Kimaadili hakuna kiongozi wa kulinganishwa naye

MIAKA 18 YA KIFO CHA MWL NYERE:

Rai - - WIK KUMBUKUMBU - NA HILAL K SUED

“Tanganyika” bali ilikuwa ni kuhusu hali mbaya ya makazi yake. Ilikuwa ni aibu kwa Serikali kuiacha nyumba ya rais mstaafu katika hali ile. Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi, iliitikia kilio hicho na mara moja ikapeleka mafundi na vifaa kukarabati nyumba ya Mwalimu.

J UMAMOSI itatimia miaka 18 kamili tangu kututoka Mwasisi wa Taifa hili na Rais wake wa kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyefariki katika hospitali moja mjini London, Uingereza.

Daima siishi kushangazwa kwamba kwanini Mungu Mwenyezi anakuwa mbahili wa kupindukia kwenye uzalishaji wa watu wazuri ili wawe viongozi katika Bara hili, watu wenye busara na uadilifu mkubwa, badala ya majambazi ambao kazi yao kuu baada ya kuingia madarakani ni kujilimbikizia mali, wao, wanafamilia wao na maswahiba.

Kweli kabisa ule usemi wa “Penye miti hukosa wajenzi.” Baada ya kulipa Bara letu utajiri mkubwa wa madini na maliasili nyingi, Mwenyezi Mungu akalikabidhi kwa maharamia wa aina ya Mafia kuliongoza.

Mwalimu alikuwa mmoja miongoni mwa viongozi wachache sana Bara hili lilibahatika kupata. Duniani alitukuzwa sana na maliberali wa mrengo wa kushoto kwa utetezi wake wa aina yake ya itikadi ya kisoshalist wa Kiafrika, ingawa pia alisulubiwa na wapinzani wake kama ni mtu ambaye harakati zake zilishindwa kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Lakini kutokana na hili la pili aliamua kung’atuka kwa hiari, kabla hata ya utamaduni uliokuja baadaye wa kulazimishwa kwa viongozi wengine barani Afrika kujiweka kwenye maamuzi ya raia zao kupitia chaguzi za demokrasia ya vyama vingi ambazo pia walizihujumu ili kuendelea kubakia madarakani.

Aidha, Mwalimu alikuwa miongoni mwa viongozi wachache barani humu ambao hotuba zake kadhaa bado zinaishi kwa kuwa na mantiki hadi leo na nukuu zake kutumika katika medani mbalimbali pamoja na vyuoni.

USAHIHI WA SERA YAKE YA MADINI IMETHIBITIKA

Kwa mfano usahihi wa sera yake kuhusu madini yetu ndiyo sasa unadhihirika, kwani katika enzi yake ya uongozi alisema ni vyema madini yakabakia huko huko ardhini hadi pale nchi itakapopata wataalamu wake wenyewe wa kuyachimba.

Hakusikilizwa, badala yake yule kiongozi aliyemwamini na kumwachia nchi akaanza kuleta wachimbaji wageni ambao kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wetu kupitia mikataba ya ovyo, walitukamua madini hayo hadi michanga wakasomba na kutuachia mapango yaliyo matupu.

H i v y o tunapoadhimisha miaka 18 ya kuondoka kwake na takriban miaka 56 tangu usiku ule aliposimama Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) akipokea saluti wakati bendera ya Uingereza (Union Jack) ikiteremshwa na ile ya Tanganyika mpya (ya kijani, nyeusi na dhahabu) ikipandishwa, ni vyema tukachukua muda kidogo kutafakari umuhimu wa Mwalimu kwa Tanzania.

ALIACHA OMBWE LA UONGOZI

Lazima tuwe wakweli, kuna kitu hakipo miongoni mwetu, ombwe kubwa la uongozi. Nahisi mara kadhaa anaweza hata kutikisika kaburini akijua aina ya uongozi uliojijenga baada ya kuondoka kwake; kupotea kwa vitu muhimu vilivyokuwa vinawaweka wananchi pamoja vikiwemo maadili, utawala bora unaozingatia sheria na uwajibikaji.

Pamoja na mapungufu yake mengi tu aliyokuwa nayo, mengine yakitokana na udhaifu wa kibinadamu, kitu kimoja kikubwa Nyerere alichowapatia Watanzania, ukiacha ukombozi wao kutoka kwa makucha ya ukoloni, ni heshima ya nchi yao mbele ya dunia.

