JPM kuna watendaji serikalini wanakuhujumu

Rai - - WIK KUMBUKUMBU - NA SIDI MGUMIA, MBARALI

NI jambo la ajabu na linalosikitisha kuona kasi na dhamira ya dhati ya Rais Dk. John Magufuli ya kuwatumikia Watanzania ikikwamishwa na baadhi ya watendaji ndani ya Serikali yake.

Huu ndio ukweli, wapo baadhi ya watendaji kwa kujua ama kwa kutokujua wamekuwa wakizihujumu jitihada za Rais.

Uhujumu huu kama ulivyokuwa ukifanyika kwenye madini ndivyo unavyoonekana sasa kufanyika kwenye ardhi.

Wapo watendaji wanaamua kutumia ardhi za vijiji kuwapa wawekezaji kinyume cha utaratibu au kufuata utaratibu, huku wakihalalisha kwa njia zisizostahiki.

Ukweli wa jambo hili unadhihirika wazi kwenye mgogoro wa shamba la mpunga la Kapunga, lililopo ndani ya Kijiji cha Kapunga, Kata ya Itamboleo, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya.

Lakini pia, Wilaya ya Mbarali ni miongoni mwa wilaya zilizo katika mradi wa Ardhi Yetu, Agenda Yetu unaotekelezwa na wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kwa kushirikaina na Shirika la Care International, unaowawezesha wananchi kufahamu na kudai haki zao katika masuala ya ardhi.

Hali ilivyo katika kijiji hicho ni kwamba mgogoro wa shamba la Kapunga bado upo na haujaisha, wananchi wanaendelea kudai ardhi yao wakisema wamedanganywa juu ya utekelezaji wa agizo la Serikali kurudisha hekta 1,870 kwa wananchi kutoka kwenye shamba lenye ukubwa wa hekta 7,370 alilopewa mwekezaji kimakosa.

Shamba la Kapunga lilibinafsishwa na kuuzwa kwa Kampuni ya Export Trading kwa lengo la kulifufua shamba hilo ambalo awali lilimilikiwa na Serikali.

Kabla ya kuuzwa shamba hilo lilitumiwa na wakulima wadogo waliokuwa wakilima kwa kukodi, ambapo walifanikiwa kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani sita za mpunga kwa hekta.

Pamoja na mafanikio hayo ya wakulima wadogo na ombi lao la kulinunua shamba hilo hata kwa shilingi bilioni kumi, walipuuzwa na hatimaye kuliuza kwa kampuni hiyo kwa gharama ya shilingi bilioni 2.5.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Kapunga, Brighton Mwinuka, ni kuwa Serikali ilishafanya kazi yake na wao wamekwishakabidhiwa ramani na baada ya waatalamu kufanya vipimo vyao, ikabainika kuwa kuna wanakijiji wanatakiwa kuhama kutoka katika eneo la shamba la mwekezaji kuhamia kwenye eneo walilokabidhiwa.

“Baada ya eneo kupimwa iligundulika kuwa kuna kaya 13 katika Kitongoji cha Mkanada ambazo zimo ndani ya eneo la mwekezaji, hivyo wanapaswa waondoke kupisha eneo la mwekezaji. Kimsingi kuna tofauti ya namna sisi wanakijiji tulivyokuwa tunaelewa mipaka ya shamba na namna wanavyotuambia wataalamu baada ya vipimo vyao,” alisema Mwinuka.

Kwa nyakati tofauti wanakijiji wamelaumu kuwa kazi ya upimaji wa hekta hizo umefanyika bila ya wananchi kushirikishwa na hivyo kutengeneza mgogoro zaidi ya mgogoro uliokuwepo hapo awali, kwani wanaamini kuwa mwekezaji kapewa eneo kinyume na maagizo yalitolewa hapo awali.

Kwa upande mwingine, Mwinuka alisema kuwa hatua ya Rais John Magufuli kuwapatia eneo hilo kutakifanya kijiji kiwe na mipango ya maendeleo na kwamba, wanamshukuru Rais kwa kuingilia kati mgogoro wao na kwa kuagiza kurudishiwa hekta 1870 kutoka kwa mwekezaji Export Trading.

Naye Faraja Kyando, Katibu wa Jukwaa la Wakulima katika Kijiji cha Kapunga, anasisitiza kuwa bado suala hilo la kurejesha ardhi kwa wananchi halijatekelezwa kisawasawa kama ambavyo maandishi yanasema.

“Mpaka hivi sasa bado kuna mgogoro kati ya mwekezaji na wanakijiji kutokana na kwamba vitongoji viwili vya Mkanada na Lwanjili bado viko mikononi mwa mwekezaji, ambapo anasema kwamba ni eneo lake licha ya kwamba ramani haisemi hivyo,” alisema Kyando.

