Polepole amekumbwa na nini?

Rai - - WIK KUMBUKUMBU - JIMMY CHARLES 0688 063839

MIONGONI mwa vijana wachache niliokuwa nikiamini kuwa ni hazina ya nchi katika kuwasemea wasio na sauti ni Humphrey Polepole.

Nikiri wazi kabla ya Aprili 6,2012 Polepole hakuwa midomoni wala vichwani mwa Watanzania wengi.

Hakupata nafasi hiyo kwa sababu hakuwa na kitu au jambo lililomlazimisha ama kumsukuma kuwa mjadala.

Baada ya Rais wa awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kumjumuisha ndani ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Joseph Warioba aliyekuwa akisaidiwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Augostino Ramadhani na kuundwa na manguli wa sheria, ndipo kijana Polepole alipochomoza.

Lakini si tu alichomoza kwa sababu ya kujumuishwa kwenye Tume hiyo iliyompa nafasi ya kujumuika pamoja na manguli wa sheria, lakini pia alionesha uwezo wa hali ya juu wa kusimama imara, kujenga na kutetea hoja.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba mbali ya kuundwa na viongozi wake ambao nimewataja hapo juu, lakini pia ilikuwa na wajumbe 30 waliogawanyika katika makundi mawili, kundi moja la wajumbe 15 kutoka Zanzibar na kundi la pili kutoka Bara.

Tume ilikuwa na watu makini kama Prof. Mwesiga Baregu, Riziki Mngwali, marehemu Dk. Edmund Sengodo Mvungi, Richard Lyimo, John Nkolo, Alhaj Said EL – Maamry, Jesca Mkuchu, Prof. Palamagamba Kabudi, Yahya Msulwa, Esther Mkwizu, Maria Kashonda, AlShaymaa Kwegyir. Mwantumu Malale na Joseph Butiku kwa upande wa Bara.

Kwa upande wa Zanzibar wajumbe walikuwa ni

Dk. Salim Ahmed Salim, Fatma Said Ali,Omar Sheha Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali Said, Ussi Khamis Haji, Salma Maoulidi, Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohamed Saidi, Muhammed Yussuf Mshamba,Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed, Abubakar Mohammed Ali na Ally Abdullah Ally Salehe.

Sekretarieti ya Tume hii iliongozwa na Katibu Assaa Ahmad Rashid na Naibu wake alikuwa ni Casmir Sumba Kyuki, hawa wote hawakuwa watu dhaifu na sitaki kuamini kama walikuwa na mikono michafu, kilikuwa ni kikosi kilichobeba matumaini ya Watanzania wengi katika kupata Katiba Mpya.

Na kwa hakika hadi leo heshima ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni kubwa na imeendelea kusalia mioyoni mwa watu tofauti na ilivyokuwa kwa Bunge Maalum la Katiba ambalo lilibeba sura ya kupindisha kile kilichohitajiwa na wananchi, ingawa nao walifanya kazi kubwa kulingana na matakwa yao. Msingi wa andiko langu la leo si kujadili makosa yaliyofanywa na Bunge Maalum la Katiba, natambua walichokifanya kwa wakati ule kilikuwa ni kwa maslahi yao.

Hoja iliyonisukuma kufanya rejea ya yote hayo ni Polepole, ambaye kama nilivyoandika hapo juu, yeye alikuwa ni miongoni mwa wajumbe wa Tume akiwakilisha Bara.

Pamoja na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuundwa na wajumbe 30 na viongozi wawili, ukweli ni kwamba Polepole ndiye aliibuka kuwa nyota wa kikosi kazi kile.

Mara baada ya Tume kuwasilisha maoni ya wananchi kwa Rais na kufikishwa bungeni mwaka 2014, ambako maoni yalikutana na vipingamizi kadhaa nje na ndani ya Bunge la Katiba, Polepole ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kusimama na kutetea kila alichokiamini ambacho kilikuwa ni matakwa ya wananchi.

Polepole alikuwa mstari wa mbele kutoa maelezo, ufafanuzi na kukabiliana kwa hoja na waliokuwa wapinzani wa rasimu ya Katiba iliyowasilishwa, akijipambanua kama muumini wa haki na usawa.

