Ubelgiji isiyovuma kuishangaza dunia 2018?

Rai - - MBELE - HASSAN DAUDI NA MITANDAO

UBELGIJI si miongoni mwa mataifa yanayozungumziwa sana kwenye mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia za mwakani nchini Urusi. Mashabiki wengi wa soka wamekuwa wakizungumzia zaidi Brazil, Ujerumani na Hispania. Hata hivyo, wachambuzi wa soka wanakitazama kwa jicho la tatu kikosi hicho cha kocha Roberto

UBELGIJI si miongoni mwa mataifa yanayozungumziwa sana kwenye mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia za mwakani nchini Urusi. Mashabiki wengi wa soka wamekuwa wakizungumzia zaidi Brazil, Ujerumani na Hispania.

Hata hivyo, wachambuzi wa soka wanakitazama kwa jicho la tatu kikosi hicho cha kocha Roberto Martinez, wakiamini kinaweza kuishangaza dunia kwenye fainali hizo, hasa kutokana na kiwango chao katika miaka ya hivi karibuni.

Kinachowaaminisha wachambuzi hao kuwa Ubelgiji ni timu inayopaswa kuogopwa kwenye michuano hiyo ni kile ilichokifanya kwenye mechi za kufuzu,iliposhinda mechi nane kati ya tisa za hatua ya makundi na hatimaye kuwa taifa la kwanza barani Ulaya kukata tiketi ya kwenda Urusi, ukiacha Urusi waliofuzu moja kwa moja kama wenyeji.

Katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014, Ubelgiji ilifika robo fainali,hatua ambayo pia waliifikia katika michuano ya Euro mwaka jana nchini Ufaransa.

Lakini je, nini kinachoweza kuwapa jeuri Wabelgiji katika fainali za Urusi zitakazofanyika katika miji tisa?

Kwanza, wachambuzi wa masuala ya soka wanaamini kuwa timu hiyo ina safu nzuri ya ulinzi. Langoni, kocha Martinez atakuwa akimtegemea mlinda mlango aliye kwenye ubora wa juu katika kikosi cha Chelsea, Thibaut Courtois. Katika eneo la beki wa kati, Ubelgiji ina wachezaji wazoefu kama Vincent Kompany, Toby Alderweireld na Jan Vertonghen, ambao wanakipiga Ligi Kuu England. Faida kubwa kwa Ubelgiji ni kwamba Alderweireld na Vertonghen wanacheza pamoja kwenye eneo la beki wa kati katika kikosi cha Tottenham, hivyo watakuwa na maelewano mazuri.

Kwa upande wa beki wa pembeni, Ubelgiji wana Thomas Meunier na Jordan Lukaku, ambao mbali na kuzuia wamekuwa wakifanya kazi nzuri ya kupandisha mashambulizi.

Pia, Vertonghen amekuwa akitumika katika eneo la beki wa kushoto pale anapohitajika, ingawa amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.

Wachambuzi wa soka wanalitaja pia eneo la kiungo kuwa ni silaha nyingine ya Ubelgiji kuelekea fainali hizo za Kombe la Dunia. Katika eneo la kiungo wa ulinzi, kocha Martinez ana Axel Witsel anayeichezea klabu ya Tianjin Quanjian ya Ligi Kuu nchini China.

Safu hiyo pia ina Mousa Dembele wa Tottenham, Youri Tielemans wa Monaco, Radja Nainggolan anayekipiga Roma na Marouane Fellaini anayeziba pengo la Paul Pobga kwenye kikosi cha Manchester United. Mbali na hao, eneo la kiungo la Ubelgiji litakuwa na nyota anayefanya vizuri kwenye kikosi cha Manchester City, Kevin De Bruyne.

Kunapotokea janga la majeraha kati ya nyota hao, kocha Martinez atawageukia Leander Dendoncker wa Anderlecht na Steven Defour anayecheza Ligi Kuu England akiwa na klabu ya Burnley.

Wachambuzi wa soka wanaamini kikosi cha Ubelgiji pia kimekuwa na makali kwenye safu yake ya ushambuliaji, ambayo imekuwa ikiongozwa na Eden Hazard.

Faida kubwa waliyonayo Wabelgiji kwa nyota huyo wa Chelsea ni uwezo binafsi, hasa pale timu inapozidiwa. Hazard atakuwa akishirikiana na Dries Mertens wa Napoli na kinara wa mabao wa Ligi Kuu England, Romelu Lukaku.

Lakini pia, kocha Martinez ana akiba ya wapachikaji mabao,hata pale janga la majeruhi linapomkumba mmoja kati ya mastaa wake hao. Kikosi hicho kina Michy Batshuayi, Christian Benteke na Divock Origi.

Upande wa washambuliaji wa pembeni, Carrasco, Kevin Mirallas, Nacer Chadli na Charly Musonda walifanya kazi kubwa kuhakikisha Ubelgiji inakwenda Urusi na wanatarajiwa kuendeleza moto huo watakapofika nchini humo hapo mwakani kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia.

Kwa Afrika, Nigeria lilikuwa taifa la kwanza kufuzu michuano hiyo baada ya ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya Zambia, mchezo uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Ikiwa ni takribani miaka 27 toka ishiriki fainali hizo, Misri nayo ilikata tiketi ya kwenda Urusi hapo mwakani baada ya ushindi wake wa mabao 2-1 dhidi ya Congo mwishoni mwa wiki.

Katika mtanange huo uliochezwa mjini Alexandria, staa wa Liverpool, Mohamed Salah, ndiye aliyepeleka furaha nchini mwake baada ya kufunga mabao hayo na kuwapeleka Misri katika fainali za kwanza tangu mwaka 1990.

Kikosi cha Ubelgiji kilichofunzu kucheza Kombe la Dunia mwakani nchini Urusi

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.