Mwalimu Nyerere aliona mengi katika nchi

Rai - - MAONI/KATUNI - GABRIEL MUSHI 0715126577

KILA kona ya nchi sasa imekuwa kilio cha ‘maisha magumu’. Tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani Novemba 5, mwaka 2015, wimbo wa maisha magumu umezidi kushika kasi na kuleta ubishani usio kifani miongoni mwa Watanzania ikiwamo wachumi na wachambuzi wa masuala ya kijamii.

Hali hiyo imesababisha asilimia kubwa ya wananchi wasahau kufikiria huduma muhimu kama vile maji, elimu, afya na kufikiria namna ya kujinasua katika hali ngumu ya maisha.

Ukweli huo unadhihirishwa na utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza Juni mwaka huu, ambapo ulibainisha kuwa asilimia 18 ya wananchi wana hamu ya kumuuliza Rais John Magufuli kuhusu ugumu wa maisha, huku masuala ya elimu yakishika asilimia tisa, afya (asilimia nane), miundombinu (asilimia sita) na maji (asilimia tano).

Licha ya kwamba utafiti huo ulionesha wananchi wanaukubali utendaji wa Rais Magufuli kwa asilimia 96, suala la ugumu wa maisha bado limeendelea kuwa kilio cha wengi hasa kutokana na jukumu la kuinyoosha nchi.

Itakumbuka kwamba Rais Magufulialipoingiamadarakani aliahidi kushughulikia na maadui wakubwa wa Taifa hili, ambao ni wala rushwa, mafisadi, wabadhirifu wa mali za umma na wapiga dili. Hata hivyo, wapo watumishi wengi waliotumbuliwa kutokana na tuhuma mbalimbali kubwa ikiwa ni rushwa.

Licha ya juhudi hizo ambazo zimeonekana kukonga nyoyo za Watanzania wengi, uchungu ulianza kuonekana baada ya kuweka wazi kuwa Serikali yake imedhamiria kubana matumizi.

Kwamba zile safari za nje na ndani, posho za vikao na mikutano ya Serikali hotelini, wakwepa kodi, mikutano ya Serikali hotelini sasa basi! Lakini pia rais alienda mbali zaidi na kuagiza fedha zote za mashirika na taasisi za umma zihifadhiwe Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Na kweli hayo yote yametekelezwa ambapo sasa asilimia kubwa ya watumishi katika sekta zote za umma wanadaiwa ‘kulia njaa’.

Wakati kilio kikizidi kuongezeka, mara kadhaa rais amejitokeza na kusema wanaolia ni wale waliozoea kupiga ‘dili’ kwamba wale waliozoea kupata fedha isivyo halali na kuongeza kuwa asiyefanya kazi na asile. Hali hii imekuwa ikitafsiriwa na kada mbalimbali katika maana nyingi.

Baadhi ya wachambuzi ya masuala ya kiuchumi na kijamii wanaona kuwa ‘maisha magumu’, umekuwa ni sawa msemo ambao huikumba Serikali yoyote inayoingia madarakani, mathalani Serikali ya Awamu ya Tatu ililalamikiwa pia kwamba imebana matumizi, hivyo maisha yakawa magumu, vivyo hivyo kwa Serikali ya Awamu ya Nne hakuna aliyesema maisha kwake ni mteremko kwa mantiki hiyo wachambuzi hao wanaona hata sasa ni jambo la kawaida tu kusema maisha magumu kwa sababu hayajawahi kuwa rahisi.

Hata hivyo, Gavana wa Benki Kuu (BOT), Profesa Benno Ndulu, alikaririwa na vyombo vya habari kuwa fedha zipo na kwamba wanaolalamika kuwa zimepotea ni mafisadi ambao walikuwa wakizipata kwa njia zisizo halali, huku Rais Magufuli akisema kupotea huko kwa fedha kunatokana na watu kuzificha na akatishia kubadilisha noti.

Aidha, Ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) hivi karibuni, ilibainisha kuwa mwaka mmoja uliopita mtawanyiko wa fedha umepungua kutoka asilimia 16.2 Januari mwaka jana hadi asilimia nne mwaka huu Januari.

Katika hali ya kawaida, ni dhahiri kuwa hali iliyopo sasa inachangia asilimia kubwa ya Watanzania kutafuta mbinu za kujikimu kimaisha kwa sababu sekta nyingi zimetikiswa na kusababisha biashara kufungwa, ambapo kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na gazeti dada la MTANZANIA, zaidi ya biashara 17,000 zimefungwa.

