JPM na kauli 7 nzito

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

RAIS Dk. John Magufuli juzi alifungua Mkutano Mkuu wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), pamoja na mambo mengine ametoa kauli saba nzito ambazo baadhi yake zimeibua mjadala.

Katika mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na baadhi ya wakuu wa mikoa, wabunge, mameya na madiwani, Rais Magufuli alielezea mambo yaliyofanyika katika kipindi chote cha utawala wake pamoja na yale anayotarajia kuyafanya ili kuwaletea maendeleo Watanzania.

Rais aliweka wazi kuwa miongoni mwa watu wanaomtukana mitandaoni ni wale watumishi waliokuwa na vyeti feki na kwamba wala hababaishwi na hilo.

Miongoni mwa kauli hizo ni 1. Watumishi waliokuwa na vyeti vya kughushi ndio wanaonitukana mitandaoni. Sibabaishwi, nikiona najua hawa ndio wale 12,000 wa vyeti feki wanahangaika.

2. Rais aliwatahadharisha Wakurugenzi walevi na kuwataka wajirekebishe vinginevyo atawavua madaraka yao.“Nina taarifa kuna wakurugenzi watano wa Halmashauri ni walevi, hawa lazima nitawaondoa.

3. Kuhusu kupunguza matumizi ya Serikali Rais Magufuli alisema wapo watumishi walikuwa wakilipwa mishahara hadi ya sh. milioni 40 wakati yeye mshahara wake ni sh. milioni tisa kwa mwezi.

“Kuna taasisi za umma, zilikuwa zinafanyia mikutano ya bodi nje ya nchi. Wakiwa huko wanapandishiana mishahara hadi milioni 40, mimi mshahara wangu ni milioni 9 tu kwa mwezi. Sasa nimezuia mikutano ya bodi kufanyika nje, waliokuwa wananufaika hawawezi kunipenda, lakini nikipendwa na mke wangu inatosha, sikuja ikulu kuuza sura.”

4. Kuhusu Serikali kuhamia mkoani Dodoma, Rais alisema hadi kufikia mwakani Serikali yote itakuwa imeshahamia huko kwani tayari Waziri Mkuu yuko huko.

“Makamu wa Rais amebakiza miezi miwili tu ahamie Dodoma, mimi nitahamia mwakani, halafu nione ambaye atabaki Dar es Salaam, atanieleza.

5. Kwa upande wa kupandisha mishahara, amesema hajachaguliwa kupandisha mishahara. “Sijapandisha mishahara ya watumishi na sitapandisha kwa sababu sikuchaguliwa kupandisha mishahara. Nilichaguliwa kusaidia wananchi wanyonge wapate huduma, jukumu langu ni kutoa huduma kwa wananchi.”

6. Rais amemsifia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kusema kuwa amekuwa ni mchapa kazi na kutaka aigwe na wenzake.

“Makonda ni mchapakazi. Hata kama hajui kusoma hata herufi A, lakini kwa sababu anakamata madawa ya kulevya basi huyo ni msomi mzuri sana.

7. Katika kauli hizo saba Rais alisema kama Diwani anajiona hana kazi ya kumwingizia kipato ni vema akajiweka kando. “Kama kuna diwani ambaye hana kazi ya kujiingizia kipato ajiuzulu udiwani haraka,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.