Umeme wa uhakika changamoto kwa uchumi wa viwanda

Rai - - MAKALA - NA MOSES NTANDU Makala hii imendaliwa na Mwandishi na Mtafiti katika Kituo cha kutoa Taarifa kwa umma Tanzania (TCIB) anapatikana kwa namba 0714 840656 na Baruapepe mosesjohn08@yahoo.com

Oktoba 24 mwaka jana Tanzania na Morocco zilitiliana saini makubaliano ya ushirikiano 21 katika sekta kadhaa ambazo thamani yake ilikuwani takribani shilingi trilioni 4.

Katika makubaliano hayo yalishuhudiwa na wakuu wa mataifa hayo Tanzania ikiwakilishwa na Rais John Magufuli na Moroco ikiwakilishwa na mfalme wa taifa hilo Mohammed VI.

Nishati mbadala ilikuwa ni miongoni mwa sekta muhimu kati ya mikataba ile 21 ambayo ilisainiwa siku hiyo ili kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya mataifa haya mawili Tanzania na Morocco.

Kwa kuzingatia mafanikio ambayo Morocco imeyapata katika sekta hii, Tanzania imefanikwa kuingia katika makubaliano ya ushirikiano kwa sekta hiyo kwani kuna mengi sana Tanzania inapaswa kujifunza kutoka Morocco ili kuhakikisha kuwa Tanzania inaboresha huduma ya nishati ya umeme na miundombinu yake.

Changamoto kubwa barani Afrika ni uhaba wa nishati ya umeme ambapo inaelezwa kuwa hadi kufikia mwaka 2020 bado bara la Afrika litakuwa na upungufu wa nishati ya umeme kwa asilimia 60.

Na hii inaelezwa kuwa watu tisa kati ya 10 ya watu barani Afrika wanaishi bila kuwa na nishati ya umeme. Hii maana yake ni kwamba pia kuna changamoto kubwa katika uzalishaji mali pia kwani uwepo wa viwanda unategemea uwepo wa nishati hii muhimu.

Kwa sasa Tanzania inanadi sera yake ya uchumi wa viwanda kwa nguvu zote huku kukiwa na changamoto hii kubwa ya upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika. Kinachopaswa kufanyika kwa sasa ni kuitumia fursa hii kwa nguvu zote kwani taifa la Morocco kwa sasa limepiga hatua katika sekta hii.

Ninachoweza kuthubutu kusema kwa sasa ni kwamba kama taifa tutafanikiwa vyema katika suala la uchumi wa viwanda ikiwa tutaitumia ipasavyo fursa hii ya ushirikiano kwa nishati mbadala na taifa la Morocco.

Habari njema kwa sasa ni kwamba Serikali ya Morocco imeialika serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Madini kuhudhuria mkutano wa tatu uitwao Photovoltaica ambao ni Mkutano wa kimataifa wa maonesho ya nishati ya jua ambao utafanyika nchini Morocco mapema mwezo Februari mwakani.

Lengo kuu la mkutano huo ni kuonesha mipango na mikakati ya taifa hilo kuboresha na kuendeleza nishati mbadala. Pia mkutano huo utakutanisha watafiti mbalimbali, wajasiriamali na mamlaka mbalimbali za kimataifa kushiriki na kujadili masuala mazima ya nishati mbadala.

Serikali ya Morocco inamiradi mingi inayozalisha nishati ya umeme kwa nguvu ya jua ambayo pia huzalisha umeme mwingi sana na kuuingiza katika gridi ya taifa, miradi hiyo ambayo ni pamoja na mradi wa NOOR Ouarzazate wenye uwezo wa 510 MW CSP na 70 PV, mradi mwingine ni NOOR Tafilalt na Atlas ambao unauwezo wa 300 MW PV, mradi wa NOOR Midelt 300 MW CSP na 300 MW PV, pia NOOR Laayoune na Boujdour 100 MW PV, miradi mingine ni NOOR Tata 300 MW na 300 MW ya CSP PV na miradi mingine ya nishati ya jua ya ukanda wa kiuchumi wa 150 MW PV. Yote hii ni miradi mikubwa ya uzalishaji wa nishati kwa kutumia nguvu ya jua.

Haya yote ni kuhakikisha kuwa wanahamasisha upatikanaji wa nishati mbadala kwa matumizi ya umma na matumizi ya uzalishaji viwandani ili kuhahakisha kuwa gharama za maisha kwa wananchi zinashuka na kuepuka uharibifu wa mazingira. Pia kupunguza matumizi ya nishati ya umeme unaozalishwa kwa nguvu mafuta.

