Watanzania watarajie nini?

Rai - - MAKALA - NA SUSAN UHINGA, TANGA

MFULULIZO wa makala zangu hizi unaangazia zaidi fursa nyingi zinazo na zitakazopatikana kutoka kwenye mradi mkubwa wa bomba la mafuta ghafi linaloanzia Hoima nchini Uganda hadi Tanga, Tanzania.

Hii ni fursa kubwa kama nilivyopata kueleza katika makala kadhaa zilizopita, ni ukweli usiopingika mradi huu utahuisha uchumi wa mkoa wa Tanga uliokuwa umedumaa.

Mbali na mradi kuifaidisha Tanga, lakini pia ni mradi wenye tija kwa nchi nzima maana Serikali itakusanya kodi ya kutosha itakayoweza kusaidia kuendeleza na kuboresha huduma za jamii.

Tayari Rais Dk. John Magufuli ameshaiona tija kubwa kupitia kwenye mradi huo, ambao ni yeye mwenyewe ameshiriki kikumilifu kuchagiza ujio wake pamoja na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba hilo.

Kama hiyo haitoshi kitendo cha wananchi wengi wawe ni wa Tanga au wa kutoka maeneo mbalimbali nchini wakipata ajira, maana yake tatizo la ajira litapungua kwa kiasi Fulani.

Pamoja na ukweli huo, lakini ipo dhana kuwa huenda mradi huo ukawa na manufaa kwa watu wachache waliopachikwa jina la vigogo.

Hii ni dhana potofu ambayo tunapaswa kuipinga na kuitokomeza kabisa kwani inaweza kuzalisha virusi vya uvivu, chuki na uhasama ambao hautasaidia mtu mmoja mmoja wala Taifa kwa ujumla.

Jambo pekee ambalo linapaswa kutawala vichwani mwetu ni kuona tija inapatikana kwa kila raia wa Tanzania bila kujali mpata tija atapata ajira ya moja kwa moja au ataipata tija kwa kufanya biashara zitakazowagusa moja kwa moja watumishi wa mradi huo.

Tujiulize ni kipi ambacho Watanzania wanapaswa kukitarajia kwenye mradi huu, hapa ndipo panapaswa kubeba msingi wa hoja hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk. James Mataragio lipata kusema kwa uwazi kuwa yapo matarajio mengi na kwamba ujenzi wa bomba hilo utaharakisha utafutaji wa mafuta nchini, hasa maeneo ya Kaskazini ambako korido ya Kaskazini, ambako hakujafanyika utafiti wa kutosha ni wazi sasa utafanyika kwa sababu sasa miundombinu hakuna ila ujio wa bomba hilo utarahisha kazi.

Anasema uwepo wa bomba utachochea uwekezaji kwani kampuni nyingi zitakuja kufanya utafiti na iwapo yatapatikana itakuwa rahisi kuingiza kwenye bomba lililopo na kuendelea na bisahara.

“Ni sawa na una barabara ukilima utasafirisha mazao kwa kuwa una barabara. Uzuri uliopo tayari kuna kiwango cha mafuta kimeshaonekana, lakini tutashindwa kusafirisha kwa kuwa hatuna miundombinu.

“Kampuni zilisita kwa kuwa eneo la Ziwa Tanganyika liko porini. Ukichimba gharama, zitakuwa kubwa na mafuta ni kidogo,” anasema Dk. Mtaragio.

Anasema uwepo wa bomba, utaongeza idadi ya wawekezaji wanaokuja nchini, utaimarisha matumizi ya bandari ya Tanga na kuongeza mapato ya serikali.

“Bandari itaboreshwa na itawezesha meli nyingi kuweka nanga. Ujenzi wa barabara takribani kilomita 200 na nyingine zitaboreshwa kwa kiwango cha changarawe kilomita 150.

Pia reli itaboreshwa na kutoa fursa kwa Kampuni ya Reli Tanzania (TRC), kutumika kusafirisha vifaa mbalimbali wakati wa ujenzi.

Anasema matarajio ni mabomba 123 yatakayosafirishwa na ni fursa mpya kwa TRC. Mkurugenzi huyo anasema miundombinu itakuwa inamilikiwa na TPDC na moja ya majukumu yake ni kushiriki katika uwekezaji wote wa miundombinu katika mkono wa chini, hivyo wao ni wasimamizi wakubwa.

Dk. Mataragio, anasema eneo husika ambako bomba la mafuta litafikishwa ni tambarare, hivyo kuendana na mahitaji ya uwekaji bomba la mafuta.

Anasema athari za mlima ni kwamba, unaleta changamoto ya gharama za ziada katika ujenzi.

“Tanga iko tambarare kwa kiasi kikubwa, kuna milima midogo midogo. Pia, bandari yake ina mazingira mazuri, kwani ili kuweza kuwa na uzalishaji kwa mwaka mzima, ni lazima meli ije kuchukua mafuta kwa mwaka mzima,” anasema.Anafafanua wasifu wa Bandari ya Tanga, kwamba ina kingo za asili ambazo ni adimu sana kwa bandari nyingi duniani.

Mkurgenzi huyo TPDC anafafanua umuhimu wa kingo hizo kuwa ni katika baadhi ya vipindi baharini kunakuwepo upepo mkali na meli zitashindwa kupakia bandarini.

Anasema manufaa ya bandari hiyo ni kwamba, kuna kisiwa cha Pemba kwa upande wa Mashariki, ambacho kinazuia mawimbi kutoka bahari kuu, hivyo inaipa uwezo bandari ya Tanga kupakia mafuta mwaka mzima.

Mkurugenzi huyo anasema, bomba hilo la mafuta kutoka Hoima hadi Tanga litakuwa na urefu wa kilomita 1,444 na katika umbali huo, kilomita 1,144 ambazo ni asilimia 79 zitakuwa upande wa Tanzania na kilomita 300 zitakuwa upande wa Kenya.

0767 414 185

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.