TAMASHA LA FIESTA 2017

liwe chachu ya kuibua vipaji zaidi

Rai - - MICHEZO - NA MWANDISHI WETU

BAADA ya kurindima mjini Tabora na Kigoma mwishoni mwa wiki iliyopita, tamasha la kubwa la muziki la Tigo Fiesta 2017, linahamia Nyanda za Juu Kusini katika mikoa ya Njombe na Iringa mwishoni mwa wiki hii.

Tamasha hilo hadi sasa limeshapita katika miji ya Arusha, Musoma, Kahama, Mwanza, Tabora na Kigoma ambapo kwa mujibu wa waandaaji, jumla ya miji 15 itapata uhondo wa tukio hilo la burudani la kila mwaka, ukiwamo Mkoa wa Njombe.

Na linapotarajiwa kupiha hodi Nyanda za Juu wikiendi hii, wapenzi wa burudani wa maeneo hayo, wanashauku kubwa kuona ni wasanii gani watakaofunika, lakini pia nyimbo ambazo zitabamba zaidi.

Kama ilivyokuwa katika miji iliyopitiwa na tamasha hilo ambalo mwaka huu limepata udhamini wa nguvu kutoka kampuni ya Tigo Tanzania, wasanii waliopo katika orodha ya watakaotumbuiza Nyanda za Juu ni wazi hawatakuwa tayari kuwaangusha wakazi wa huko kwa kuhakikisha wanafanya shoo ‘bab kubwa’ kukonga nyoyo zao.

Wasanii ambao wameacha vumbi katika maeneo yaliyopitiwa na Tigo Fiesta mwaka huu, miongoni mwao ni Ali Kiba na wimbo wake wa Seduce ME, Roma na Darasa wanaounda umoja uliopewa jina la Rostam, Nandy, Chege, Ben Pol na rafiki yake Jux.

Wengine ni Darasa, Joh Makini, Mr. Blue, Fid Q, Shilole, Maua Sama, Ommy Dimpoz, Ney wa Mitego, Young Dee, Aslay, Msami na wengineo.

Lakini pamoja na burudani kutoka kwa sanii watakaopanda jukwaani Tigo Fiesta Njombe kesho na Iringa Jumapili, tamasha hilo mwaka huu linatarajiwa kutoa fursa nyingine kwa wasanii chipukizi kuibukia kupitia tukio hilo la burudani.

Bahati nzuri, tamasha hilo tayari limefanikiwa kuibua vipaji lukuki vya muziki ambavyo awali havikuwa vikijulikana, mifano hai ikiwa ni kwa wasanii kama Rubby, Young Killer, Nay Lee, Edo Boy na wengineo wengi.

Na kwa kuwa tamasha hilo linaambatana na tukio dogo la kusaka vipaji la Tigo Fiesta Super Nyota, ni wazi kila mji litakapofanyika, litaondoka na msanii mmoja kama si zaidi wenye kipaji na mwisho wa siku kuendelezwa kuweka kufikia mafanikio ya wakali wa Bongo Fleva kama Diamond Platnumz, Ali Kiba, Nandy na wengineo.

Akizungumzia tamasha hilo la mwaka huu, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Tigo, William Mpinga, anasema kuwa tamasha hilo lenye kaulimbiu ya ‘Tumekusomaa’ ambalo ni la 16, limepangwa kurindima katika miji 15 ambayo ni Arusha, Musoma, Kahama, Mwaza, Tabora, Kigoma, Dodoma, Iringa, Songea, Njombe, Sumbawanga, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Mtwara na kuhitimishwa jijini Dar es Salaam.

“Kupitia Tigo Fiesta 2017Tumekusoma, Tigo imejikita kuinua vipaji vya wasanii wa Kitanzania kama njia mojawapo ya kukuza sanaa nchini. Kama tunavyojua, sanaa imekuwa mojawapo ya nafasi kubwa za ajira kwa vijana wetu na baaadhi ya wasanii wetu pia wamepata nafasi ya kuperusha bendera ya nchi katika nchi za kigeni, kwa hiyo kusaidia kuitangaza nchi yetu.

“Tuna imani kuwa kupitia ushirikiano huu tutaweza kuwakutanisha wasanii wetu na mashabiki wao, kuwajengea uwezo na hivyo kuwasaidia wasanii wengi zaidi kufikia viwango vya kimataifa,” anasema Mpinga.

Kwa msimu uliopita, kampuni ya simu za mkononi ya Tigo ilitoa msaada wa madawati zaidi ya 5,700 kwa maeneo yote ambayo tamasha la Fiesta lilifanyika, madawati hayo yaliweza kufanikisha adhma ya serikali ya kumuinua mtoto toka kukaa sakafuni hadi dawatini.

“Kwa mwaka huu nguvu nyingi tunazielekeza katika kuhakikisha kwamba mtandao wetu unakuwa na nguvu zaidi za kuweza kuzikabili changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikitokea katika maeneo mengi nchini, hii itatuwezesha sisi kuwa mtandao bora na pendwa kwa Watanzania bila kujali maeneo waliyopo,” aliongeza Mpinga.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Fiesta, Sebastian Maganga, anasema kuwa wakazi wa maeneo yatakayofikiwa na tamasha hilo, watarajie shoo kabambe na ya aina yake kutoka kwa wasanii wao wakali wa hapa nchini.

“Tunawaletea wasanii wenye hadhi kulingana na mapendekezo ya mashabiki husika wa mkoa huo, tena wale waliojizolea sifa ndani na nje ya nchi,” anasema Maganga.

Nandy akiwa jukwaani

Aslay akitoa burudani

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.