ALIONA MENGI KATIKA NCHI

Rai - - MBELE - NA MARKUS MPANGALA 0764 936655

OKTOBA 14 tunaadhimisha kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere tangu alipofariki dunia mwaka 1999. Katika uhai wake Baba wa Taifa aliacha maneno mengi yenye busara na kuwaelimisha Watanzania kupitia hotuba na vitabu mbalimbali alivyopata kuandika katika uhai wake.

Endelea kuzisoma hapa ili ujifunze zaidi……

“Lakini watu wetu hawataki au kufurahishwa au kutumbuizwa na viongozi wao, wala wananchi hawataki ahadi nyingi za uongo juu ya raha ambazo mtu fulani atawaletea; watu hawataki kuwasikiliza viongozi wao wakiwatukana watu au kikundi cha watu kama kisingizio cha shida walizonazo watu.

Viongozi wa Tanzania na hao ndio sisi sote tuliopo hapa leo, lazima tuonyeshe, kwa maneno na matendo kwamba tunatambua jambo moja kubwa, dhamana ya uongozi.(Julius Nyerere, Ujamaa uk. 157)

“Bunge lililojaa watu wanaoweza kusema ‘ndiyo ndiyo’ kufuatisha mawazo ya watu wengine halitasaidia maendeleo yetu wala demokrasia. (Julius K. Nyerere, Binadamu na Maendeleo, uk. 113-114.

“Sihubiri ujamaa, muda umepita sana kufanya hilo. Ninachotaka kusema, hata hivyo ni kwamba ubepari ni unyama zaidi hivi sasa kuliko zama zile, ambapo kuwepo ukomunisti kulifanya kidogo uwe na ubinadamu.” (Julius Nyerere, 1995)

“Ziko Serikali mbili tu duniani; mosi Serikali zinazopenda maendeleo na pili ni Serikali zinazopenda au zinazonyonya watu tu (Julius Nyerere).

“Haya ni mawazo ya ajabu kabisa. Wenzetu hawa nchi za magharibi wanadhani kusaidiwa na nchi zile zenye kufuata itikadi za ujamaa basi tunataka kujiunga kambi hiyo. Hatuwezi kuishi katika mtindo huu, kwani kusaidiwa na nchi hizo hakumaanishi tunakuwa wajamaa (Julius K. Nyerere, Crusade For Liberation).

“Usawa na heshima kwa watu wote unalenga kuzalisha jamii ya kisoshalisti, kushirikiana kupata malighafi ambayo yatafanikisha mipango yetu, hasa kila mmoja akishiriki kwa kufanya kazi bila kumnyonya yeyote (Julius K. Nyerere, Elimu ya Kujitegemea, 1967).

“Maendeleo ni watu, kwa watu na ya watu, ambapo wanatoa pia umuhimu wa ukombozi wa mtu, kwa mtu na watu. Hivyo basi maendeleo ni watu (Julius K. Nyerere, Binadamu na Maendeleo)

“Hapakuwa na sababu hata moja ya kuwafanya wadai Serikali ya Tanganyika, maana hata ukiwa na Serikali ya Tanganyika bado viongozi wetu wanaweza kukiuka sheria na Katiba ya nchi na dawa haitakuwa kuigawa nchi tena na kuongeza Serikali, bali ni kuwadhibiti viongozi wahalifu (Julius K. Nyerere, Uongozi Wetu na Hatima ya nchi yetu).

“Sehemu muhimu katika kujenga umma wenye demokrasia ni majadiliano huru vikifuatiwa na utekelezaji wa maamuzi ya pamoja; ikiwa watoto watazoea hivyo shuleni watakuwa wanajifunza wajibu wa wananchi katika umma huru .(Julius K. Nyerere, Elimu ya Kujitegemea)

“Tunasema tunataka kufanya mapinduzi. Na siku hizi neno mapinduzi linapendwa sana Afrika. Mengine si mapinduzi; mengine ni maasi tu, nayo yanaitwa mapinduzi!

Lakini nasema tunataka kufanya mapinduzi; na ni kweli tunataka kufanya mapinduzi. Lakini kwanini tunataka kufanya mapinduzi? Inafaa turudi nyuma kidogo, kutazama kwanini lazima tufanye mapinduzi katika Afrika. (Julius K. Nyerere, Jumamosi Mei 30, 1969).

