Mtatiro: Lissu amenipa ujasiri

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi –CUF, Julius Mtatiro (pichani) ameweka wazi kuwa kitendo chake cha kukutana na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kimempa ujasiri zaidi.

Katika Mazungumzo yake na RAI juzi, Mtatiro alisema kwa sasa haoni sababu ya kukaa kimya na kwamba yuko tayari kusema bila woga.

“Nimegundua, tukiendelea kuwa waoga bila kuyasema yale ambayo wao hawapendi kuyasikia, hakutakuwa na wa kutusemea, tuseme bila woga na mimi sitaacha kusema,”alisema Mtatiro.

Aidha, katika ukurasa wake wa facebook, Oktoba 8, mwaka huu Mtatiro aliandika ujumbe uliosomeka: SALAMU KUTOKA NAIROBI. Mtatiro. J

“Hapa jijini Nairobi leo nimepata fursa ya kumtembelea na kuzungumza kwa kirefu na ndugu yetu Tundu Lissu. Kama kuna mtanzania imara, asiyeogopa na mwenye maono makubwa ni Lissu. Lissu hana wasiwasi and he will strike hard very soon!

“Risasi zote zilizopenya kwenye mwili wa Lissu zimemtengenezea uimara maradufu, mara 70, mara 100. Waliodhani kuwa kumuua Lissu ndiyo kuua harakati za Watanzania kudai taifa la haki na linalofuata misingi ya sheria na katiba bora, wanajidanganya.

Lissu ameniambia “Mtatiro nenda kawaambie kuwa nitarudi nikiwa mzima na tutaendelea na mapambano maradufu zaidi, faraja muhimu nayohitaji kutoka kwa Watanzania hivi sasa ni kuendeleza mapambano ya kudai haki na kupambana na udikteta, tusikubali nchi yetu iharibiwe na kikundi cha watu wanaoogopa kukosolewa”

“Nimemwambia Lissu fikra zangu, kuwa ..siku nilipotaarifiwa kuwa umepigwa risasi nyingi ikiwa ni njia ya kukuua, nilitabasamu, nilijua mapambano ya kudai haki yamekolea, nilijua umekuwa imara mno maishani mwako na kwamba mateso utakayopitia yatakujenga na yatatujenga sisi zaidi!”

“Mimi binafsi kama Mtatiro, kumuona Lissu kumenijenga zaidi, kumenifundisha kuwa ukipigwa risasi hata 100 kwa sababu u mkosoaji wa watawala yapo mambo mawili yatatokea, aidha utapona kama Lissu au utakufa kama ilivyowatokea wapigania haki wengi.

“Uki-survive kama Lissu jambo moja litatokea, utaungana na wananchi wote kupigania haki kwa nguvu kubwa zaidi. Ukiuawa kwa risasi kama wapigania haki wengi jambo moja kubwa litatokea, kifo chako kitapandikiza mbegu kubwa ya ukombozi, kifo chako kitaliamsha taifa kupigania haki na kupambana na madikteta wajinga.

“Kama wapuuzi waliomshambulia Lissu walidhani kuwa wanatutisha, kutuogofya na kuturudisha nyuma, wanajidanganya. Wanatuandaa kimwili na kiroho kulipigania taifa na kupambana kudai utawala wa haki, utawala wa sheria na katiba bora. Wanatuandaa kujitolea maisha yetu kwa ajili ya Taifa.

“Nataka kuwaambia watanzania kuwa nchi yetu siyo Rwanda, siyo Burundi, siyo Congo wala siyo Uganda. Zipo njia zilitumika kuwazoesha Wanyarwanda, Warundi, Waganda na Wakongo udikteta. Kama yupo mtu anadhani anaweza kuipeleka Tanzania udiktetani anajidanganya. Tutalipigania taifa letu, utu wetu na uhuru wetu wa kuzaliwa bila kuogopa mikanda ya risasi” alisema.

Oktoba 9, mwaka huu aliandika tena: Kama wapuuzi waliomshambulia Lissu walidhani kuwa wanatutisha, kutuogofya na kuturudisha nyuma, wanajidanganya. Wanatuandaa kimwili na kiroho kulipigania taifa na kupambana kudai utawala wa haki, utawala wa sheria na katiba bora. Wanatuandaa kujitolea maisha yetu kwa ajili ya Taifa. Tutalipigania taifa letu, utu wetu na uhuru wetu wa kuzaliwa bila kuogopa mikanda ya risasi.”

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.