Stars itapatikana kwa vigezo si makubaliano

Rai - - MAKALA JAMIOIKTOBA - „ ABDUL MKEYENGE

ILIWAHI kutokea kwa wakati mmoja Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuwa nahodha wa Yanga na timu ya taifa, pia Agrey Morris, nahodha wa Azam huku Said Cholo, kuwa nahodha wa Simba.

Hii iliwahi kutokea miaka kadhaa iliyopita na hata sasa bado wapo wengi wakinguuruma ndani ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Yote hayo watu waliona jambo la kawaida kwa wachezaji hao wanaotokea visiwani Zanzibar kuwa viongozi kwa wachezaji wenzao katika Ligi ya Tanzania Bara, wengine wakitoka mataifa mbaliambali kwenye ngazi za klabu.

Si hilo tu bali iliwahi kutokea pia wachezaji wengi zaidi kutoka Visiwani wakiunda kikosi cha Timu ya Soka ya taifa ‘Taifa Stars’ huku kwa vipindi kadhaa wachezaji wa nafasi ya kipa walitokea huko na kufanikiwa kushikilia namba.

Wachezaji kama Riffat Said, Juma Bakari Kidishi, Rashid Korosheni, Athanas Michael, Seif Baus, Rashid Lato, Mohammed Said Babeshi, Innocent Haule, Ibrahim Kapenta, Ridhaa Khamis, Mohammed Abdulkadir Tash, Ally Bushiri ni miongoni mwa waliotokea Zanzibar na kufanikiwa kutamba ndani ya kikosi hicho wka nyakati tofauti.

Lakini katikati mwa wiki iliyopita viongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) wamewaangusha Watanzania wenzao kwa kutoa kauli inayoweza kuivuruga sekta ya mchezo wa soka nchini.

Wametuangusha kwa kujitokeza hadharani na kudai wanataka usawa katika uteuzi wa wachezaji wa timu hizo kuanzia za vijana hadi za wakubwa. Usawa huo ni wachezaji wanaocheza Ligi ya Zanzibar kuitwa Taifa Stars.

Viongozi hao wamelalamika na wamekwenda mbali wakidai wanahitaji usawa kwa wachezaji wa visiwani na wale wa Bara ndani ya vikosi vya timu za taifa. Wapi tunapotaka kwenda Watanzania?

Uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliomaliza muda wake uliweka kipaumbele cha kuhakikisha ZFA inapata uanachama ndani ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kabla ya kunyang’anywa muda mfupi tu baada ya kuupata.

Maneno ya namna hii ndiyo yanayowaaminisha baadhi ya wadau kuamini TFF inaitenga ZFA kitu ambacho si kweli. ZFA iombe radhi!

Ukweli ni kwamba uteuzi wa wachezaji wa timu za taifa unatokana na viwango vya wachezaji wanavyovionesha katika Ligi na kamwe si kuangaliana usoni au kuwa agenda ya kimkataba kati ya pande hizo. Hapa ZFA ilipaswa kujitathimini kwanza ubora wa ligi yao.

Suala la uteuzi wa wachezaji wa timu ya taifa ni suala la kiutaalamu zaidi hivyo haina budi wanaochaguliwa kukidhi viwango fulani vinavyotakiwa na kocha husika, sui suala la kuridhishana na kufurahishana tu.

Baada ya CAF kutengua uanachama wa ZFA, ni kweli ZFA wanapaswa kurudi kwa TFF na kuweka mikakati ya pamoja ya kuinua soka lao na si kuanza kutafuta chokochoko za kutofautiana.

Kama tunajenga nyumba moja, kwanini tuanze kugombania fito? Katika kikosi cha sasa cha timu ya taifa kinachojiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi, kuna mchezaji Adeyum Saleh anayetokea visiwani lakini akishiriki Ligi Kuu Bara.

Timu ya taifa ni timu ya kila Mtanzania, si timu ya TFF wala ZFA. Mchezaji ambaye yuko vizuri kwa muda ambao timu ya taifa inaitwa basi hujumuishwa kw avigezo mvya viuwango vyao na ndiyo maana wachezaji kama Nadir Haroub ‘Canavaro’ Aggrey Moris, Rifat, Bushiri, Abdi Khassim Babi walitamba ndani ya kikosi hicho kwa nyakati tofauti, ZFA walitaka TFF ifanye nini?

