AU iache kuwa kundi la kulindana wezi wa kura

Rai - - MAONI/KATUNI -

Hali ya kulindana kwa kukithiri iliyomo ndani ya serikali nyingi Barani Afrika ndiyo sasa hivi imo pia katika Umoja wa Afrika (AU) – muungano uliobuniwa miaka 16 iliyopita kusimamia masuala ya Afrika, yakiwemo ya uchumi, maendeleo, siasa, amani na mengineyo.

Masuala ya siasa na amani, ambayo yana uhusiano mkubwa, ndiyo masuala yanayouumisha kichwa umoja huo kwani migogoro mbali mbali ikiwamo ile inayozua vita vya wenyewe kwa wenyewe inakosa ufumbuzi – na hivyo kulifanya Bara la Afrika – pamoja na utajiri wake mkubwa wa mali ya asili – kubaki nyuma katika masuala mengi ya maendeleo. Hii huthibitishwa na takwimu mbali mbali zitolewazo kwa kulilinganisha na Mabara mengine.

Kwa kuhofia kile kinachoweza kuwafika kutoka kwa watawala watarajiwa, watawala wengi waliopo madarakani wamekuwa hawakubali katu kuachia ngazi hivi hivi, na demokrasia waliyolazimishwa baada ya miongo kadha ya utawala wa kidikteta wa chama kimoja wameifinyanga ili iwahakikishie kubakia madarakani.

Wako tayari kuziingiza nchi zao katika mfarakano mkubwa, pamoja na vita ya wenyewe kwa wenyewe kuliko kuachia ngazi na hatimaye wakajikuta wanasimamishwa vizimbani.

Hayo tumeyaona katika nchi kadha, na mfano mzuri wa jirani na kwetu ni Zambia. Serikali ya nchi nyingine zilizowahi kuwasimamisha vizimbani watawala wao wa zamani na baadhi yao kuwahukumu ni Ghana, Ethiopia, Chad, Mauritania, Mali, Liberia, Sudan, Rwanda na Sierra Leone.

AU haiwezi kutatua mgogoro wowote Barani hapa kwani wengi wa viongozi wake wamejikita katika uporaji wa mali za wananchi wao. Kama nilivyosema, sasa hivi Umoja huo umeanza mtindo wa kulindana – yaani kama kiongozi mmoja wa nchi mwanachama kazusha mfarakano nyumbani kwake kutokana na masuala ya demokrasia na chaguzi, basi viongozi wenzake katika AU humlinda kwa kutumia njia ya kutomkaripia.

Tofauti moja kubwa imejitokeza kule Gambia, lakini hata katika mfano huo mgogoro haukutatuliwa kutokana na jitihada za AU – jitihada kubwa za kumuondoa madarakani Yahya Jammeh aliyedhamiria kupora ushindi zilifanywa na Umoja wa wa kiuchumi wan chi za magharibi mwa Afrika – ECOWAS.

Lakini hebu fikiria: Katika viongozi wa nchi 53 zinazounda Umoja huo, ni vigumu kupata angalau hata viongozi watano ambao wako madarakani nchini mwao kwa njia ya demokrasia iliyo ya wazi na inayokubalika, na kwamba uchaguzi wake ulikukuwa hauna dosari kabisa.

Na hapa neno “uchaguzi” namaananisha uhuru wa siasa katika uwanja ulio na usawa (level playing field) uandikishaji wa wapiga kura usio na dosari, tume huru za uchaguzi ambazo huendeshaji usimamizi wa haki wa uchaguzi -- usimamizi usiokuwa na upendeleo, na kadhalika, na kdhalika.

Mimi nadhani idadi ya viongozi watano niliyotaja kwamba ni halali ni wengi sana. Sasa kama hali ni hiyo, kuna kiongozi gani wa nchi mwanachama wa AU anayeweza kudiriki kumwambia mwenzake “wewe bwana uliiba kura nchini mwako.”

AU ilipoanzishwa, na kwa kuzingatia udhaifu na mapungufu yaliyokuwapo katika chombo kilichotangulia, yaani Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) kulionekana umuhimu wa kuwapo kwa namna ya viongozi wa nchi kujiwekea nidhamu.