Hata hivyo, mafanikio ya kuboresha uzalishaji wa nishati ya umeme na uboreshaji njia ya usafirishaji wa umeme nchini humo, mkakati wake ulianza kuratibiwa toka mwaka 2009 na kuleta mafaniko kufikia mwaka 2015.

Matumizi ya awali ya nishati ya umeme nchini Morocco imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia tano kwa miaka ya hivi karibuni ambapo kumekuwa pia na ongezeko la matumizi ya nishati hiyo kwa asilimia 6.5 kwa mwaka. Ongezeko hili limetokana na serikali kuweza kusambaza umeme katika sehemu kubwa ya taifa hilo ambapo vijiji vingi tayari vina umeme na kufanya watumiaji wa nishati hiyo kuongezeka pia huduma nyingine za miundombinu, viwanda, kilimo, utalii na makazi bora kuongezeka.

Ili kuweza kufikia maboresho hayo na kwenda mbele zaidi inaelezwa kuwa serikali ilikuja na mkakati huo kabambe mwaka 2009 katika maboresho yaliyoratibiwa na kwa karibu na uongozi wa mfalme wa taifa hilo Mohammed VI. Pia lengo la mradi huo lililenga kuhakikisha usalama wa usafirishaji wa umeme, kuongeza upatikanaji wa umeme nchini humo na kuwafikia wananchi wengi zaidi na kwa vyanzo sahihi, pia lengo jingine mahsusi lilikuwa ni kuhakikisha kuwa sekta ya nishati mbadala inaboreshwa ili kuweza kulinda mazingira.

Mkakati huo ni bora sana hata kwa nchi yetu kwani kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya nishati mbadala kutachangia katika utunzaji wa mazingira huku nchi ikiweza kukabiliana na tatizo la upungufu wa umeme ambao umekuwa ni changamoto kubwa sana kwa taifa letu kwa miaka mingi sana.

Miradi ambayo imetekelezwa na serikali ya Morocco imeweza kufanikiwa kupata nishati ya umeme wa ziada wa takribani 2760MW kwa kipindi cha kati ya mwaka 2009 na 2015.

Kupatikana huku kwa nishati mbadala ya takribani 2760MW kwa kipindi kifupi cha miaka sita si jambo la kubeza kwani ni mafanikio makubwa tena kwa muda mfupi, pia ni jambo la kujifunza na taifa letu kuanza miradi kama hii kwa kupitia makubaliano ambayo Tanzania ilitiliana saini na serikali ya Morocco. Kuanza kwa miradi hiyo hapa nchini kutakuwa na mafanikio kwani vyanzo vya uzalishaji wa nishati hizo hapa nchini ni vingi sana kama vilivyotumika huko Morocco ambavyo ni, jua na upepo.

Pia njia za usafirishaji wa umeme nchini Morocco inaelezwa kuwa ni njia imara na ya kisasa zaidi ambapo kuna takribani 3753 km zinazo beba umeme mkubwa ambazo zilijengwa na kuimarishwa mwaka 2009 na 2014 na kufanya taifa la Morocco kuwa na mtandao wa usafirishaji wa umeme mkubwa kuwa ni 23,331 km hadi kufikia mwaka 2014.

Kwa upande wa umeme wa nishati ya upepo serikali ya Morocco imewekeza katika mradi wa 2000MW, mradi huu ni mkubwa uliopangwa kutekelezwa kwa maagizo ya mfalme na unategemewa kukamilika kabla ya mwaka 2020 na unatarajiwa kuzalisha nishati ya 6600 GWh kwa mwaka na mradi huo utachangia asilimia asilimia 26% ya umeme wote unaozalishwa nchini Morocco.

Mradi huu utaiwezesha serikali ya Morocco kuokoa dola za Kimarekani milioni 750 kwa mwaka na pia mradi huu utaiwezesha nchi hiyo kuweza kuepuka uharibifu wa mazingira kwani utapunguza uzalishaji wa kaboni kwa tani milioni 5.6 kwa mwaka. Nchini humo kuna miradi mingine ya uzalishaji wa umeme wa upepo ambayo inazalisha takribani 850 MW ambayo ni pamoja na mradi wa Tanger II 100 MW, Jebel Lahdid 200 MW, Midelt 150 MW, Tiskrad 300 MW na mradi wa Boujdour 100 MW.

Hata hivyo, mafanikio ya kuboresha uzalishaji wa nishati ya umeme na uboreshaji njia ya usafirishaji wa umeme nchini humo, mkakati wake ulianza kuratibiwa toka mwaka 2009 na kuleta mafaniko kufikia mwaka 2015.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.