Tamko la Askofu Shoo ndio msimamo wa KKKT

Rai - - MAKALA -

Baada ya mijadala katika mtandao ya kijamii, napenda kuweka wazi kwamba naunga mkono kabisa tamko la Mkuu wetu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dk. Fredrick Shoo (pichani) juu ya mashambulizi ya Watazania hususan Tundu Lissu alilolitoa siku kadhaa zilizopita akiwa Ujerumani. Ile ni kauli ya Kanisa letu.

Ieleweke kwamba KKKT ni Kanisa moja na mmoja wetu anapochaguliwa kuliongoza basi Maaskofu wengine wote tunaheshimu na kusimama pamoja naye pasipo tashwishwi zozote. Hatugombanii vyeo bali tunatunza umoja wa ushuhuda wetu ikiwemo utume wa kinabii wa kanisa.

Tunaheshimu misingi ya demokrasia tuliyojiwekea katika kupata viongozi wa kanisa pasipo uchungu wala hila. Akisha kuchaguliwa mmoja wetu tunakubali kwa moyo mweupe na kusimama pamoja naye ili kazi ya Mungu na utume wa kanisa uendelee mbele. Kwetu sisi kuongoza kanisa sio utawala bali ni utume huku tukiheshimu sana maamuzi ya wafuasi wa Kristo ndani ya Kanisa.

KKKT imekuwa mfano mzuri wa kuheshimu maamuzi ya watu na hivyo tumekuwa mfano bora wa demokrasia. Mkuu wetu wa Kanisa alipohoji mambo kuhusu kushambuliwa mchana kweupe kwa Lissu na ukimya wa mamlaka zilizopo kutosema kitu hiyo ni kauli ya KKKT. Na tena kuangaliza kwamba watazaliwa Malissu wengI hiyo ni kauli ya Kanisa letu.

Bado tunangoja majibu juu ya tukio hili la kinyama alilofanyiwa Lissu na ambalo limeamsha hofu miongoni mwa jamii. Ieleweke kwamba mimi binafsi kama Mwenyekiti wa Kamisheni ya Haki na Amani ya KKKT nasimama na Mkuu wetu wa Kanisa katika hili pamoja na matukio mengine ya kutishia amani ya jinsi hii.

Vilevile ieleweke kwamba kanisa zima liko pamoja naye. Mkuu wetu wa Kanisa kwa mapokeo yetu anawajibika kusimamia utume wa kinabii. Nitasimama naye katika mambo haya ya unabii wa kanisa na kanisa zima litasimama pamoja naye pasipo utata. Napenda jambo hili lieleweke kwa wale wote waliokuwa wakizungumza katika mitandao ya kijamii.

Nayasema haya wazi kwa sababu wapo watu ambao wameanza kusema kwamba kauli hizi za kinabii ni za kanisa la Kaskazini mwa Tanzania. Hayo ni mawazo potofu na ya watu ambao wanagawa nchi yetu katika kanda. Huo ni upotofu ambao sikubaliani nao. Tena ni mawazo ya watu ambao dhana ya demokrasia imekuwa ngumu kwao.

KKKT siku zote imesimamia haki na hapa tukumbuke tamko la Bagamoyo lililotolewa na mababa zetu waliotutangulia wakati wa awamu ya pili ya utawala wa nchi yetu. Sisi tunasimama katika roho ileile ya unabii waliyokuwa nayo baba zetu. Hatutayumba bali tutaendelea kusimama katika kweli na haki kama jinsi Mungu alivyotuita na kututuma kwenda ulimwenguni mwote kuihubiri Injili.

Utume huu ni wa kuhubiri kweli na haki. Ni ujumbe huu ambao ni uzima na mauti kwa maaskofu wa wachungaji wote wa KKKT.

Popote atakapoitwa Askofu Dk. Shoo kwa mahojiano au vinginevyo juu ya utume wa kweli na haki (kuhusiana na kauli aliyoitoa) nitasimama pamoja naye katika utume huu.

Hata hivyo, narudia tena kusema kwamba KKKT ni moja na asitokee yeyote kutugawa kiukanda au kikabila. Askofu Dk. Fredrick Shoo ndiye Mkuu wa KKKT na sisi Maaskofu wote wa KKKT nchi nzima tuko pamoja naye.

Askofu Dk. Stephen Munga, Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, na Mkuu wa Chuo Kikuu SEKOMU.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.