia hatua ya mwisho ya kupatikana kwa Katiba Mpya.

Kutokana na kukwama kwa Katiba Mpya ndani ya utawala wa Serikali ya awamu ya nne, jamii iliamini kuwa serikali ya awamu ya tano ingemalizia pale palipo salia.

Hata hivyo, Novemba mwaka jana Rais Dk. John Magufuli aliwaambia Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini alipokutana nao kuwa kamwe suala hilo si kipaumbele chake badala yake anataka kuinyoosha nchi kwanza.

Tangu wakati huo hakukuwa na harakati za waziwazi za kuhitaji Katiba Mpya hadi hivi karibuni pale Askofu Severin Niwemugizi wa Kanisa Katoliki Ngara, pamoja na baadhi ya viongozi wa kisiasa akiwamo Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu kujitosa hadharani kuelezea uhitaji wa Katiba mpya.

Askofu Niwemugizi alinukuliwa akisema kuwa yuko tayari “kuitwa mchochezi” endapo juhudi za kudai Rasimu ya pili ya Jaji Warioba haitazingatiwa.

Kiongozi huyo wa dini aliyasema hayo alipokuwa katika mkutano wa zaidi ya asasi 80 za kiraia, ambapo alisema si dalili nzuri kwa Taifa lenye afya njema kushindwa kukamilisha mchakato huo wa Katiba mpya.

“Ni vielelezo vyenye dira mbaya. Imefika wakati tukae kama Taifa tukubaliane kuwa tunataka dira njema ambayo ni Katiba.

“Rais anafanya mengi mazuri na alipoanza kila mmoja aliona dalili za matumaini, lakini juhudi hizo zinaweza zisiwe endelevu kama hakuna ulinzi wa Katiba. “Tunahitaji Katiba tena Katiba nzuri ambayo haitaruhusu kuchezewa na yeyote kwa masilahi au matakwa yake binafsi,” alisema.

Muda mfupi baada ya kauli ya Askofu Niwemugizi, aliibuka Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ambaye alipendekza kufanyiwa kazi suala hilo ambalo bado lipo njia panda.

Nyalandu aliandika ujumbe huo kwenye ukurasa wake wa twitter wiki iliyopita na kusema kwamba sasa nchi ya Tanzania inahitaji katiba hiyo ili kuwe na mipaka ya muingiliano wa kazi kwenye mihimili ya nchi.

“Tanzania inahitaji katiba mpya mihimili ya utawala iwekewe mipaka iliyo wazi, na kuwepo ‘checks and balance’ kwa serikali, bunge, na mahakama”, ameandika Lazaro Nyalandu.

Hatua hiyo imeonekana kuwaamsha baadhi ya wasomi ambao nao wanakubaliana na hoja ya kufufuliwa kwa mchakato wa Katiba Mpya ili ukamilike kwa asilimia 100.

Hoja yao ni kwamba kwa sasa nchi inahitaji Katiba Mpya ili kulinda mema yote yanayofanywa sasa na Rais Magufuli ili baadaye yasijekuvurugwa na uongozi utakaofuata.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wameenda mbali zaidi na kubainisha kuwa si kwamba nchi haina Katiba, bali inayotumika sasa inatakiwa kubomolewa ili iwe nyenzo ya kusimamia mazuri anayoyanyoosha Rais Magufuli.

Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Profesa Mwesiga Baregu pamoja na mambo mengine alisema ni kweli nchi inahitaji Katiba Mpya kwani hamasa ilioanzishwa na Tume hiyo ya Jaji Warioba haiwezi kuishia hewani.

Akizungumza na RAI mwanzoni mwa wiki hii Profesa Baregu alisema mchakato wa kutunga Katiba Mpya haukumalizika licha ya kwamba kazi kubwa ilifanyika.

“Hamasa iliyoanzishwa na ile Tume ya Jaji Warioba bado haijafa, mchakato huu wa Katiba mpya bado umening’inia hewani. Ule msingi ulioanzishwa na tume hiyo bado unapaswa kutekelezwa. Tunaona kuwa Rais Magufuli alipoingia madarakani alisema kwamba Katiba mpya si kipaumbele chake, lakini haya yanayoendelea katika kukiuka taratibu na kanuni Watanzania wanakuwa na wasiwasi ndio maana wameamka sasa ili kujua kwamba tunaenda wapi.