Aliongeza kuwa, “Si kweli kuwa vitongoji hivyo ni mali ya mwekezaji kwakua shamba lina ramani zake. Tunachosikitika ni kwamba, tunashindwa kuelewa kinachoendelea kwani nia ya Rais ni njema lakini tunapata kigugumizi kwa hawa watendaji wa chini pindi inapofikia hatua ya kutekeleza maagizo ya viongozi wa juu kwa maana wanafanya mambo kinyume na maagizo ya Rais pamoja na Waziri wa Ardhi.”

“Upo udanganyifu juu ya uwekaji wa mipaka, kwani eneo alilopewa mwekezaji si eneo alilostahili kupewa na hii maana yake ni kuwa maeneo yamemegwa na maeneo tuliyokuwa tunayatumia yamepewa mwekezaji na shida ndio iko hapo,” alisema Kyando.

“Kwetu sisi baada ya kubaini udanganyifu huo tulipeleka malalamiko yetu kwenye ngazi mbalimbali kama vile mkoani, wilayani lakini bado tukaambiwa kuwa sisi haturidhiki, tunasababisha migogoro, kwahiyo kukawa na hali kama ya vitisho iliyosababisha tushindwe kusema lolote, tukanyamaza kimya.”

Akizungumzia changamoto hizo, Kyando ametaja kuwa wapo baadhi ya watu ambao wameshabomolewa makazi yao na mwekezaji katika Kitongoji cha Mkanada, pia kuondolewa kwa nguvu katika maeneo hayo pamoja na kushindwa kupita katika eneo hilo ili kufanya shughuli za kilimo katika eneo hilo ambalo limezungukwa na mashamba ya wenyeji.

Akizungumzia kilichojiri baada ya agizo la urejeshwaji wa ardhi, Jackson Mbilinyi ambaye ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kapunga, anasema Serikali ya kijiji ilifanya mkutano na wananchi Februari mwaka huu ili kufahamu ni nini kifanyike katika ardhi hiyo iliagizwa urudishwe.

“Katika mkutano huo tuliamua kuwa viwanja 250 vyenye ukubwa wa 35 kwa 35 vitolewe kwa wanakijiji kwa ajili ya makazi katika vitongoji vya Ofisini na Mapogoro lakini pia viwanja hivi kugawiwa kwa shilingi 100,000,” alisema Mbilinyi

Aliongezza kuwa walitenga pia viwanja 60 vyenye ukubwa wa ekari moja kwa ajili ya uwekezaji ambapo kila kimoja kitapatikana kwa gharama ya shilingi milioni mbili. Tulifanya tena marekebisho na kushusha na gharama sasa ni shilingi milioni moja.

Naye Feint Mwashikumbulu anasema wao kama wawakilishi wa wananchi wamekataa na wamesema wao wametoa heka 5500 na ndizo zitolewe kwa mwekezaji lakini wanaamini mwekezaji kapewa eneo kubwa zaidi ya hapo.

“Ushauri wetu sisi ni kuwa wataalamu waje na tupime kupitia mfumo wa GPS ili tuweze kujiridhisha kuwa hekari hizo ni 5500 kweli na si vinginevyo na hapo hapatakuwa na mgogoro tena na hii ni kuondoa ubishi uliopo sasa,” alisema Mwashikumbulu

Anaongeza kuwa wazo lao halijakubaliwa mpaka sasa na wanashangaa ni kwa nini wataalmu hawataki kutumia mfumo wa GPS kuondoa utata na wao wanaogopa kupita eneo hilo kwakuwa bado liko chini ya umiliki wa mwekezaji.

Lakini pia alizungumzia namna ambavyo mwekezaji huyo amekuwa akiwakwamisha katika matumizi ya maji ambayo yanapatikana katika eneo shamba hilo la mpunga, amekuwa akitoa maji kidogo na kwa namna anavyopendezwa yeye jambo ambalo si jema kwa ustawi wa zao la mpunga.

“Na kwa hili la maji tumeshalalamika kwa wahusika lakini bado hakuna kinachofanyika mpaka sasa, mwekezaji anatunyanyasa na maji, hatuyapati ipasavyo,” alisisitiza Mwashikumbulu

Akitolea ufafanuzi swala hilo, Abisai Chilunda ambaye ni Msimamizi wa Ofisi ndogo ya Bonde la Mto Rufiji iliyopo Mbarali amesema kuwa vibali vyote ya maji vilikuwa vinamilikiwa na serikali kabla ya ubinafsishwaji na sasa vibali vinamilikiwa na mwekezaji na kwakuwa sasa shamba linarudishwa kwa wanakijiji ni vyema na wao wakafuata taratibu za kuomba vibali halali vya umiliki wa maji hayo katika shamba hilo ili waweze kuyatumia kwa namna wanavyohitaji na sio kumtegemea mwekezaji kufanya anavyotaka kwakuwa yeye ndio mmiliki wa maji hayo.

