Magufuli asikilize kilio cha Katiba mpya

Rai - - MAONI/KATUNI - NA HILAL K SUED

K

ilinchomsukuma Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia kupeleka Bungeni notisi ya muswada wa kurekebisha kipengele cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kurefusha kipindi cha urais kukaa madarakani kutoka miaka mitano ya sasa hadi saba bado hakijajulikana.

Hata hivyo masuala kama hayo si mageni sana katika Bara hili la Afrika na hasa ukanda huu, na huenda hatua yake hiyo imekuja tu kiasili (naturally) au tuseme mvuto wa smaku (magnetic force) ukiangalia yanayotokea nchini Uganda, Rwanda, Burundi na DRC kwa staili tofauti, ingawa lengo ni lile lile – kurefusha vipindi vya watawala.

Tumeona wiki iliyopita picha za video zilizoonyesha Wabunge wa Bunge la Uganda wakitwangana makonde na hata kuumizana kutokana muswada uliyopelekwa Bungeni wa kuondoa kipengele cha ukomo wa umri kwa wagombea urais, ambacho sasa ni miaka 75.

Lengo hapa hata mtoto wa miaka 11 atajua – kumpa fursa rais Yoweri Museveni kugombea tena mwaka 2021 ambapo atakuwa na umri wa miaka 77. Ni ajabu sana kwa nchi za Afrika kung’ang’ania madarakani kwa mbinu na hatua mbali mbali zikiwemo zile moja kwa moja zinaashiria uchu wao wa madaraka. Hivi Katiba inachezewa kwa kukidhi haja ya mtu mmoja? Waambieni Wamarekani nao wafanye hivyo.

Sasa hivi Barani Afrika kuna viongozi wa umri mdogo ambao wanahangaika na katiba za nchi zao kujiongezea muda nadarakani. Hawa ni wan chi za Congo DRC, Rwanda na Burundi, na bila shaka wanasukumwa kufanya hivyo baada ya kutambua kuwapo viongozi wengine waliowahi kukaa madarakani kwa muda mrefu – kuanzia miaka 30 na kuendelea na hata baadhi yao kufia madarakani, na wengine bado wako madarakani.

Hawa ni pamoja na Robert Mugabe (Zimbabwe), Teodoro Obiang Nguema (Eq. Guinea), Paul Biya (Cameroon), Douardo Dos Santos (Angola), Lansana Conte (Guinea), Mobutu Sese Seko (Zaire – Congo), Hassan Al-Bashir (Sudan) na wengineo.

Hapa Tanzania hakuna kitu kama hicho, na hii imetokana na busara za viongozi wetu wa awamu mbali mbali, na bila shaka hili limechangia hali ya utulivu iliyodumu kwa miongo mingi. Hakuna haja ya kuuvuruga utulivu huu kwa kuanza kutikisa mashua (kama methali ya Kiingereza isemavyo – do not rock the boat).

Lakini kwa upande mwingine nasi hapa tuna rekodi yetu ambayo haiashirii mema na utulivu hapo baadaye. Katiba iliyopo ni ile ile iliyopo kwa zaidi ya miaka 40 sasa – rekodi kwa nchi za ukanda huu, kama siyo kwa Afrika nzima. Kibaya zaidi ilikuwa katiba ya mfumo wa demokrasia ya chama kimoja ambayo baadaye utawala wa chama hicho hicho uliiwekea viraka kukidhi mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Sasa ‘viraka’ hadi lini? Vinatosha, na kinachotakiwa ni kuifumua upya (overhaul) katiba iliyopo na kuja na nyingine inayoendana na mazingira ya sasa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, yaliyopo nchini na duniani kote.

Niliwahi kuandika katika safu hii miaka minne hivi iliyopita kwamba kama Rais wa Awamu ya Nne ya Jakaya Kikwete anataka abakie na kitu cha kukumbukwa (legacy) baada ya kuondoka madarakani, basi kitu hicho ni kuwapatia wananchi Katiba mpya.

Ilikuwa ni wakati mchakato wa katiba mpya aliouanzisha mwishoni mwa 2011 umeanza baada ya kuanzishwa sheria ya mchakato huo na uundwaji wa tume ya kuratibu maoni ya wananchi.

Lakini baada ya Tume hiyo kuja na mapendekezo yake waliyoyapata kutoka kwa wananchi, kwa mshangao wa wengi Kikwete aliyapinga, hatua ambayo ilionekana wazi kuyumbisha mchakato mzima uliotumia mabilioni ya hela za wananchi.

Isitoshe mchakato mzima haukuendeshwa kwa makubaliano (consensus) ya wajumbe wa

Bunge la Katiba kwani ilionekana waligawanyika kiitikadi ya vyama na hivyo kuonekana kuwapo kwa uburuzaji wa waziwazi. Ilikuwa dhahiri kwamba kwa upande wa chama tawala (CCM) jicho lake moja lilikuwa ni kuendela kwake kukaa madarakani.

Suala la muungano nalo ndiyo lilikuwa chanzo kikubwa cha migongano na kikubwa hapa ni kwamba wenzetu wa Visiwani walitaka muungano wenye uhuru zaidi (more autonomy) kuliko ilivyo – hususan kuhusu mfumo wa serikali tatu.

Sasa hivi sauti za wito wa kuurejesha ule mchakato wa katiba mpya au hata kuanzisha mwingine zimeanza kupazwa, na zote zinaelekezwa kwa Rais John Magufuli. Kwa kifupi anaambiwa atafute ujasiri kama wa Kikwete kuanzisha mchakato huo na ambao akifanikiwa ndiyo kitakuwa kitu kikubwa cha kukumbukwa katika historia baada ya kuondoka madarakani.

Makala mbali mbali katika magazeti siku za karibuni, pamoja na kumuunga mkono katika kampeni yake ya kupambana na rushwa na kutetea rasilimali za nchi, zimemtaka alete katiba mpya ambayo mambo yote anayolalamikia kwenda ndivyo sivyo aliyoyakuta ndani utawala yaainishwe moja kwa moja katika katiba mpya.

Baada tu ya kuteuliwa kuwa waziri wa Sheria na Katiba Aprili mwaka huu, Profesa Palamagamba Kabudi alijikuta akibanwa na wabunge kuhusu mchakato wa Katiba Mpya. Kabudi alikuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Akiwa mbele ya Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge, Wabunge wa chama tawala – CCM walimtaka aisukume serikali ianzishe mchakato wa Katiba mpya kwa sababu ilikuwa ni sehemu ya ilani ya uchaguzi ya chama chao, na walimuuliza awaambie Watanzania lini watarajie Katiba hiyo. Aidha walishangaa kuona suala hilo kutotengewa bajeti ya mwaka huu wa fedha 2017/18.

Msukumo mkubwa zaidi wa kupata Katiba mpya ulikuja mwishoni mwa mwezi uliopita ambapo wawakilishi kutoka asasi zaidi ya 80 za kiraia (CSOs) waliongeza sauti zao –zilimtaka Rais John Magufuli aanzishe mchakato uliosita mwaka 2014.

Wawakilishi hao waliiomba serikali ifikirie gharama kifedha, rasilimali-watu na muda uliotumika katika mchakato ule, na kuongeza kwamba haiingii akilini kwa nini suala hili lisipewe kipaumbele na utawala huu wa sasa.

Waziri wa Sheria na Katiba Prof Palamagamba Kabudi.

Rais Dk. John Magufuli

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.