Pia tunaona kuwa benki zinayumba, baadhi ya viwanda vinapunguza wafanyakazi, mizigo bandarini imeelezwa kupungua na wananchi waliokopa ili kupata fedha za kusaidia kuendesha maisha, sasa wanalia hali ngumu; wanashindwa kufanya marejesho matokeo yake nyumba na mali zao zinapigwa minada kila kukicha.

Ili kupambana na hali hii, ni dhahiri kuwa vitendo vya rushwa vitazidi kuongezeka. Ila vitakuwa katika ustadi mkubwa ili kukabiliana na usimamizi imara wa Serikali iliyopo madarakani.

Licha ya Serikali ya Awamu ya Tano kujipambanua kupambana na rushwa, tunaona kuwa hali ya ugumu wa maisha yaweza kuchangia ongezeko la vitendo vya rushwa kwa sababu hadi sasa, takwimu zinaonesha kuwa vitendo vya rushwa bado vimekithiri nchini. Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Transparence iliyotolewa hivi karibuni inaonesha kuwa Tanzania ni nchi ya 116 kati ya nchi 177 duniani kwa kuwa na vitendo vya rushwa katika kipindi cha mwaka 2016. Lakini pia ni nchi ya 25 barani Afrika katika viwango hivyo vya rushwa. Nchi za Afrika Mashariki na viwango vya rushwa duniani ni Rwanda (50), Kenya (145), Uganda (151), Burundi (159) na Sudani Kusini 175. Mwaka 2014 Tanzania ilishika nafasi ya 119, mwaka 2013 ikashika nafasi ya 113 na 2012 Tanzania iliangukia nafasi ya 102 kwa rushwa duniani kati ya nchi 174. Kwa kuwa huu ni tamati ya mwaka wa pili wa Serikali ya Awamu ya Tano, Watanzania wengi macho na masikio yao wameyaelekeza kuona iwapo chini ya uongozi wa Rais Magufuli rushwa itaendelea kukithiri ama itapungua na kudhibitiwa.

Kutokana na pato la mtu mmoja mmoja kuendelea kuwa tete, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanaona bado hali itakuwa ngumu kudhibiti vitendo vya rushwa nchini kwa sababu kila mmoja atajilinda ili maisha yaendelee.

Mmoja wa wachambuzi hao, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, anasema nafasi ya 117 kidunia ni hali halisi kwamba Rais John Magufuli ana kazi kubwa ya kufanya.

“Sijui kama ataweza kupenya kwa vigogo. Nchi masikini kama Tanzania kuhusika kwa rushwa tutapata maendeleo kweli? Inasikitisha sana.”

Anasena ingawa Rais Magufuli ameonyesha nia, zinahitajika juhudi za ziada ili kasi aliyoanza nayo iendelee na aboreshe zaidi mikakati yake.

Hoja hiyo inaungwa mkono pia na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi ambaye anasema licha ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuonesha mfumuko wa bei za bidhaa kuwa unashuka, bado hali hiyo haiwezi kuondoa kilio cha ugumu wa maisha kwa wananchi.

“Bado wananchi wanazungumzia ugumu wa maisha kwa sababu bei za bidhaa na huduma zinaweza kuwa chini, lakini hawana kipato cha kununua. Fedha imepungua kwenye mzunguko na wengi hawana ajira, hivyo ni lazima wataona ugumu wa maisha kwa sababu hata kama bei zitakuwa chini hawawezi kununua,” anasema.

Wakati hayo yakiendelea Septemba mwaka huu, Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) limeitaja Tanzania kuwa nchi ya tano duniani ambayo uchumi wake unakua kwa kasi kwa asilimia 7.2, nchi inayoongoza ni Ethiopia uchumi wake ukitajwa kukua kwa kasi ya asilimia 8.3, Uzbekistna nafasi ya pili kwa kasi ya 7.6 na Nepal ikishika nafasi ya tatu uchumi wake ukikua kwa kasi ya 7.5.

Hayo yanajiri katika kipindi hiki ambacho asilimia kubwa ya wananchi wanakereka na takwimu hizo hasa ikizingatiwa wengi wao wanakosa hata pahali pa kujisitiri baada ya nyumba zao kubomolewa hususani katika mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.