‘Vijeba’ kujitosa Fainali za Kombe la Dunia U-17?

Rai - - MICHEZO KIMATAIFA - HASSAN DAUDI NA MITANDAO

FAINALI za Kombe la Dunia kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, zinatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii nchini India. Michuano hiyo, ambayo ni ya 17 tangu kuanzishwa kwake, itashirikisha mataifa 24 na itachezwa kwenye miji sita badala ya 10 kama ilivyokuwa imependekezwa hapo awali.

Wenyeji India wako Kundi A wakiwa na Ghana, Colombia, Marekani na India, ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kung’ara kwenye fainali hizo.

Licha ya kwamba michuano hiyo itafanyika kwao, mashabiki wa soka nchini India hawatakuwa wakitarajia makubwa kwenye kundi hilo, hasa kutokana na rekodi ya mataifa hayo kwenye ulimwengu wa soka.

Kwanza, zitakuwa ni fainali za sita kwa Colombia ingawa itakuwa ni kwa mara ya kwanza tangu waliposhiriki zile zilizofanyika Nigeria mwaka 2009, ambapo waliweza kushika nafasi ya tatu. Kwa upande wao, Ghana wamekuwa na uzoefu mkubwa pia kwenye fainali hizo kwani wameshiriki mara tisa kuanzia zile zilizofanyika Scotland mwaka 1989.

Mbali na kushiriki, pia imebeba taji hilo mara mbili (1991 na 1995) na kumaliza nafasi ya pili mara kadhaa. Hata katika fainali za mwaka 1999 nchini New Zealand, Ghana walishika nafasi ya tatu.

Marekani nao ni wakongwe kwani wamekuwa wakishiriki mashindano hayo mara nyingi tangu yalipoanishwa mwaka 1985. Ni mwaka 2013 tu ndipo walizikosa fainali hizo lakini za mwaka huu zitakuwa za 16.

Kwa rekodi za mataifa hayo, ni wazi India watakuwa na kibarua kigumu kuvuka hatua ya makundi na kisha kufanya maajabu kwenye ardhi yao ya nyumbani, japo hakuna linaloshindikana katika mchezo wa soka.

Kuelekea fainali hizo zitakazoanza wiki hii, kuna taarifa ya Kocha wa India, Luis Norton de Matos, amelazimika kukipangua kikosi chake baada ya mmoja wa wachezaji kugundulika kuvuka umri wa miaka 17. Tayari Mreno huyo alishaandaa ‘jeshi’ lake la makinda 21 lakini alilazimika kulipangua na kumwacha mchezaji huyo.

Tukio hilo linaakisi jinsi ambavyo michuano ya vijana imekuwa ikikumbwa na kashfa kubwa ya wachezaji waliozidi umri. Mfano mzuri ni fainali za mwaka huu za Mataifa ya Ulaya kwa vijana wenye umri chini ya miaka 21 (Euro U-21).

Katika mchezo wa hatua ya robo fainali, ambao England waliibuka na ushindi dhidi ya Poland, kulikuwa na madai kuwa kulikuwa na wachezaji waliozidi umri ‘vijeba’ kwenye kikosi cha England. Ilielezwa kuwa nyota wanne walikuwa na umri wa miaka 23 na tayari walikuwa na zaidi ya mechi 170 za Ligi Kuu England.

Lakini pia, kuelekea fainali za AFCON kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 zilizofanyika Gabon mwaka huu, jumla ya wachezaji 26 wa kikosi cha timu ya Taifa ya Nigeria waligundulika kuwa ni ‘vijeba’. Ikumbukwe kuwa Nigeria walikuwa ndiyo mabingwa watetezi.

Hata hivyo, hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Nigeria kuingia kwenye kashfa hiyo kwani hata Rais wa zamani wa Chama cha Soka nchini humno (NFF), Anthony Kojo Williams, alikiri kuwa umekuwa ni utamaduni wao kwa miaka mingi.

“Huwa tunatumia wachezaji waliozidi umri kwenye michuano ya vijana, nalijua hilo. Kwanini hatulisemi hilo? Huo ndiyo ukweli. Huwa tunadanganya. Ni kweli kabisa. Unapodanganya, unawanyima haki vijana wanaotakiwa kucheza michuano husika,” alisema bosi huyo.

Hata mwaka 2013, Nigeria ililazimika kuwaacha wachezaji wake muhimu katika fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17, baada ya kugundulika kuwa walivuka umri huo. Mmoja kati ya wachezaji waliokutwa katika janga hilo ni Abuchi Obinwa anayeishi Marekani.

Kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), mchezaji anayetakiwa kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wenye umri huo ni yule aliyezaliwa kabla ya Januari Mosi, 2000.

Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 itakayoshiriki fainali za Kombe la Dunia 2017 nchini India.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.