UN na changamoto mpya ya Korea Kaskazini

Rai - - KIMATAIFA / KATUNI - NA ABBAS MWALIMU Abbas Mwalimu (Abbas Abdul Mwalimu) Facebook Abbas Abdul Mwalimu Simu +255 719 258 484 Instagram @abbasmwalimu Twitter @MwalimuAbbas

KATIKA siku za karibuni tumeshuhudia nchi za Marekani na Korea Kaskazini zikitoleana vitisho, hali ambayo imeendelea kuzua sintofahamu katika ustawi wa amani na usalama duniani.

Makala hii inaangazia mgogoro uliopo kwa kuyatazama majukumu ya Umoja wa Mataifa na hasa kupitia Baraza lake la Usalama.

Umoja wa Mataifa ulianzishwa mwaka 1945 ukichukua nafasi ya Jumuiya iliyokuwepo kabla yake ambayo ilijulikana kama League of Nations.

Umoja wa Mataifa una malengo makuu manne kama yalivyoainishwa katika ibara ya kwanza ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa (The United Nations Charter), ambayo ni haya yafuatayo;

(1) Kuimarisha amani na usalama duniani

(2) Kuleta mahusiano ya kirafiki baina ya mataifa duniani

(3) Kuleta ushirikiano wa kimataifa katika kutatua matatizo ya kimataifa ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na yale yenye tabia ya kibinadamu.

(4) Kuwa kitivo cha kuunganisha utendaji wa mataifa katika kuyafikia malengo yake.

Umoja wa Mataifa umegawanyika katika mizizi saba ambayo kimsingi ndiyo inayoundwa Umoja huu;

(1) Baraza Kuu (General Assembly)

(2) Baraza la Usalama (Security Council)

(3) Baraza la kiuchumi na kijamii (Economic and Social Council)

(4) Baraza la Wadhamini (The Trusteeship Council)

(5) Kamati Kuu (The Secretariat)

(6) Mahakama ya Kimataifa ya Haki (The International Court of Justice) ambayo ina wajibu wa kutatua migogoro ya kimipaka na kutafsiri matukio ya kimahusiano kama lile la kuuawa kwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa ndugu Bernadote nchini Israel mwaka 1948.

Kwa lengo la kutaka kufahamu kinachojiri katika mgogoro baina ya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini, makala haya yatajikita zaidi katika kuelezea namna migogoro inavyotatuliwa na Umoja wa Mataifa na hasa ndani ya Baraza la Usalama la Umoja huu, maamuzi linayoyafanya sambamba na changamoto linazokabiliana nazo.

MUUNDO WA BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaundwa na wanachama 15. Kati ya hao, wanachama watano ni wa kudumu na 10 ni wale wasio wa kudumu. Wanachama wa kudumu wa Umoja wa Mataifa ni nchi za China, Ufaransa, Urusi (ambayo ilirithi kutoka kwa iliyokuwa Jamhuri ya Muungano wa Kisovieti-USSR mwaka 1990), Uingereza na Marekani.

KWANINI NCHI HIZI TANO ZIMEITWA WANACHAMA WA KUDUMU UN?

Sababu kuu inayoelezwa ni kutokana na mchango wao katika kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa-UN na kwa mantiki hiyo zitaendelea na wajibu wao wa kuimarisha amani na usalama duniani.

Katika Baraza la Usalama nchi hizi wanachama wa kudumu wa UN zimepewa upendeleo wa nguvu ya kipekee ya kura iitwayo kwa kingereza ‘Right to Veto’ yaani ‘Haki ya Kura ya Turufu.’

Nchi 10 zilizobaki ambazo si wanachama wa kudumu hupatikana kwa mzunguko wa kikanda ambapo nchi huchaguliwa kukamilisha idadi ya wanachama 15 ambao wanatoka kanda za Afrika, Asia, Ulaya Mashariki, Mataifa ya Kilatini, Ulaya Magharibi na nchi nyingine. Mzunguko huu hudumu kwa muda wa miaka miwili. Tanzania iliwahi kuwa mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja huu mwaka 2008 mpaka 2010 ikiliwakilisha bara la Afrika ambapo Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete alipata kushiriki vikao vyake.

UN INAVYOTATUA MIGOGORO DUNIANI

Kwa mujibu wa ibara kubwa ya sita yaani Chapter VI inayozungumzia utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani (Pacific Settlement of Disputes), ibara ndogo ya 33 inazitaka pande hasimu kutatua mgogoro baina yao kwa njia za amani.

Njia hizi za amani ni kama vile njia ya majadiliano yaani Negotiations, njia ya upatwanishi yaani Mediation, njia ya utatuzi wa kimahakama yaani Arbitration sambamba na maamuzi ya kimahakama bila ya kusahau jumuiya za kikanda kama vile Umoja wa Afrika -AU, Jumuiya ya Afrika ya MasharikiEAC, Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) na Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Kusini mwa Afrika yaani SADC.

Kwa mujibu wa ibara ya 34, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litachunguza kuona kama mgogoro huo unaweza kuleta msuguano wa kimataifa na kuhatarisha uimarishwaji wa amani na usalama duniani.

Baraza la Usalama linapopelekewa mgogoro na nchi mwanachama wa UN (Ibara ya 35 ikichukua kutoka ibara ya 34), linaweza kutoa mapendekezo juu ya hatua stahiki za kuchukuliwa ili kutatua mgogoro huo kwa kutathmini hatua zilizochukuliwa na pande zilizo katika mgogoro sambamba na mwongozo wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, huku ikizingatia haki za msingi za pande hizo hasimu.

Endapo pande hasimu zitashindwa kufikia mwafaka kwa kutumia njia zilizotajwa kwenye ibara ya 33, zitawasilisha suala hilo kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa sambamba na Baraza la Usalama la umoja huo.

Baraza la Usalama litachunguza kuona kama endapo mgogoro huo ni kweli unahatarisha uimarishwaji wa amani na usalama duniani na kuamua ama kufanya uamuzi kwa mujibu wa ibara ya 36 ama kushauri njia bora za usuluhishi ambazo Baraza litaona zinafaa bila ya kuathiri ibara ya 33 mpaka ya 37.

Baraza la Usalama huzishauri pande hasimu kusuluhisha mgogoro wao kwa njia za amani (Pacific ways). Ibara ya 38 (2) imekazia suala hilo hilo la utatuzi wa migogoro kwa njia za amani.

Katika eneo hili tunatarajia kuona ile bodi ya Ushauri Juu ya Upatanishi iliyoundwa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterrez ambayo ndani yake yupo Mwanadiplomasia mahiri wa Tanzania, Balozi Asha-Rose Migiro, ikifanya kazi yake kwa ufanisi wa hali ya juu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.