Kutenganisha wizara kulete tija kwa taifa

Rai - - MAONI/KATUNI -

MWISHONI mwa wiki iliyopita Rais John Magufuli alifanya mabadiliko makubwa kwenye baraza lake la mawaziri kwa kuhamisha baadhi ya mawaziri, manaibu waziri kupanda na kuwa mawaziri kamili, kuwaacha mawaziri wanne pamoja na kuongeza wizara mbili.

Tunampongeza Rais kwa hatua hiyo kwani pamoja na mengine, bila shaka aliona utendaji wa baadhi yao ulikuwa hauridhishi kwa kasi yake ya uongozi.

Jambo kubwa zaidi tuliloliona katika mabadiliko hayo ni kuongezeka kwa idadi ya wizara kutokana na kutenganisha wizara mbili za zamani – Wizara ya Nishati na Madini ambayo sasa zitakuwa mbili – Wizara ya Madini, na Wizara ya Nishati.

Wizara nyingine iliyotenganishwa na kuwa mbili ni ile Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo kwa sasa kutakuwa na Wizara ya Kilimo inayojitegemea na nyingine itakuwa ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Tunaamini amelifanya hili kwa sababu kadha wa kadha kubwa ikiwa ni kuhakikisha wizara hizo zinapunguziwa mzigo ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa kiwango anachokitaka.

Wote tunajua ugumu wa wizara ya Nishati na Madini, kabla ya kutenganishwa wizara hiyo ilikuwa ni kaa la moto kwa Mawaziri waliopewa dhama ya kuingoza.

Mbali na hilo lakini pia hatuioni haja ya kusema kuwa wizara hiyo ni miongoni mwa wizara za zamani hapa nchini, kwani ilianzishwa mwaka 1961 mara tu baada ya kupata uhuru.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba tangu zama za ukoloni nchi hii ilikuwa ikifanya shughuli za uchimbaji madini pamoja na za nishati – kama vile usambazaji wa umeme na uagizaji wa mafuta ya magari na mitambo.

Hata hivyo katika miaka ya karibuni wizara hiyo imetokea kuwa miongoni mwa wizara zenye misukosuko mikubwa kiasi kwamba mawaziri wanaoteuliwa kuiongoza huwa hawakai muda mrefu.

Waziri wa mwisho kuongoza Wizara kabla ya kutenganishwa mapema wiki hii ni Profesa Sospeter Muhongo ambaye alikuwa ni wa 30 akitanguliwa na Amir H Jamal (1961-64). Katika kipindi cha miaka 25 iliyopita tayari mawaziri 11 wameiongoza.

Sababu kubwa ya wizara hiyo kuongozwa na Watanzania wengi ni ukubwa wa wizara yenyewe na umuhimu kwa taifa – hususan kutokana na maliasili ya madini ambayo hutoa mchango mkubwa kwa pato la taifa na nishati ambayo ni muhimu pia katika maendeleo ya nchi.

Katika miaka ya karibuni, Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikikumbwa na kashfa nyingi zikiwemo za ufisadi kutokana na mikataba ya uchimbaji wa madini, mikataba ambayo ilikuwa hailipi taifa mapato halisi kutokana na rasilimali ya madini inayopatikana kwa wingi nchini.

Kwa upande wa nishati kadhalika suala la kuruhusu makampuni binafsi ya kufua umeme kuzalisha umeme na kuiuzia Tanesco, shirika la umma la ugavi wa umeme kupitia mikataba iliyokuwa inaikaba koo shirika hilo katika uendeshaji wake.

Ni matumaini yetu kwamba baada ya kutenganishwa wizara hizo mbili zitaendeshwa kwa ufanisi na kuwepo kwa tija zaidi kwa wananchi kuliko ilivyokuwa hapo awali.

Tunawaomba mawaziri waliopewa dhamana hiyo waende na kasi ya Rais Magufuli, ambaye tangu aingine madarakani ameonesha dhahiri kupambana na watu wote wanaotafuna mali za Taifa hili.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.