Ukawekwa mkataba wa hiari (Peer Review Mechanism) baina ya nchi wanachama kama mpango wa kujiratibu wenyewe kwa wenyewe kwa lengo la kuwepo kwa usawa katika masuala ya siasa, uendeshaji wa utawala bora na uchumi, na maadili yaliyo safi.

Kwa bahati mbaya mpango huu ulifeli mtihani wa kwanza kabisa wakati wa mgogoro wa uchaguzi nchini Madagascar mapema mwaka 2002. Mgogoro huo haukuwa na tofauti sana na ule wa Kenya wa 2007.

Kiongozi wa zamani Didier Ratsiraka, aliyeshindwa uchaguzi na mpinzani wake Marc Ravalomanana, hakuonyesha maadili mema ya kuachia ngazi. Na hata hivyo kulikuwepo mgawanyiko mkubwa ndani ya viongozi wa nchi wanachama wa AU kwani kuna baadhi yao, kama vile Rais Levy Mwanawasa wa Zambia (marehemu), walimmuunga mkono Ratsiraka.

Mgogoro ulikuja kutatuliwa na nchi iliyokuwa koloni la nchi hiyo, Ufaransa, ilipofanikiwa kumshawishi (pia inasemekana kwa kutumia misuli kidogo) Ratsiraka abakie uhamishoni nchini mwake (Ufaransa).

Hii inadhihirisha moja kwa moja kwamba nchi za nje, hususan za Magharibi na hasa zilizokuwa makoloni ndiyo bado zenye uwezo wa kutatua mogogoro inayoanzishwa na watawala wa hovyo Barani humu.

Tumeona hivi majuzi tu jinsi Jumuiya ya Madola (Commonwealth) za nchi zilizokuwa makoloni ya Uingereza ilivyofanikiwa kuepusha mgogoro wa kisiasa nchini Zambia kabla ya kukua pale Katibu wake mkuu alivyoweza kuushawishi utawala wa Rais Edgar Lungu kumuachia kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Hakainde Hichilema.

Kuhusu Kenya, baada ya kupora ushindi katika uchaguzi mwaka 2007 aliyekuwa rais wa nchi hiyo Mwai Kibaki wa Kenya alihudhuria mkutano wa kila mwaka wa AU huko Addis Ababa na na kutoa hotuba ambayo kusema kweli haikuwa katika kusaidia usuluhishi wowote nchini mwake – kwa maana ya kwamba kiongozi huyo aliyepora urais waziwazi alijiona kisha tambuliwa na AU.

Na baada ya hapo msemaji mkuu wa ‘serikali’ yake – Alfred Mutua alijitapa katika mahojiano ya redio – kwamba hakuna haja tena ya usuluhisho nchini mwake isipokuwa Raila Odinga “akubali tu kwamba alitaka kunyakuwa nchi kwa nguvu – kitu ambacho hakikubaliki.”

Ajabu ni kwamba viongozi wa AU, hata kama waliona umuhimu wa kumruhusu Kibaki kuhudhuria kikao, si haidhuru basi wangemwalika pia Raila naye ahudhurie na aseme ya upande wake? Hiyo ni iwapo AU ilikuwa inaamini kuna mgogoro wa kisiasa nchini Kenya unaotakiwa kutatuliwa.

Kulikuwa ugumu gani kumwambia Kibaki: “Samahani sana, hali iliyoko nchini mwako hairidhishi hata wewe kuja hapa, kwanza kuna Kofi Annan kule umemwacha solemba, rudi kwanza kayamalize yale uliyoyanzisha.”

Walishindwa kumwambia hivyo na badala yake wakampa jukwaa na kujisikia kwamba “kumbe wananitambua, usuluhisho wa nini?”

Ukawekwa mkataba wa hiari (Peer Review Mechanism) baina ya nchi wanachama kama mpango wa kujiratibu wenyewe kwa wenyewe kwa lengo la kuwepo kwa usawa katika masuala ya siasa

Aliyekuwa Rais wa Gambia, Yahya Jammeh.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.