Halikuwa jambo la ajabu kuona akipongezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, tume ilikuwa na wajumbe wengi, lakini wengi wao walikuwa kimya ni yeye ndiye aliweza kukabiliana na upotoshaji uliokuwa ukifanywa na wale waliokuwa wakiikosoa rasimu yao.

Baadhi ya watu ndani ya mitandao ya kijamii walipata kusema kuwa Polepole ni hazina inayopaswa kulindwa , alipata hadhi hiyo kwa sababu aliweza kupambana kisawasawa na upotoshaji uliofanywa na waliokuwa wakikataa kile kilichokusanywa na Tume.

Kwa wakati huo wapo waliokwenda mbali zaidi na kudai kuwa kuwa Humphrey Polepole ni zaidi ya wabunge wote wa Chadema ... ukimtoa Tundu Lissu, huenda yalikuwa ni mawazoi yao yaliyosukumwa na nia njema ya Polepole kwa wakati ule.

Ikumbukwe kuwa wakati Polepole akionekana na wengi kuwa shujaa na hazina ya nchi alishajipambanua kuwa yeye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini mwenendo na matamshi yake yalimfanya kuonekana mwanachama tofauti kabisa na wengine wengi wa chama hicho kwa sababu alikuwa akisimamia haki za wengi.

Hatua hiyo iliwasukuma baadhi ya watu ndani ya mitandao ya kijamii kutamani kijana huyu atunukiwe shahada ya Heshima kwa sababu aliweza kumshinda kwa hoja Mwigulu Nchemba walipowahi kukutana kwenye baadhi ya vipindi vya Televisheni ya Star Tv.

Jambo la ajabu ambalo limenisikitisha na kutamani kujua Polepole amekumbwa na nini ni kauli yake iliyonukuliwa mwanzoni mwa wiki hii na gazeti moja la kila siku kuwa eti! Wamebaini kuwa mchakato wa Katiba uliofikia hatua ya kupata Katiba Inayopendekezwa, umepita kwenye mikono michafu hivyo kuna hatari ya kupata Katiba chafu!

Ajabu sana, nimeshindwa kumwelewa kijana huyu amekumbwa na nini, sitaki kuamini kama nae anajilazimisha kulewa madaraka, sitaki kuamini kama Polepole yule wa 2014 aliyejinasibu kuwa mpigania haki ndiye amebadilika kwa kasi kiasi hiki.

Sitaki kuamini kwa sababu kama ni suala la mikono michafu basi hata yeye ni miongoni mwao na hawezi kujitoa kwenye bakuli la wenye mikono michafu.

Nini kimemfanya Polepole apotoke namna hii, anataka kusema nini juu ya kile kilichofanywa na Rais mstaafu juu ya Katiba Mpya, anataka kuwaaminisha nini Watanzania anatoa wapi jeuri ya kujitukana mwenyewe, kwanini anayasema haya leo?

Hebu Polepole asimame hadharani na kuweka wazi hiyo mikono michafu ilianzia wapi, je, ni kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo yeye alikuwa miongoni mwao au ndani ya Bunge Maalum la Katiba ambalo baadhi ya wakubwa zake wa leo walikuwamo ndani ya Bunge hilo!

Naweza kumwelewa kama atatoa ufafanuzi zaidi wa kauli yake hiyo iliyonukuliwa na gazeti hilo la kila siku lililotoka Oktoba9, mwaka huu.

Sina mashaka na uwezo wa Polepole, bado nina imani nae, huenda alikengeuka na atajitokeza kuwaomba radhi Watanzania kwa sababu yeye ni miongoni mwa Watanzania wachache waliotumia fedha za wavuja jasho kuzunguka kule na huko kusaka maoni ambayo kumbe yeye alijua wazi kuwa mchakato unapita kwenye mikono michafu.

Nimwombe Polepole kwa busara na uungwana ule ule aliopata kuwa nao ambao bado naamini anao, asione soni kusema samahani kwa kauli yake hiyo na kama haioni haja hiyo basi si dhambi akatufafanulia ni wapi mchakato ulikutana na mikono michafu. Natamani kumsikia tena Polepole.

Halikuwa jambo la ajabu kuona akipongezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, tume ilikuwa na wajumbe wengi, lakini wengi wao walikuwa kimya ni yeye ndiye aliweza kukabiliana na upotoshaji uliokuwa ukifanywa na wale waliokuwa wakiikosoa rasimu yao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.