Dk. Kigwangalla akalia kuti kavu

»Mawaziri wa zamani watoa ushauri »Dk. Charles Tizeba ashangilia

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

TAYARI Dk. Kigwangalla ameshaliona tatizo la Loliondo na ameliweka kwenye vipaumbele vyake vitatu ambavyo amehidi kushughulika navyo, vingine ni kupambana na ujangili pamoja na kutangaza vivutio vya utalii.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla ndiye waziri pekee ndani ya Baraza jipya la mawaziri lililotangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita aliyekalia kuti kavu kutokana na ugumu wa wizara aliyopewa. RAI linachambua.

Rais Dk. John Magufuli mwishoni mwa wiki iliyopita alifanya mabadiliko makubwa kwenye Baraza lake la Mawaziri kwa kuongeza wizara mbili, kuwaacha mawaziri wanne na kupandisha Manaibu Waziri kuwa mawaziri kamili.

Hatua hiyo imekuja baada ya baadhi ya wizara kukaa kwa muda mrefu bila mawaziri na nyingine kukosa manaibu waziri.

Kabla ya uteuzi huu, wizara mbili ya Nishati na Madini ambayo sasa imegawanywa ilikuwa wazi pamoja na Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Wizara ya Nishati na Madini ambayo ilikuwa mwiba kwa mawaziri wake sasa imegawanywa na kuwa wizara mbili tofauti huku Nishati ikisimamiwa na Dk. Medard Kalemani ambaye atasaidiwa na Subira Mgalu na Madini ikisimamiwa na Angellah Kairuki ambaye atasaidiwa na Stanslaus Nyongo.

Aidha, wizara mbili ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu ilikosa Naibu Waziri kwa zaidi ya miezi saba baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Dk. Abdallah Posi kuteuliwa kuwa Balozi na Wizari ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, nayo haikuwa na Naibu Waziri mwezi mmoja baada ya aliyekuwa akikalia kiti hicho Edwin Ngonyani kujiuzulu.

Katika kuhakikisha Rais anajaza nafasi zilizokuwa wazi pamoja na kuongeza ufanisi, Rais Dk. Magufuli amewaacha mawaziri wanne alioanza nao.

Mawaziri hao ni aliyekuwa Waziri Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge ambaye nafasi yake imechukuliwa na Mbunge wa Katavi, Mhandisi Issack Kamwele aliyekuwa Naibu waziri wa wizara hiyo.

Panga hilo limempitia pia aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Annastazia Wambura ambaye nafasi yake imechukuliwa na Mbunge wa Viti Maalum CCM, Juliana Shonza.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani naye ametupwa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ambaye nafasi yake imechukuliwa na Dk. Hamis Kigwangwala aliyekuwa Naibu Waziri Wizara ya Afya.

Wakati hali ikiwa hivyo, mwenendo wa historia ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii unaonesha wazi kuwa Dk. Kigwangalla ni miongoni mwa mawaziri ambao wana nafasi kubwa ya kutumbuliwa kabla ya muhula wa kwanza wa Rais Magufuli kwisha au wasipate nafasi ya kuingia barazani kwenye awamu ijayo kama Rais atawania na kushinda tena urais pamoja na umri wake kuwa mdogo.

Ingawa Kigwangalla anatazamwa kama mwanasiasa mwenye misimamo na mwenye kufanya kazi kwa weledi, lakini anaingizwa kwenye kikaango hicho kutokana na historia mbaya wanayokumbana nayo mawaziri ndani ya wizara yake mpya.

Wizara ya Maliasili na Utalii inatajwa kuwa ni kaa la moto kama ilivyokuwa kwa Nishati na Madini kabla ya kugawanywa.

Ukweli wa hilo unadhibitishwa na hatua ya kutupwa nje ya wizara Prof. Maghembe ambaye alirudishwa kwenye wizara hiyo kwa mara ya pili, ambapo mara ya kwanza alihudumu wakati wa utawala wa Serikali ya awamu ya Nne.

Prof. Maghembe alikuwa akitajwa kama miongoni mwa mawaziri wasiopenda kupindisha mambo na kwamba hata baadhi ya masuala aliyoyasimamia katika kipindi chake chote ndani ya wizara hiyo kilikuwa ni msimamo wa Serikali.

Hata hivyo, kuwa na msimamo hakumfanyi waziri yeyote anayeongoza wizara hiyo kuepuka anguko lake ndani ya muda mfupi au hata mrefu.

