MAHAKAMA ZA WATOTO PASUA KICHWA

Rai - - MBELE - NA OSCAR ASSENGA, TANGA

KUTOKUWA na uwakilishi wa kisheria katika mahakama za watoto wanaokinzana na sheria, kimekuwa kikwazo kikubwa kupata haki ambayo wanastahiki kupatiwa. Jambo hili limesababisha watoto wengi kuhukumiwa kutumikia adhabu mbalimbali.

Hali hiyo pia imesababisha maumivu makubwa kwa jamii hasa baada ya ndugu na jamaa zao kulazimika kuwa kizuizini kutokana na makosa mbalimbali ambayo huenda ametenda, anatuhumiwa au amesingiziwa.

Uwepo wa changamoto hiyo kubwa kwa watoto umekipelekea Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) mkoani Tanga, kutoa elimu juu ya namna ya utoaji wa msaada wa kisheria kwa watoto walio katika ukinzani na sheria kwa wadau wake kwenye masuala ya watoto walio katika ukinzani na sheria.

Licha ya kutoa elimu hiyo, chama hicho pia kinatoa msaada wa kisheria kwa watoto walio katika ukinzani na sheria kwa kuwapatia wanasheria wa kuwawakilisha mahakamani kupitia mpango wake wa Pro bono.

Kupitia mpango wake huu wa Pro bono, Tawla iliwezesha kumpatia msaada wa kisheria mtoto, Sophia John Komba (17) ambaye alituhumiwa na kosa la mauaji ya kondakta wa daladala inayofanya safari zake kati ya Nguvumali na Raskazone. Mtoto Sophia aliwekwa kizuizini tangu Januari mwaka huu katika kituo cha mahabusu ya watoto.

Binti huyo ambaye ni mtahiniwa wa mtihani wa kidato cha nne, alitakiwa kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka huu lakini alishindwa kwenda shule kutokana na kukabiliana kesi ambayo yeye na baba yake mzazi zinawakabili.

Mratibu wa Chama cha Wanasheria Wanawake mkoani Tanga (Tawla), Mwanasheria Latifa Mwabondo, anasema Tawla kupitia mradi wake wa utoaji wa msaada wa kisheria kwa watoto na wanawake waliokuwa katika ukinzani na sheria, aliembelea mahabusu ya watoto ili kuweza kujua idadi ya watoto walio katika ukinzani na sheria na kujua makosa yanayowakabili ili kuwapatia msaada wa kisheria.

Anasema walipoanza kufuatilia walielezwa watoto watatu ambao walikuwa na makosa tofauti kama mauaji, wizi wa kutumia silaha na wizi bila kutumia nguvu ambapo watuhumiwa wamewekwa katika mahabusu ya watoto.

Baadaye walipokwenda mahabusu ili kuweza kupata maelezo ya kesi ili kuwapatia uwakilishi, waliambiwa amebaki mtoto Sophia John ambaye alikabiliwa na kesi ya mauaji ya kondakta wa daladala jijini Tanga.

“Kwa sababu ni mtoto na chama hicho kwa sasa kinaendesha mradi wa uwezeshaji wa msaada wa kisheria kwa watoto na wanawake walio katika ukinzani wa sheria, tukaona ni bora tumpatie msaada wa kisheria,” anasema.

Anasema Tawla walifuatilia kesi na kuelezwa bado kesi ipo kwenye hatua ya upelelezi. Na baadaye wakampatia mwanasheria ambaye atakuwa na binti huyo ili kumhoji maswali kwa sababu habari walizozisikia ni tofauti na zinazoelezwa.

Anaeleza kuwa siku kesi hiyo ilipotajwa walikwenda mahakamani wakawa pande zote mbili na wanasheria kwa kuongeza kuwa wapo tayari kumtetea binti huyo katika kesi iliyokuwa na watoto watano huku yeye akiwa watatu.

“Tuliamua kumtetea kwa sababu yeye ni mtoto na ana haki zake za msingi, ambapo tuliiomba mahakama ili kuharakishwa kwa upelelezi wa kesi hiyo kwa kuwa mshtakiwa ni mwanafunzi mtahiniwa wa kidato cha nne. Ambapo alinishauri kukutana na upande wa waendesha mashtaka na wapelelezi ili kufanya upelelezi wao haraka baada ya kuambiwa faili lake lipo kwa RCO,” anasema.

Anasema kesi ilipopangwa kwa mara nyingine, wao walimwakilisha wakiongozana nawakiliTumainiBakariambaye ndiye atakayemwakilisha katika kesi hiyo, ambapo katika utetezi wakili wa chama hicho waliomba upelelezi uharakishwe.

Wakili huyo alitaka jambo hilo kufanyiwa haraka kwa kuwa mtoto huyo ni mtahiniwa na alikuwa anatakiwa kuwepo shuleni wakati huo kwa matayarisho ya mitihani na pili kujua hatima ya mteja wetu kama ana kesi ya kujibu au la.

Anaeleza baada ya hilo hakimu alihimiza upande wa waendesha mashtaka wahimize upande wa upelelezi kufanya upelelezi mapema ili kutoa nafasi ya kusikilizwa kesi hiyo.

Latifa anasema walihimiza upande wa utetezi wamshirikishe Ofisa Ustawi wa Jamii kufuatilia usahili wa mtuhumiwa kama umefanyika na awepo mahakamani kwa siku ya kesi inayofuata na taarifa kamili kwa lengo la kujua huyo mtoto amepewa namba ya kufanya mtihani.

Aliongeza kuwa walipoenda mahakamani kwa mara ya tatu mambo yakawa ni yale yale. Ila ofisa ustawi wa jamii alitoa taarifa ya kwamba mtuhumiwa alikuwa ametahiniwa.