Pamoja na mambo mengine, Mjumbe wa Jukwaa la Wakulima, Kapunga, Sekelaga Sandube aliishukuru Serikali hususan Rais Magufuli na Waziri Lukuvi kwa kumaliza mgogoro ambao uliwashinda wengi kwa muda mrefu sana.

Sandube anasema kuwa kwa upande wao hawana mgogoro na mwekezaji kwakuwa amekiri kuwa aliuziwa eneo la hekta 7370 wakati huo wauzaji wanasema wamemuuzia hekta 5500. Mwekezaji alisharidhia kupitia maamuzi yaliyotolewa kuwa aliuziwa eneo kimakosa na eneo lilozidi lirudishwe.

“Pamoja na mambo mengine wasiwasi mwingine unaibuka pale ambapo muda uliotumika kutekeleza agizo hilo, badala ya siku 30 walizopewa wataalamu kufanya upimaji na kutoa ramani mpya, wao walitumia siku sio zaidi ya 12,” alisisitiza Sandube

Hata hivyo, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alitoa agizo hilo Januari 04, mwaka 2016 ambapo alitoa siku 30 kukamilisha zoezi hilo. Hata hivyo, Januari 16, mwaka 2016, ramani hiyo ilikuwa tayari imetayarishwa na kusainiwa, hatua iliyosababisha wananchi hao kuamini kuwa ramani ilikuwepo tayari hivyo walihadaiwa.

Sandube anaendelea kusisistiza kuwa katika mgogoro mzima, tatizo liko kwa wataalamu na sio serikali wala mwekezaji kwani wataalamu ndio wamempelekea rais vipimo sivyo kwa maana yakufanya mambo kinyume na walivyoagizwa.

“Tunaomba rais aingilie kati hili swala linalofanywa na wataalamu ili tufikie muafaka maana kwa sasa sisi tunafika mahala tunakosa imani na wataalamu,” alisema Sandube

Akiongelea kinachojiri sasa, Kaimu Ofisa Ardhi na Maliasili wa Mbarali, Geofrey Mwaijobele, anasema wanaandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa kijiji chote cha Kapunga ambapo eneo lililorudishwa pia litajumuishwa na baada ya mpango huo kukamilika ndipo watakapoanza kuwagawia wanakijiji maeneo na kuwamilikisha na taratibu za mpango huo zinajulikana hivyo wanakijiji wanapaswa kushiriki kikamilifu.

“Matumizi hayo ni pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya huduma za kijamii kama vile shule, zahanati na vinginevyo, hivyo kijiji kitaanda mpango wao pia na kuchangia fedha kidogo kwakuwa serikali ina bajeti kidogo, hivyo watafanya kwa pamoja ili kuhakikisha wanafanikiwa kuleta maendeleo endelevu kwenye kijiji cha Kapunga,” alisema Mwaijobele

Amesema baada ya mpango huo kukamilika watatoa pia hati miliki kwa mwanakijiji mmoja mmoja ambazo zitawasaidia katika taasisi za kifedha ili watumie kama dhamana zao an itawasaida pia kuapata mikopo na mahitaji mengine. Mgogoro wa mipaka ya Shamba la Kapunga umedumu kwa miaka 11 sasa, baada ya kuibuka rasmi mwaka 2006 lilipouzwa.

Mwaka 1995, wanakijiji walitoa hekta 5,500 za ardhi kwa Kampuni ya Taifa ya Kilimo (Nafco), huku eneo la hekta 1,870 likiwa la wakulima wa kawaida.

Hata hivyo katika mazingira ya kutatanisha, Serikali ilichukua hati moja iliyojumuisha hekta 5,500 na nyingine 1,870 bila kuwajulisha wananchi, hivyo mwekezaji aliponunua eneo la Nafco alikabidhiwa hati ya eneo lote.

Pamoja na Serikali ya awamu ya nne kubaini Nafco ilisajili na kupata hati moja kwa eneo lote likiwamo la kijiji, lakini kwa miaka yote imeshindwa kutoa uamuzi hadi pale Serikali ya awamu ya Tano ilipoingia madarakani na kuagiza eneo la kijiji lirudishwe kwa wahusika, hata hivyo baadhi ya watendaji wamefanya udanganyifu wenye kuashiria kumuhujumu Rais Dk. John Magufuli.

Waandishi wa habari wakizungumza na viongozi wa Kijiji cha Kapunga

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.