Ni wachache wanaolia kuwa Magufuli ‘anabana’

Rai - - WIK KUMBUKUMBU - NA FRANCIS GODWIN, IRINGA

“NIMEPATA kura 803 kati ya kura 853 huu ni ushindi mkubwa na ni imani ambayo imeonyeshwa na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Iringa vijijini mkoani Iringa. Kazi iliyombele ni kuendelea kumuunga mkono Rais John Magufuli” hiyo ni kauli ya mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa- Arif Mbarak Abri baada ya kufanikiwa kunyakua nafasi hiyo.

Mbarak anasema amefurahishwa na kazi inayoendelea kufanywa na mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. Magufuli ndani ya chama pia nje ya chama kwa nafasi yake ya urais kwani kila mmoja anajivunia kuitwa mtanzania kutokana na kazi anayofanywa kiongozi huyo.

“Ni wachache kati ya wengi ambao wanaona kama Rais Magufuli anawabana ila tuliowengi tunaunga mkono kazi hiyo nzuri anayoifanya ndani ya chama chetu na nje ya chama kwa nafasi yake ya urais mambo yanakwenda vizuri na sasa hadi mataifa ya nje yanatamani kazi ya Rais wetu“

“Tuna deni kubwa kwa Rais wetu ambalo kila mtanzania ni kuendelea kumuombea afya njema ili azidi kutufikisha kwenye Taifa lenye uchumi wa viwanda na neema kwa kila mmoja bila kubaguana “

Akielezea hatua ya CCM kutoanika majina ya wagombea kama ilivyokuwa zamani kwa wagombea kuanza kutangaza nia kisha kuzunguka kufanya kampeni na baadhi yao kutumia rushwa ili kupita nafasi walizoomba, Abri anasema kuwa heshima kubwa ya CCM imeonekana katika uchaguzi huu kuanzia ngazi za chini hadi wilaya kutokana na wagombea wote kutojulikana hadi siku ya uchaguzi .

“Utaratibu huu umeongeza heshima kubwa kwa chama chetu ila pia umeonyesha nguvu ya CCM na mtaji wake mkubwa ni watu “anasema.

Viongozi ambao wamepatikana sasa ni viongozi ambao ni wawajibikaji kwa wanachama waliowachagua kutokana na kutotumia pesa kupata uongozi hivyo lazima watawajibika zaidi kwa kuwa wasipofanya hivyo watawajibishwa bila kuogopwa .

Anasema hata wachama ambao huwa huwageuza wagombea kitega uchumi kwao kwa uchaguzi huu imekuwa vigumu kwani hakuna aliyeingia ukumbini akiwa amefanya kampeni zaidi ya kutumia jukwaa kuomba kura .

Msimamizi wa uchaguzi huo mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini Mahamudu Mgimwa akitangaza matokeo ya uchaguzi huo alisema upande wa nafasi ya ujumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa wagombea walikuwa 10 na waliohitajika ni watatu pekee .

Aliwataja wagombea hao na idadi ya kura zao katika mabano kuwa ni Arif Abri (803), mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela (589) , Velentino Msuva (363) ambao ndio walioshinda nafasi hiyo huku waliokosa ni Ritha Mlagala (182), Bertha Luhavi (182), afisa tarafa ya Kalenga, Adestino Mwilinge (134), Shakila Kiwanga (118), mfanyabiashara Jeremia Msofa (80) na mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa Stephen Mhapa (76).

Wakati nafasi ya ujumbe mkutano mkuu wa CCM mkoa nafasi zilikuwa mbili na wagombea walikuwa wawili Nuru Mkeng’e na Shafi Sambu ambao walipita bila kupingwa.

Nafasi ya ujumbe wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya wagombea walikuwa 25. Nafasi zilizokuwa zikitakiwa ni wajumbe 10. Waliochaguliwa katika nafasi hiyo ni Stanslaus Mhongole (477), Jeremia Msofa (450), Adestino Mwilinge ( 437), Christopher Mahembe ( 348),Wensi Minzi ( 316) Abel Mgimwa (276) ,Mombeyega Asecheki ( 278), Godliva Mvanda ( 263),Abel NYamhanga (243) na Jodith Waziri (231)

Nafasi ya mwenyekiti ambayo iliwaniwa na wanachama watatu baada ya vikao vya juu kukata jina la aliyekuwa mwenyekiti wa CCM wilaya ya Iringa vijijni, Adelphina Mtafilalo wagombea waliochuana ni watatu ambao ni diwani kutoka jimbo la Ismani Costandino Kihwele, wawili kutoka jimbo la Kalenga Shakila Kiwanga na Shaaban Kipufya. Katika uchaguzi huo Kihwele aliibuka mshindi kwa kupata kura 576 huku akifuatiwa na Shakila aliyepata kura 234 na Kipufya akipata kura 33.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.