Dk. Kigwangalla anachukua wizara hiyo akiwa na mtihani mzito mbele yake wa kumaliza mgogoro wa pori tengefu la Loliondo lililopo ndani ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Wakati Prof. Maghembe akiwa Waziri wa wizara hiyo aliwahi kuingia kwenye msuguano wa kimaamuzi na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambaye alipuuza uamuzi wa wizara huyo ambaye alitaka kutengwa eneo la kilomita za mraba 1,500 kwa ajili ya pori tengefu la Loliondo

Mbali na kutolea uamuzi kilomita hizo, pia alisema kilomita za mraba 2,500 ambazo zilikuwa sehemu ya pori tengefu Loliondo, zinarejeshwa kwa wananchi kwa lengo la kuhifadhi Ikolojia ya Serengeti ambayo sasa ipo hatarini.

Gambo alipuuza agizo hilo na kutangaza kuendelea kwa majadiliano ya kutafuta suluhu, ingawa waziri alishatoa uamuzi.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwaambia waandishi wa Habari kuwa kamati aliyounda kutafuta suluhu inaendelea kama alivyoagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kwamba tamko la Waziri ambalo lilinaonekana kuhitimisha kazi ya kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Loliondo uliodumu kwa zaidi ya miaka 25 ni maoni tu.

Tayari Dk. Kigwangalla ameshaliona tatizo la Loliondo na ameliweka kwenye vipaumbele vyake vitatu ambavyo amehidi kushughulika navyo, vingine vikiwa ni kupambana na ujangili pamoja na kutangaza vivutio vya utalii.

Alisema atayatekeleza hayo matatu ili kuifanya wizara hiyo isonge mbele na kwamba atatumia muda wake mwingi kuwekeza katika kutangaza vivutio nchini kwa sababu eneo hilo limekuwa na changamoto nyingi ikiwamo rasilimali fedha.

“Nitaweka nguvu zangu na kuweka mbinu mpya kutangaza vivutio kwa sababu ni eneo ambalo limekuwa na changamoto nyingi. Pia nitamaliza mgogoro wa Loliondo mkoani Arusha, nitahakikisha unafika mwisho.

“Jambo jingine ambalo nitalishughulikia ni kupambana na ujangili,”alisema.

Ukwlei ni kwamba tatizo kubwa ambalo linaweza kuwa mwiba kwa Dk. Kigwangalla ni mgogoro huo wa Loliondo na kwamba kama asipokuwa makini anaweza kujiingiza kwenye mtifuano na Gambo na upo uwezekano wa kutumbuliwa mapema.

Aidha, historia inaonesha Wizara hiyo kuwa kaa la moto kwa wanasiasa walioteuliwa kuiongoza, katika kipindi cha miaka 25, imeshaongozwa na mawaziri 11 tofauti.

Tangu mwaka 1988 ni waziri mmoja tu, Zakhia Meghji ndiye aliweza kudumu kwa muda mrefu akiiongoza wizara hiyo kwa miaka minane kuanzia 1997 hadi 2005.

Kumbukumbu zinaonyesha pia kuwa awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete wizara hiyo imetia fora kwa kubadili mawaziri, tangu mwaka 2005, iliongozwa na mawaziri watano tofauti na ilivyokuwa wakati wa awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa iliongozwa na mawaziri wawili.

Wafuatiliaji wa mambo ya siasa wanaamini kutodumu huko kwa mawaziri kunatokana na mapato makubwa yanayotokana na rasilimali kama za utalii na uwindaji ambavyo vimesababisha kuwapo kwa tuhuma nyingi za rushwa na ufisadi.

Kashfa nyingi katika wizara hiyo zimeitikisa Serikali mara nyingi kama ile ya uuzaji wa pori la Loliondo, kuuzwa kwa hoteli za kitalii zilizokuwa zinamilikiwa na Serikali kwa bei ya kutupa, uuzwaji wa vitalu na biashara ya pembe za ndovu na vipusa.

BAADHI YA MAWAZIRI WATOA NENO

Baadhi ya mawaziri waliowahi kukalia kiti cha wizara hiyo walielezea changamoto walizokabiliana nazo katika kipindi cha uongozi wao.

Arcardo Ntagazwa alisema tatizo lililopo kwa viongozi wa sasa ni kufanya uamuzi bila kumuogopa Mungu... “Wanasiasa na viongozi wa kada mbalimbali wanatakiwa kumtanguliza Mungu kabla ya kuchukua uamuzi, lakini pia wanatakiwa kutambua kuwa wao ni watumishi wa watu.”

Alisema akiwa waziri wa wizara hiyo aliwahi kuongoza Operesheni Uhai ambayo ililenga kutokomeza vitendo vya ujangili kama ilivyokuwa Operesheni Tokomeza Ujangili, na kusema hii iliyofanywa miaka michache iliyopita ilikithiri matukio ya ajabu.