Na katika suala la ukombozi, hakuishia kwa nchi yake tu, kwani alikuwa mstari wa mbele kabisa katika ukombozi wa watu wengine waliokuwa bado wanatawaliwa barani humu kama vile Angola, Msumbiji, Namibia na Afrika Kusini. Pia alikwenda nje ya Afrika katika kupigania haki za wengine waliokuwa wanakandamizwa kama vile Wapalestina na Wavietnam.

ALICHUKIA KUNYANYASWA WANANCHI

Sote tunakumbuka alivyokuwa anachukia udhalilishaji wa aina yoyote kwa wananchi wake. Si mara moja au mbili amewahi kuwatimua wageni waliokuja kufanya kazi hapa au kuwekeza (yaani kufanya biashara kama ilivyokuwa ikiitwa siku hizo) ilipobainika kwamba mgeni huyo alitukana au kunyanyasa wananchi wazalendo. Mara kadhaa alifanya hivyo kwa kuwapa muda mfupi, saa 24 tu kuondoka.

Leo hii kitu kama hicho hakuna, mgeni anayenyanyasa wananchi, hafanywi kitu chochote, sana sana wale wanaomtuhumu ndio huandamwa na pengine kufukuzwa kazi, iwapo ni wafanyakazi wa umma.

Lakini Mwalimu aliweza kulinda heshima ya mwananchi na kwa kiasi kikubwa aliweza kufanya hivyo kwa sababu yeye mwenyewe aliwaongoza wananchi wake kwa uadilifu mkubwa, hakuwa na wala hakutaka makuu, hasa katika kujilimbikizia mali.

Alifanya hivyo ili kutoa mfano kwa viongozi wenzake na hata kusisitiza kwa kuwawekea miiko mikali ya uongozi chini ya Azimio la Arusha. Alijua kuwa mamilioni ya Watanzania bado walikuwa katika umasikini mkubwa na hivyo viongozi wakijiingiza katika kujilimbikizia mali, basi kuna uwezekano mkubwa kuwasahau hao wananchi.

BINAFSI HAKUJILIMBIKIZIA

MALI

Watanzania wengi wanayafahamu yote hayo, hakuna mtu anayeweza sasa hivi kusema bila kutafuna maneno kwamba katika utawala wake Mwalimu alijilimbikizia mali. Hakuna. Kama wapo, ni waongo wakubwa, wanafiki waliokubuhu, wenye ajenda zao za siri. Yeye na familia yake waliishi maisha ya kawaida tu.

Binafsi nakumbuka kwa mara ya kwanza kabisa nilifika nyumbani kwa Mwalimu Msasani mwaka 1992, wakati akiwa anaishi kama rais mstaafu. Wakati huo nilikuwa mwandishi katika gazeti la Kiingereza la Family Mirror, miongoni mwa magazeti ya kwanza yaliyoanzishwa baada ya tasnia ya upashaji habari iliporuhusiwa kwa magazeti binafsi. Hivyo nilikuwa katika kundi la waandishi wa habari aliowaita kuzungumzia suala la hoja ya kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika iliyoanzishwa na kikundi cha wabunge kilichoitwa G55.

Baada ya kuandikisha majina yetu kwa mlinzi getini tulitembea kuelekea jumba la ghorofa moja umbali kama mita mia moja hivi. Lilikuwa jumba la kawaida tu, kama jumba lolote lile katika maeneo ya Magomeni, Ilala au Mwanayamala ambapo mpita njia hana sababu ya kulitupia macho mara mbili.

Wengi tulishtushwa kukuta hadhi ya nyumba ile, baadhi ya vioo vya madirisha ya luva (louvre) vimevunjika, nyavu zake za kuzuia mbu zimechanika, huku rangi za kuta imepauka. Binafsi nikafikiri labda jengo hili ni la walinzi na wafanyakazi wa Mwalimu na kudhani kuwa makazi yake halisi yalikuwa nyuma ya jengo.

ALIKATAA ANASA KWENYE MAKAZI YAKE MSASANI

Fikra hizi zilifutika muda mfupi baada ya kukaribishwa kwenye veranda iliyotazamana na Bahari ya Hindi kwa mbali na kutokana na picha nilizokuwa nikiziona katika magazeti ya Daily News na Uhuru miaka ya nyuma, hapa ndipo ilikuwa sehemu alipokuwa akikutana na kuongea na viongozi mashuhuri duniani wakati wa uongozi wake.

