Kibiti ni uchumi siyo siasa kinzani kimaendeleo

Rai - - MBELE - NA SHERMARX NGAHEMERA

USEMI kuwa mchezea mwiba huota tende ndio hali halisi ya utata wa tatizo la Kibiti na wilaya zote za Mkuranga na Rufiji na tukifanya ajizi mambo yanaweza kuwa kombo zaidi.

Ninachofanya hapa ni kufikiri kwa sauti kubwa kuwa mtu mwenye njaa mara nyingi huwa ana hasira sana na iliyopitiliza kwani akizinduka hujisikia anaonewa na kila mtu na bila sababu. Ndio mchecheto ulioko Rufiji yote hadi Kilwa kwa maelezo ya Wanarufiji walioko Dar es Salaam ambao utawapata Mbagala, Tandika na Yombo Dovya.

Historia ya nchi yetu haijaandikwa kikamilifu na tumependa sana kutumia ile kauli funika kombe mwanaharamu apite tukisahau kuwa kwa kufanya hivyo tunakalia kuti kavu na upepo ukizidi tutaanguka nalo.

Chombo kimerudi ngamani na hakuna wa kutoa simile kwani jini subiani limetoka kwenye chupa kulirudisha ni kazi kubwa inayotaka chano na uvumilivu mkubwa kwani twapigana na kivuli chetu wenyewe.

Mganga au fundi anasema tujichunguze na kujisahihisha kwani adui ya mtu ni mtu nasi Wapogoro twalonga ‘Mlungu Chibidu’ yaani ogopa watu kwanza Mungu yuko mbali’.

Watu wanadai Tanzania haikupigana vita kupata uhuru wake na hivyo kuona Vita ya Majimaji, Vita ya Mtemi Bushiri na ile ya Mtemi Mkwawa kuwa ni vurugu tu na sijui wafe watu wangapi ionekane kuwa ni vita ya ukombozi. Watawala wa kikoloni hawakutaka kupigana kwani walikwisha onja ukali wake katika mapambano ya Majimaji na kwenye makabila mengine.

Uhuru wa Tanzania ulipiganwa Pwani au Jimbo la Mashariki kukiwa na mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Tanga na Pwani yenyewe ikiwa na maana ya Kisarawe, Bagamoyo, Kibaha, Kilwa, Mafia, Rufiji, Ulanga na Lindi.

Lakini cha maana zaidi ni kuwa nini kilitokea baada ya ‘rabsha’ hizo ndio kinasikitisha zaidi kwani wajanja waligeuza vibao na kuvutia kwao maendeleo na kusahau wapiganaji wao halali.

Ninapata tabu kidogo na kupata ukakasi mwingi kuzungumzia siasa uchumi za nchi hii kwani ni rahisi sana kuitwa mchochezi na kutoeleweka kwani zimekaa tenge kwa kupendelea upande wa Kaskazini mwa nchi yetu na kutelekeza eneo la Kusini mwa nchi. Ni pale tu aliposhika madaraka ya urais kwenye awamu ya tatu ndio Kusini kukakumbukwa kidogo. Mipango ya gesi ilipopamba moto ikaongeza umuhimu wa eneo hilo kwa uchumi wa nchi.

Haya ni maono tu kwani sote tuko sawa na hakuna wa pande hizo wa kulalamika kwani kama watu tumeingiliana sana bila ubaguzi wowote. Hayo si mageni ni wazi kabisa hata Mwalimu Nyerere aliyajua alipokuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kusini (South-South Commission) alipouona mgawanyo wa Kaskazini na Kusini na ule wa Mashariki na Magharibi ambao uko dunia nzima.

Kwani Vita ya Majimaji ilianza na ilipiganwa sana Rufiji, Kisarawe na Kilwa (Mkoa wa Pwani), Lukuledi (Nachingea) na Masasi (mkoani Lindi na Mtwara), Mahenge (Mkoa wa Morogoro), Njombe na Iringa (Mkoa wa Iringa, Mbeya na Songea (Mkoa wa Ruvuma) ambapo majenerali wa vita 8 wa Kingoni walinyongwa hadharani.

Mangi Sina wa Kibosho naye alinyongwa akipinga kutawaliwa na wakoloni kule Uchagani, Mkoa wa Kilimanjaro na vivyo kwa Mwinyi Bushiri wa Pangani.

Ni vema kukumbuka kuwa Julius Nyerere ambaye ni Baba wa Taifa alikuwa Mbunge wa Kwanza wa Jimbo la Pwani kwa maana ya Jimbo Mashariki (Eastern Province) mwaka 1958 katika Baraza la Kutunga Sheria (LEGICO). Tokea hapo moto wa kudai Uhuru ulipamba kila upande chini ya Nyerere na watu wa Pwani wakiwa vinara wa moto huo. Ulipopatikana Uhuru walisahauliwa vibaya na nafasi yao kuchukuliwa na wasomi waliotoka maeneo ambayo hayakupambana.

Ni ukweli unaouma kuona kuwa wale wanaochelewa kuingia kwenye mapambano mara nyingi ndio wanaofaidi matokeo ya mapambano hayo.

Kwa hasira wakoloni waliamua kutelekeza maeneo hayo yaliyokuwa mahasimu kwao na utawala baada ya uhuru ilifuata mwenendo ule ule wa kikoloni na kufanya maeneo hayo kutengwa na kufikika kwa tabu.

Lakini siku hizi kwa yaliyo mengi mambo yamebadilika kwani Serikali imefanikiwa kuunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za lami.

Hali imeanza kubadilika sana baada ya ugunduzi ya vikoleza pesa yaani kuweko kwa shughuli zakuzungusha fedha kwa wingi na hivyo kutamanika na wawekezaji na hivyo kugeuza meza kwa wa juu kuwa wa chini na wa chini wakawa juu.

Kwa maneno mengine mambo yamegeuka sana kwani wa mbele amerudi nyuma na wa nyuma sasa amekuwa mbele katika mstari ule wa maendeleo. Kijeshi tunasema ‘about turn’ yaani nyuma geuka! Ndio hali yetu sasa.

Kimitazamo ya kiuchumi Pwani, Mtwara na Lindi kuna uhai wa kiuchumi mkubwa kwa siku za usoni kuliko Kilimanjaro kutokana na kupatikana na kuchimbwa kwa gesi asilia ambayo imeshaanza kusababisha kuchanua kwa uchumi wa Tanzania. Hapo baadaye uchumi huo utaning’inizwa kwenye madini hayo na kwa mbali madini ya Kinywe ambayo yataanza kuchimbwa mwakani na yako kwa wingi, Lindi, Mtwara na Ulanga.

Warufiji na Mganga au Jenerali Kinjekitile kwao ni pale Muhoro Wajerumani walishindwa kumnyonga Kinjekitile kwani mara tatu aliponing’inizwa kamba ilikatika na hivyo kuachiwa huru kwani hukumu ilikuwa ni kunyongwa hadi kifo na si kuuawa na kwa vile majaribio matatu yalifanyika bila kufanikiwa ni kuwa hakustahili kufanyiwa hayo. Ni ukweli ambao Wazungu hawakutaka kuuzungumza kwani ulikua Kioja, nacho huwa hakizungumzwi kwani ni uchuro!

Itaendelea wiki ijayo

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.