“Kwanza mmeuliza, ‘kwanini majeshi ya kikoloni yalikuwa yanakatazwa siasa?’ na mimi vilevile nitawaulizeni nyinyi, ‘Majeshi ya kikoloni yapi yaliyokatazwa siasa na maana ya kutazwa siasa ni nini? Tuchukue tulivyokuwa kabla hali ya kutawaliwa.

Linakuja Taifa la kigeni linavamia taifa jingine; watalitafuta jeshi la mahali pale, walipige lile jeshi, walinyang’anye silaha; kisha waone kama wananchi wanazo silaha basi wanyang’anywe. Sasa kuna mambo mawili.

“Ama hawa walioingia kwa mfano, Waingereza, watashinda na wakishinda watabaki na jeshi lao liwatazame wale waliokwishapigwa; kwa hiyo mara huundwa jeshi la kuwasimamia wananchi wasishike silaha. Jeshi haliwezi kuwa halina siasa; jeshi maana yake ni chombo cha siasa.

“Siasa iko, ila inayogomba ni siasa ya nani. Tusidhani kuwa wakubwa wale waliokuwa wanasimamia jeshi enzi za kina Colonel Chacha, walikuwa hawasimamii siasa hapa; walikuwa nayo siasa.

Lakini sisi hatutaki jeshi la mfumo wa Kiingereza bali tunataka jeshi la kulinda ndani ya nchi yetu, ndiyo walinzi wa wananchi. (Julius K. Nyerere, Julai 27, 1968 Zanzibar)

“Waheshimiwa, ijapokuwa nawachekesha lakini narudi kulekule kunako uhuru wetu. Uhuru wa watu waliowahi kuonewa, si uhuru wa bendera, uhuru wa bendera hautoshi hata kidogo; hauwezi kuwa uhuru wa passport nao hautoshi hata kidogo.

“Lazima uhuru wetu uwe uhuru wa mioyoni, wa mtu kukubali na kuthamini utu wake. Mara nyingi watu walioonewa hawafanyi hivyo au tuseme hawaanzi hivyo. (Julius K. Nyerere, Novemba 1970, Bagamoyo).

“Lazima tu ufanye kazi japo ya kujipatia riziki tu, chakula cha matata-matata hivihivi na kaguo ka matata-matata hivihivi na banda japo ovyo-ovyo hivi; lakini ni lazima wafanye kazi japo kwa kuishi tu ni lazima wafanye kazi. (Julius K. Nyerere, Saba saba ya 1970).

“Mheshimiwa mbunge anaposema kuwa wananchi wa sehemu yake wana shida ya maji, je Serikali ina mpango gani wa kuondoa shida hiyo? Jibu analopenda ni kwamba Serikali inao mpango wa kuwapa maji wananchi wa sehemu hiyo-KWA FEDHA.

“Mheshimiwa mbunge anaposema kuwa wananchi wa sehemu yake haina barabara au shule au hospitali au vyote, je, Serikali ina mpango gani?

Naye jibu ambalo angependa kupewa ni kuwa Serikali inao mpango safi kabisa wa kutengeneza barabara au kujenga shule au hospitali kwa wananchi wa sehemu ya mbunge mheshimiwa huyu–KWA FEDHA. Hatuwezi kuendelea kwa mtindo huu wa kudai fedha! Fedha! Fedha! Fedha!” (Julius K. Nyerere, Ujamaa, uk.20).

“Chama Cha Mapinduzi kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa watu wake, mazoea ya watu na ubovu wa vyama vya upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania pamoja na kansa ya uongozi wake.

“Au watu wanaweza wakachoka, wakasema ‘potelea mbali’ wakachagua chama chochote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya lakini uhai wa nchi yetu unataka yasemwe. (Julius K. Nyerere, Uongozi Wetu na hatima ya Nchi Yetu, uk.61.).

“Askari wa Tanzania lazima awe ‘askari mzalendo’; si uzalendo tu, bali aipende nchi yake na mipaka yake. Lakini askari huyo lazima azidi kidogo uzalendo. Kama alivyosema Major General: “Lazima askari wetu aelewe siasa ya nchi yetu”.