“Kwa sababu Rais anasema anataka kuinyoosha nchi, atainyoosha vipi nchi ili hali hayo mambo mazuri anayotaka kuyatekeleza hayalindwi na Katiba? ina maana mtu mmoja au kikundi cha watu kinaweza kuinyoosha nchi bila wananchi kuridhia kwa kupitia Katiba waliyoitaka! Katiba mpya ndio nyenzo ya kumsaidia kuinyoosha nchi hivyo nadhani Watanzania wameanza kushtuka ndio maana hata sasa kuna vipande vya video vinavyomuonesha Mwalimu Nyerere akisisitiza umuhimu wa kufuata Katiba,” alisema.

Aidha, alisema wananchi si kwamba wanahitaji Katiba Mpya tu, bali wanahitaji Katiba inayotokana na rasimu ya pili ya tume ya Jaji Warioba.

“Lazima tuende mbele badala ya kuangalia tulipojikwaa tusonge mbele kwa kuendeleza hiyo rasimu si ile Katiba pendekezwa ambayo ilitufanya tujikwae na kuanguka,” alisema.

Mhadhiri Mwandamizi wa kitivo elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaama, Dk. George Kahangwa alisema suala la Katiba Mpya limekuwa hoja ya muda mrefu ambayo inaibuka kila mara hivyo inaonesha kuwa ni kwa shauku gani watanzania waliyonayo dhidi ya uhitaji wa Katiba hiyo.

“Katiba mpya ni hoja ambayo haijawahi kufa. Hata katika imani watu wanasubiri mbingu mpya na imani hiyo haijawahi kufifia. Ndio maana tunaona kuwa shauku ya uhitaji wa katiba mpya bado ipo licha ya Rais Magufuli kusema kuwa si kipaumbele chake.

“Katika kipindi cha Kikwete (Rais wa awamu ya Nne Jakaya Kikwete) watu hawakujua pa kuendelea, lakini sasa tumeona watu wamejitokeza na kuzungumza kwa ujasiri mkubwa nawapongeza sana kwa hilo,” alisema.

Alisema watanzania wameileta hoja ya Katiba mpya katika muktadha wa sasa licha ya kwamba wanaheshimu yale mazuri anayoyafanya Rais Magufuli wanaona kabisa utawala utakaokuja siku zijazo unaweza kuyaharibu hayo mazuri kwa sababu hakuna Katiba inayoyalinda.

“Lakini pia watu wameamka kutokana na kujifunza yaliyojiri kutoka kwa majirani zetu Kenya ambapo tumeona kuwa mahakama imekuwa na uwezo wa kufuta matokeo ya uchaguzi. Ni jambo ambalo limeonesha kwa namna gani Katiba ikiheshimiwa inakuwa na nguvu yenye manufaa kwa wananchi,” alisema.

Katika kuonesha haja ya Tanzania ya sasa kuwa na Katiba Mpya, Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Pius Msekwa alipata kunukuliwa kwenye vyombo vya Habari akisema kuwa wakati wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais mahakamani umeshafika na kilichobaki ni kupitisha rasimu ya Katiba ambayo ina ibara inayotoa haki hiyo.

Msekwa ambaye pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekitiwa CCM Bara, alisema Katiba ya sasa hairuhusu, lakini Katiba inayopendekezwa imeruhusu na kinachosubiriwa ni kura ya maoni.

Aidha, Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva nae alipata kusema kuwa mchakato wa Katiba mpya unatakiwa kuendelezwa na Tume hiyo kwa kuwa ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia mchakato huo.

Katika mahojiani maalumu aliyowahi kuyafanya na gazeti hili Lubuva alisema “Kwanza nina imani pale nilipoachia pataendelezwa kwa sababu wengi niliowaacha bado hawajamaliza muda wao, Ombi langu tuendelee kuwapa ushirikiano wale niliowaacha. Kwa sababu wataweza kufanya vizuri zaidi kwani wataendelea kuongozwa na sheria jinsi zilivyo,” alisema.

Mchakato wa kubadili Katiba ulianzishwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka 2011 lakini ukakwama mwaka 2014 ukiwa katika hatua ya kura ya maoni baada ya NEC kueleza kuwa haikuwa na muda wa kutosha .

Hata hivyo, mchakato huo uliingiwa na dosari baada ya baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba, hasa kutoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD kuususia wakidai kuwa chombo hicho kiliacha Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuingiza ajenda za chama tawala.

Pamoja na kususa huko kwa wapinzani, lakini wajumbe waliosalia waliendelea na mchakato na kupitisha Katiba Inayopendekezwa.

Jaji Damian Lubuva

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.