Agosti 14, mwaka huu kesi ilitajwa tena ambapo mratibu huyo anasema walipofika mahakamani, walifika mbele ya hakimu na upande wa mwanasheria wa Serikali walisema wamepitia faili wakaona mshtakiwa namba tatu ambaye ni mtoto Sophia John kwamba hana kesi ya kujibu.

Anaeleza upande wa waendesha mashtaka walifuta shtaka kupitia kufungu 91 (1) ya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

Anaeleza baada ya hapo wakamchukua na kumpelekea Kituo cha Polisi cha Chumbageni ili kumtoa alama za vidole (Finger Print) na baadaye kumpeleka kwenye mahabusu ya watoto kwa makubaliano ya wazazi na polisi.

“Kwa ajili ya usalama wa mtoto, Tawla na Ustawi wa Jamii walikubaliana na familia ya kwamba wakati huo Sophia hawezi kwenda kuishi na familia yake kwa sababu za kiusalama. Mpaka hapo atakapohakikishiwa usalama wake,” anasema.

Anasema kwa sasa Sophia kulingana na mkasa alioupitia hayuko vizuri kisaikolojia na muda wa matayarisho wa mitihani ni mdogo sana kwake.

Anasema kwa kushauriana na ustawi wa jamii, ikaonekana ni vizuri kupitia ustawi wa jamii kuandikwe barua itakayoambatanishwa na maamuzi ili kuliomba Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kuahirisha mitihani ili aweze kufanya mwakani kwa sababu alikuwa kuzuizini na hakupata muda wa kusoma.

Akizungumzia changamoto kuhusu kesi hiyo, anasema kosa ambalo lilisababisha Sophia kufikishwa katika kituo cha mahabusu ya watoto ni kubwa, hivyo mtoto huyo hakupata nafasi ya kuendelea kusoma wala kupata walimu ambao wangeweza kumwendeleza kimasomo.

Aidha, Sophia anasema: “Baada ya kuachiwa huru nimekuwa nikishinda nyumbani wakati wakiangalia sehemu salama ya kwenda kuishi kwa sababu jamii wananiangalia kama muuaji.

“Nimekuwa nikiitwa majina mengi kama muuaji, malaya kwa sababu ya kile kilichotokea na hali hii imekuwa ikiniumiza sana na kukosa amani.

“Katika jambo hilo nawashukuru watu wote kwa kunipa ushirikiano wao likiwemo Jeshi la Polisi, Mahabusu ya Watoto, Ustawi, Ofisi ya Mwanasheria MkuuTanga katika kuwezesha kusaidia watoto kupata haki,” anaeleza Sophia.

Akizungumzia namna anavyojisikia baada ya Tawla kumtetea na kuwa huru, Sophia anaanza kwa kububujikwa na machozi kwa furaha kutokana na kutokuamini kwamba angeweza kuwa huru kutokana na namna watu walivyokuwa wakificha ukweli wa jambo hilo.

Anasema kuwa katika tukio la kipigwa kwa kondakta huyo hadi kufikia hatua ya kupoteza maisha, baba yake mzazi ambaye kwa sasa yupo gerezani hakuhusika isipokuwa ni vijana waliokuwa wakiishi nao hapo kambini ndio walishiriki katika suala la kumpiga kijana yule.

“Kiukweli nakiri kwamba baba yangu hakuhusika kwa lolote na mauaji hayo lakini baada kutokea tukio hilo vijana wa mtaani ndio walishiriki,” anasema.

Akizungumzia changamoto ambazo wanakutana nazo walipokuwa kizuizini, Sophia anasema watoto wengi wanaathirika na ucheleweshwaji wa kesi na upelelezi, jambo ambalo linasababisha kuendelea kushikiliwa huku wakikosa haki zao za msingi ikiwemo elimu na masuala mengine muhimu.

“Lakini pia kitu kingine ambacho siwezi kukisahau ni kufungiwa mahabusu kwa siku saba nikiwa sionani na mtu yeyote, huku niliowakuta kuzuizini wakinidhihaki kwa kuniita muuaji, kitendo ambacho kiliniumiza sana,” anasema.

Anaongeza kuwa suala jingine ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa watoto wanaokuwa vizuizini ni kukosa haki ya msingi ya kupata elimu, jambo ambalo linakwamisha ndoto zao za kupata elimu bora.

“Nawashukuru Tawla kwa kuonyesha mapenzi makubwa kwa kunitetea na hatimaye nimetoka mungu atawalipa,” anasema.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Chama hicho, Adophina Mbekenga, anasema kesi hiyo ilikuwa maarufu, hivyo walianza kuifuatilia tangu Machi.

Baada ya hapo waliwasiliana na Ustawi wa Jamii kuwauliza baadhi ya maswali na kweli kama huyo mtoto yupo kwenye kituo chao na anakabiliwa na kesi namba gani ili waweze kuona namna ya kumsaidia.

“Nilirudi ofisini kumweleza bosi wangu hali halisi na kuona kesi hiyo ni nzuri kwao, kwani kipindi hicho walikuwa wakitekeleza mradi ambao unajishughulisha kusaidia watoto waliopo kwenye ukinzani wa kisheria kwa lengo ya kuangalia utekelezaji mzima wa sheria ya mtoto na mwenendo mzima wa kesi zinazowakabili watoto,” anasema.

Anasema walikuwa wanaangalia namna gani anaweza kuepukana na adhabu kama mtoto, kwa sababu kwa kawaida akitenda kosa bila kumfuatilia anaweza kukosa haki zake za msingi na ndio maana wakaona namna bora ya kuharakisha kesi hiyo kwa kuangalia sheria zinasemaje.

0714543839.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.