Kwa upande wake, Anthony Diallo ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa wizara hiyo anae alipata kuliambia RAI kuwa: “Wizara ya Maliasili na Utalii imezungukwa na watu ambao wana mambo yao wanayafanya. Sasa kama kuna waziri ambaye ni mgumu (siyo rahisi kurubuniwa), lazima atawekewa vikwazo tu.” Alisema wakati akiwa waziri kulikuwa na baadhi ya watu wakiwamo watendaji wa Serikali waliomtengenezea majungu kutokana na kuwabana katika biashara zao za uvunaji wa magogo.

“Kipindi hicho tembo waliuawa wengi, uwindaji haramu pia ulikuwa ukifanyika,” alisema Diallo, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza.

Alisema baadhi ya viongozi hivi sasa hawajiamini katika utendaji wao wa kazi kutokana na kupata madaraka hayo kwa fedha zao. Alimtolea mfano Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli (sasa ni Rais) kuwa mmoja kati ya mawaziri wanaotenda kazi zao kwa kujiamini, mpaka kufikia hatua ya Serikali kuingilia uamuzi wake mara kadhaa na kuzuia utekelezaji wa jambo fulani ambalo aliliamua lifanyike.

Mawaziri wa aina hii wamebaki wachache. Lakini kinachonishangaza ni kufanyika kwa Operesheni Tokomeza huku ikihusisha wizara zaidi ya moja, ilitakiwa isimamiwe na wizara moja ili kuondoa mwingiliano wa kiuamuzi, hakukuwa na utaratibu wa kupeana taarifa,” alisema.

ORODHA YA MAWAZIRI TANGU 1988

ARCADO NTAGAZWA

Aliongoza wizara hiyo kuanzia mwaka 1988 hadi 1990. Hakurudishwa kwenye wizara hiyo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1990. Katika kipindi hicho, wizara hiyo ililaumiwa kwa hatua yake ya kubinafsisha hoteli mbalimbali za kitalii zilizokuwa zinamilikiwa na Serikali kwa bei ya kutupa. Hoteli hizo ni pamoja na Lake Manyara, Ngorongoro, Seronera na Lobo. Hoteli hizo zilijengwa kwa gharama kubwa kwa msaada mkubwa wa serikali ya Israel. Pia uuzaji wa Hoteli za Mount Meru kwa kampuni ya Accor ya Ufaransa na ile ya Mikumi ilisababisha malalamiko makubwa.

ABUBAKARI MGUMIA

Mbunge huyo wa zamani wa Tabora Mjini aliongoza wizara hiyo kuanzia mwaka 1990 hadi 1993. Katika kipindi cha uongozi wake ndipo Shirika la Utalii Tanzania (TTC) lilibadilishwa na kuwa Bodi ya Utalii. Katika kipindi hicho kulitokea malalamiko ya uharibifu mkubwa wa misitu kutokana na kupamba moto kwa biashara ya mbao.

JUMA HAMAD OMAR

Ni kati ya mawaziri, ambao hawatasahaulika kirahisi katika historia ya uongozi wa wizara hiyo. Katika kipindi cha uongozi wake ndipo ilipotokea kashfa ya Loliondo. Kutokana na hatua ya wizara yake kuuza Pori la Loliondo kwa mwana wa Mfalme wa Falme za Kiarabu. Kashfa hiyo ni kati ya matukio makubwa yaliyotikisa nchi kwani ilisababisha kuundwa kwa Kamati ya Bunge iliyoongozwa na Mateo Qaresi na chanzo cha kuondolewa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wakati huo, Muhidin Ndolanga. Omar aliondoka katika wizara hiyo mwaka 1995 baada ya Rais Mkapa kuingia madarakani.

JUMA NGASONGWA

Aliongoza wizara hiyo kuanzia mwaka 1995 hadi 1997. Alilazimika kujiuzulu baada ya kuibuka kwa kashfa ya biashara ya minofu ya samaki kuuzwa nje ya nchi bila kulipa kodi. Kamati iliyoundwa chini ya Mbunge wa zamani wa Ilala, Iddi Simba ilifichua madudu katika biashara hiyo.

ZAKHIA MEGHJI

Ndiye waziri aliyedumu kwa muda mrefu zaidi kwenye wizara hiyo kuanzia 1997 hadi 2005. Meghji anasifiwa kutokana na kutangaza utalii wa Tanzania kwa kiasi kikubwa. Hakukumbwa na kashfa yeyote pengine doa pekee lilikuwa ni kuuzwa kwa Hoteli ya Kilimanjaro.