“Lazima. Maana, kama alivyosema Major-General, haiwezekani kulinda mipaka, mabarabara na majumba tu; kulinda nchi lazima tabia yake ilindwe. Na tabia ya nchi yetu nitaitamka. Ni usawa wa wananchi wote wa Tanzania; hiyo ndiyo tabia yetu.” (Julius K. Nyerere, Septemba mosi, 1969 katika sherehe ya maonyesho ya jeshi).

“Sasa wanachama wa TANU mtakavyonisema kama ningalikuwa bepari, ‘Mwalimu naye ubepari wake umezidi, ‘Wewe bepari; wewe mwanachama wa TANU bepari. Tena ubepari wake anangojea siku ya uchaguzi. Ikifika siku ya uchaguzi anasema ‘sasa nataka uchaguzi’.

“Tunamwambia, ‘lakini yahe, wewe si mnyonyaji? Anajibu ‘Mimi mnyonyaji kwanini; mpaka sasa mimi si kiongozi. Lakini mkishanichagua nikawa kiongozi, basi nitaacha kunyonya’. Sasa imani gani ya mwanachama wa TANU? (Julius K. Nyerere, Sabasaba 1970).

“Tulipoambiwa tuwe na katiba kama ya Waingereza, tulisema ‘Hapana! Tutaunda Katiba yetu wenyewe. Tukiona kuna mambo ya Waingereza yanatufaa, tutayachukua.

“Lakini kwamba tujitahidi kuwapendeza Waingereza na Waingereza watusifu, waseme Katiba hii ndiyo shabaha yetu, tulikataa. Na bado msije mkadhani neno hilo linaeleweka kweli; bado zipo jitihada nyingi za Waafrika za kujipendekeza.” (Julius K. Nyerere, Novemba 24, 1970 katika Hotuba ya kufungua semina ya maofisa wa jeshi, Bagamoyo).

“Lakini tunakwenda kidogo kidogo; hata wabovu kabisa wanaanza kuelewa-elewa. Juzi nilikuwa nasikiliza wananchi Wabunge wanazungumza. Waheshimiwa wanasema lazima tulinde maendeleo.

“Nikaona kuwa ikiwa waheshimiwa hawa, wanasiasa, wanasema lazima tulinde maendeleo ni dalili nzuri, ndio tunakwenda hivyo. Tunaanza kuelewa, lakini nasema bado tuko mbali! Hatua ya kwanza ya mawazo, tunaelewa; lakini ya pili kazi ya kujifunza, wakubwa mnaelewa wenyewe. (Julius K. Nyerere, Hotuba iliyotolewa kwa wanajeshi wapya Zanzibar, Jumamosi Julai 27, 1968).

“Mfumo wa elimu ni tofauti kwa kila aina ya jamii duniani. Imekuwa tofauti kwa sababu kuna taasisi tofauti kila moja ina shabaha zake. Ziko tofauti kwa sababu jamii inatoa elimu iliyo tofauti na kwa sababu elimu iwe ya kisasa ama zama zote zina umuhimu.

“Umuhimu huo unasambaa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine kutokana na busara za jamii na ufahamu wao; hivyo inamwandaa kijana kuwa kiongozi wa kesho wa jamii hiyo kwa kushiriki madhumuni ya jamii yake. (Julius K. Nyerere, Elimu ya Kujitegemea).

“Kama Kuwait na Saudi Arabia wangelikuwa wanauza ndizi au machungwa, Marekani isingekwenda kule. Walikwenda Kuwait kwa sababu kuna mafuta ambayo yanaipatia utajiri nchi hiyo.”(Julius K. Nyerere, Agosti 1990, The Independent, London, Uingereza) “Afrika ni lazima ikatae kudharauliwa, kunyonywa na kusukumwa sukumwa huku na huko. Na vilevile isiwe inadharau wengine, isiwe inanyonya na kusukuma sukuma wengine. (Julius K. Nyerere, Freedom and Development).

Ama hawa walioingia kwa mfano, Waingereza, watashinda na wakishinda watabaki na jeshi lao liwatazame wale waliokwishapigwa; kwa hiyo mara huundwa jeshi la kuwasimamia wananchi wasishike silaha. Jeshi haliwezi kuwa halina siasa; jeshi maana yake ni chombo cha siasa

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.