Baada ya muda tukatangaziwa ujio wa Mwalimu. Punde tukamwona anateremka ngazi (stairs) kutoka ghorofa ya juu akifuatana na katibu muhtasi wake wa miaka mingi, Joan Wickens, aliyekuwa na asili ya Uingereza na msaidizi wake mwingine wa kiume.

Akatupa mikono wote, nami ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kupeana naye mkono na akatuashiria kuketi. Viti havikutosha na wengine kati yetu ilibidi tusimame. Aliketi katika kiti chake cha bembea (rocking chair) akiipa mgongo Bahari ya Hindi. Kuna baadhi yetu walipata bahati ya kukaa katika viti vya sofa kama vitatu hivi, viti ambavyo, pamoja na kile kiti chake cha bembea, vilikuwa vimechoka na hali ilionyesha kulipaswa kuwepo kwa samani mpya.

Miaka ya nyuma watu mashuhuri duniani kama Henry Kissinger, Kenneth Kaunda, Gamal Abdel Nasser, Indira Gandhi na Fidel Castro, waliwahi kukaa katika sofa hizo.

Baada ya kuketi mkutano ukaanza lakini mawazo yangu yalikuwa kwingine kabisa, nikijaribu kuyatuliza akilini niliyoyaona. Ilikuwaje mtu huyu maarufu, shujaa wa ukombozi wa Bara la Afrika na ambaye hata baada ya kustaafu uongozi, aliendelea na umaarufu wake kwa kushikilia msimamo wake wa uongozi wa kimaadili na visheni yake ya ujamaa, kuridhika kuishi katika mazingira duni kama haya?

Na bila shaka mazingira kama haya ndiyo alikuwa akiishi hata wakati akiwa Rais, tabia inayoeleza jinsi Mwalimu alivyowapiku viongozi wengi sana Barani Afrika na hata duniani katika uadilifu na kujinyima. Kwa vipi alikataa maisha ya anasa, kitu ambacho angeweza kukipata wakati wowote kwa ishara ya vidole tu?

Wakati nikimsikiliza Mwalimu akitoa mashambulizi yake dhidi ya kikundi cha G55 ambao alisema walikuwa wanadhamiria kuuvunja Muungano (alisema labda hiyo itokee juu ya kaburi lake), mimi nilikuwa napandwa na hasira kwa nini viongozi aliowakabidhi madaraka waliamua kuyatelekeza makazi ya Mwalimu katika hali hii?

Siku ya pili yake habari kubwa katika magazeti mengi haikuwa kuhusu kile Mwalimu alichokieleza kuhusu hoja ya “Tanganyika” bali ilikuwa ni kuhusu hali mbaya ya makazi yake. Ilikuwa ni aibu kwa Serikali kuiacha nyumba ya rais mstaafu katika hali ile. Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi, iliitikia kilio hicho na mara moja ikapeleka mafundi na vifaa kukarabati nyumba ya Mwalimu.

Matokeo ya ukarabati huo yalionekana wiki tatu baadaye nilipotumwa na Mhariri wangu kwenda tena kumhoji Mama Wickens iwapo Mwalimu anakubaliana na uamuzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuipa Barabara ya Pugu (Pugu Road) jina lake yaani ‘Julius Kambarage Nyerere Road’.

Mwalimu alikuwa Butiama lakini baada ya muda Mama Wickens (bila shaka baada ya kuwasiliana na Mwalimu kwa simu) akanijibu kwa kusema Rais mstaafu hataki jina lake lipewe jina la barabara au kitu chochote kile wakati akiwa bado hai.

Hivyo Halmashauri ya Jiji wakaondoa “Julius Kambarage” kwenye alama za barabara na kubakia “Nyerere Road” kwani akina Nyerere walikuwa wengi waliozaliwa hapa duniani.

Ukarabati huo wa makazi ya Mwalimu Msasani ndio ulikuwa wa mwisho kwani waombolezaji waliofika nyumbani kwake mara tu baada ya kufariki kwake mwaka 1999 walishangaa kuona nyumba ikiwa katika hali mbaya, mapazia yamechanika, rangi za kuta zimepauka n.k na hapo hapo kuwaona mafundi wakiirekebisha hali hiyo.