Katika kikosi cha Timu ya soka ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kilichokwenda nchini Gabon kushiriki fainali za vijana mapema mwaka huu, kulikuwa na kijana Asaad Juma ‘Deco’ anayetokea visiwani humo.

Kuna wakati timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) ilikuwa ikinolewa na Kocha, Nasra Juma ambaye anatokea visiwani humo na Timu ya soka ya Taifa soka la ufukweni (Beach Soccer) inaundwa na wacheaji wengi wanaotokea visiwani.

Kuna wakati kikosi cha Taifa Stars kilitawaliwa na robo tatu ya wachezaji wa visiwani humo na hakuna mtu aliyewahi kujitokeza hadharani Tanzania Bara kupinga idadi hiyo bali wote waliamini hao ndiyo bora na wangeweza kulivusha jahazi mahali salama. Na ndivyo ilivyokuwa.

Kama umezuka mjadala wa kulalamika kuhusu usawa wa wachezaji wa timu ya taifa, ni wazi kuna safari ndefu sana ya kuweza kuifikia nchi ya ahadi ambayo watanzania wanaiota kila siku.

Stars iliwahi kuwa na wachezaji wengi wanaotokea Mwanza. Mrisho Ngassa, Jerry Tegete, Mwinyi Kazimoto, Kelvin Yondani, Henry Joseph, Kiggi Makasi, lakini hakukuwa na mkoa uliojitokeza kulalamika juu ya kwanini Mwanza imekuwa na wachezaji wengi kikosini Stars.

Muda huu ambao Watanzania tuko kwenye maandalizi ya mwishoni kuelekea michuano ya Afcon kwa vijana ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji mwaka 2019, inatakiwa wote kama taifa kuwa wamoja, si kulalamika wala kuhisi kubaguana.

Tulitaraji kusikia viongozi hao wakijipigia upatu juu ya Uwanja wa Aman na Gombani kuorodheshwa kwenye viwanja vitakavyotumika kwa michuano hiyo ili kutanua wigo wa ajira, biashara na utamaduni ulioko visiwani humo.

Lakini kujitokeza kwa baadhi ya viongozi hao na kudai wanatengwa ni kama wanaitenga TFF na Watanzania ambao hawana tabia ya kutengana.

Sababu ya timu ya taifa Hispania kutoimba wimbo wa timu ya taifa katika michezo na badala yake kupiga ala za vyombo ilianza kwenye matatizo ya namna hii kwa majiji ya Madrid na Catalunya, kuchuana.

Majiji hayo yanajiona bora zaidi ya jingine na hali hiyo imefanya Jiji la Catalunya kutaka kujitenga na liishi kwa kujitegemea. Kwanini basi Tanzania ifike huko, wakati inawezekana kukaa pamoja na kurekebisha mambo yanapotokea kwenda mrama?

Hispania ilivyoshinda Kombe la Dunia mwaka 2010, nchini Afrika Kusini, kuna baadhi ya raia wa Hispania hawakupenda nchi yao ishinde taji hilo na sababu kuu ni uwepo wa kikosi cha Hispania kuwa na wachezaji wengi wa klabu ya Barcelona ambayo ni hasimu na klabu ya Real Madrid.

Umoja wa Watanzania wa visiwani na wa Bara, haujaanza leo wala jana ulianza tangu zamani, inakuwaje hivi sasa tunaanzisha chokochoko zenye dhana ya kiubaguzi? Kauli hiyo ni wazi haijengi zaidi inaweza kuubomoa umoja uliokuwepo miaka na miaka.

Naamini viongozi wa ZFA na watu wa visiwani humo kiujumla ni waadilifu katika masuala ya kimichezo. Kwenye hili walilopotokwa, hakuna budi kauli zao kupuuzwa na kama Watanzania kutazama mbele na kuweka mikakati thabiti ya kupandisha soka.

Kikosi cha Taifa Stars

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.