ANTHONY DIALLO

Aliteuliwa Rais Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005. Alidumu kwa kipindi cha miaka miwili baada ya kutokea mtikisiko mkubwa juu ya uuzwaji wa vitalu vya uwindaji. Aliingia katika mvutano mkali na watendaji wa wizara hiyo. Alishindwa katika vita hiyo na kujikuta akiondolewa. Ingawa aliondolewa katika kipindi ambacho Rais Kikwete alikuwa anataka viongozi kutenganisha masuala ya biashara na uongozi.

PROF. JUMANNE MAGHEMBE

Ni waziri ambaye alikaa muda mfupi zaidi kwenye wizara hiyo. Alikaa kuanzia mwaka 2007 hadi 2008. Katika kipindi chake, matatizo mbalimbali yalipamba moto na hasa juu ya uuzwaji wa vitalu na pia

uvunaji wa misitu.

SHAMSA MWANGUNGA

Aliongoza wizara hiyo kuanzia mwaka 2008 hadi 2010. Katika kipindi cha uongozi wake alitikiswa na kashfa ya uuzwaji wa vitalu. Alituhumiwa kuongeza muda wa umilikaji wa vitalu kinyume cha sheria. Aliwaongezea wamiliki hao muda wa miaka mitatu kinyume cha Azimio la Bunge la kuzuia kuongezwa kwa muda wa umiliki wa vitalu ili utaratibu mpya uandaliwe.

EZEKIEL MAIGE

Alipandishwa kuwa Waziri kamili wa wizara hiyo aliyokuwa Naibu chini ya Mwangunga. Aliongoza kuanzia mwaka 2010 hadi 2012. Alikuwa na kibarua cha kupambana na uuzaji wa vitalu. Hata hivyo, alijikuta akiondolewa katika wadhifa huo kufuatia maagizo ya Bunge baada ya kuibuka kwa kashfa ya uuzaji wa wanyama hai.

BALOZI KHAMIS KAGASHEKI

Aliteuliwa kushika wadhifa huo mwaka 2012. Kagasheki alipata msukosuko wa kwanza wa kisiasa baada ya kutangaza eneo hilo la kilomita 1,500 la Loliondo kuwa ni pori tengefu na wananchi kuachiwa kilomita 2,500.

Agizo lake lilitenguliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Hata hivyo, amejikuta akiondolewa baada ya mateso yaliyowapata wananchi wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili iliyokuwa na lengo la kupambana na biashara haramu ya pembe za ndovu. Hatua hiyo ilifuatia uchunguzi uliofanywa na Kamati ndogo ya Bunge.

LAZARO NYALANDU

Alichukua nafasi ya Kagasheki na kumaliza muhula wa pili wa Serikali ya awamu ya nne akiwa waziri wa wizara hiyo, hata hivyo hakupata nafasi ya kurejea Barazani ndani ya Serikali ya awamu ya Tano.

PROF. MAGHEMBE

Alirejea tena kwenye wizara hiyo ndani ya Serikali ya awamu ya Tano, hata hivyo amefanikiwa kukalia kiti kwa miaka miwili tu.

Dk. Kigwangala yeye ndiye waziri wa wizara hiyo kwa sasa.

DK.TIZEBA ASHANGILIA…

Kwa upande mwingine Waziri wa Kilimo Dk. Charles Tizeba amefurahishwa na mabadiliko yaliyofanywa na Rais Magufuli ikiwa ni pamoja na kuigawa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Dk. Tizeba alisema hatua ya kuigawa wizara hiyo imempunguzia mzigo na ni sawa na kumkata mbawa tatu alizokuwa nazo na kubakiwa na moja.

Alitoa kauli hiyo juzi wakati akifunga mkutano wa kimataifa wa wadau wa sekta ndogo ya mazao ya mbogamboga, matunda na viungo uliofanyika kwa siku mbili jijini Arusha.

Hata hivyo, Waziri huyo alimshukuru Rais Magufuli kwa kuipunguza Wizara hiyo kwani kutokana na unyeti wake ilihitaji kugawanywa ili sekta zote zinazohusika katika wizara hizo zipate msukumo wa kutosha.

“Wakati naenda Dar es Salaam nilikuwa na mbawa tatu, kilimo, mifugo na uvuvi. Sasa nimerudi nikiwa nimekatwa mawili na kubakiwa na moja, namshukuru sana Rais kwa kuliona hili la ukubwa wa Wizara na kuigawa kuwa mbili.

“Mabadiliko haya sasa yananifanya kuwa mkulima halisi tena namba moja, inawezekana nilikuwa siwatendei haki wakulima sasa niko nao kwa sababu mdau namba moja wa sekta ya kilimo ni mkulima na mdau namba mbili ni serikali” alisema Dk Tizeba.

Dk. Charles Tizeba

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.