ALIJALI ELIMU, WATOTO WAKE WALISOMEA HAPA HAPA

Leo hii baadhi ya wakuu wetu wa nchi wanaishi katika maisha ya pepo na anasa kubwa tofauti kabisa na hayo ya Mwalimu. Kuna baadhi wamejengewa mabwawa ya kuogelea karibu na vyumba vyao vya kulala.

Aidha, mapema miaka ya 70 nilipokuwa nafanya kazi Arusha kuna mtoto mmoja wa Mwalimu (simkumbuki vizuri ni yupi) alikuwa akisoma shule moja ya hapo, Arusha School. Shule hiyo ilikuwa ya bweni na Mkuu wa Mkoa, wakati huo Abdul-Nuru Suleman (sasa marehemu) alihisi mtoto huyo anapata adha kuishi shuleni.

Aliamua kumhamisha na kumweka nyumbani kwake huku gari la Serikali likimpeleka shuleni na kumrudisha kila siku. Mwalimu Nyerere alikuja kupata habari hizo na akamkaripia sana Mkuu huyo wa Mkoa na kumwamrisha kumrudisha bwenini mara moja kijana huyo.

Hivi ndivyo Mwalimu alivyokuwa, watoto wake walipata elimu humu humu nchini, kama watoto wa wananchi wengine. Leo hii, sababu kubwa inayotajwa kuzorota kwa elimu hapa nchini ni kwa wakubwa kuwapeleka watoto wao kusoma katika shule na vyuo vya nje. Katika hali hii wakubwa hawa hawajali sana matatizo yanayoikumba sekta ya elimu hapa na hivyo hawaoni umuhimu wa kuiboresha.

Mambo ni vivyo hivyo katika hospitali zetu na huduma za afya kwa ujumla. Hata wakati Mwalimu alipoanza kuugua, inasemekana alikuwa anapinga sana kupelekwa nchi za nje kutibiwa. Ingekuwa kuna uwezekano kwa Mwalimu kurudi katika uhai, ingawa kwa muda mfupi tu, angeweza kuwakemea sana akina Mkapa kwa kumwachia kwenda kufia katika nchi ya Wazungu, tena wale wale aliopambana nao katika kudai uhuru wa wananchi wake ili wajikomboe kutoka katika ujinga umasikini na maradhi.

Angeona Wazungu hao wangemsuta kwa kumwambia: “Baada ya miaka karibu 40 ya uhuru, mmeshindwa kujikomboa katika maradhi hadi wewe mwenyewe unaletwa kufia huku kwetu?”

Manyerere Jackton, mwanafamilia mmoja wa Mwalimu ambaye sasa ni mwanahabari na aliyewahi kuishi katika makazi ya Mwalimu ya Msasani miaka ya mwisho mwisho kabla ya kustaafu kwake, aliwahi kunihadithia jinsi Mwalimu alivyokuwa hapendi makuu.

Manyerere alisema kwamba baada ya watu wengi kuanza kujenga majumba karibu ya eneo hilo, pressure ya maji ya bomba majumbani ilikuwa inapungua, kwa hivyo mara kadha maji yalikuwa hayapandi juu ghorofani. Mapema asubuhi moja Manyerere alikuwa jikoni akitayarisha chai na mara alimwona Mwalimu amesimama mlangoni ameshika ndoo huku amevalia bukta ndefu na singlendi.

“Ee bwana eeh, leo tena maji hakuna kule juu na naona Waswahili wangu (akimaanisha wahudumu wake wa makazi yake juu ghorofani) bado hawajafika.”

Manyerere(alivyonihadithia)alimpokea ndoo na kumwambia arudi tu juu na kwamba atampandishia maji. Akamkingia maji katika ile ndoo na kumpandishia juu huku Mwalimu akimsubiri juu ya ngazi (stairs) ambapo alimpokea ndoo hiyo na kuingia nayo ndani. Mwalimu huyo!

Miaka 10 iliyopita, mfanyabiashara maarufu wa Sudan, Mohamed Ibrahim, alianzisha Tuzo ya kila mwaka kwa viongozi wastaafu wa barani Afrika waliojitokeza katika kusimamia (wakati wakiwa madarakani) uongozi uliotukuka na wa uadilifu, kudumisha utawala bora, kuwaendeleza wananchi wake, kutokumbatia ufisadi na kung’atuka kwa hiari na bila mizengwe kipindi chake cha utawala kilipomalizika.

Tuzo hii ingekuwapo enzi zile Mwalimu angeikwaa bila pingamizi yoyote.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.