Manufaa yaanza kuonekana Chongoleani

Rai - - MAKALA - NA SUSAN UHINGA, TANGA

NI umbali wa takribani kilomita 25 kutoka Tanga Mjini hadi Kata ya Chongoleani ambako huko ndiko kutakuwa na matanki ya kuhifadhia mafuta ghafi yatakayotoka Hoima nchini Uganda.

Tayari eneo la ukubwa wa ekari 500, limetengwa kwa ajili ya shughuli yote ya kupokea na kusafirisha mafuta kupitia bandari itakayotumiwa na meli za kusafirisha mafuta hayo kwenda ughaibuni.

Eneo kubwa la Chongoleani limezungukwa na vichana na minazi, huku ardhi yake ikitawaliwa na kichanga zaidi.

Kabla ya eneo hilo kuwa maarufu leo kutokana na mradi huo mkubwa na wenye gharama ya hali ya juu, Chongoleani haikuwa maarufu, haikuwa midomoni mwa watu nje na ndani ya nchi, shughuli kuu za wakazi wa eneo hilo zilikuwa ni uuzaji wa nazi, uvuvi na kilimo cha kukidhi mahitaji ya nyumbani.

Makazi ya wenyeji wengi wa Kata hiyo yalikuwa ni vibanda vidogo vya udongo vilivyoezekwa kwa makuti.

Halikuwa jambo jepesi kuona uwapo wa nyumba kubwa za tofari zilizoezekwa kwa mabati ya kisasa.

Jambo la kufurahisha kama ulipata nafasi ya kufika Chongoleani kabla ya ujio wa mradi na leo hii ukarejea tena kwenye eneo lile lile unaweza kupigwa na butwaa.

Mabadiliko makubwa ya kimaisha yameanza kuonekana kwa mtu mmoja mmoja ndani ya Kata hiyo iliyopo pembezoni mwa mji wa Tanga.

Ndani ya kipindi kifupi cha ujio wa mradi huo tayari wakazi wa Kata hiyo wameanza kujenga nyumba za kisasa na wengine wameshapata ajira za moja kwa moja na zile zisizo za moja kwa moja za mradi huo.

Nilifunga safari ya kuelekea Chongoleani kujionea maisha ya wakazi wa kata hiyo ambayo ndio kitovu cha mradi huo mkubwa,lengo lilikuwa kujionea maendeleo ya mradi na mwenendo wa maisha ya wananchi hao mara baada ya kulipwa fidia ya kuyahama makazi yao ya wali ili kupisha mradi huo.

Taswira ya eneo hilo imeonekana kubadilika kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na awali, ambapo eneo kubwa lilikua ni mapori pamoja na nyumba za udongo za wenyeji ambapo kwa sasa hali ni tofauti.

Tofauti ambayo inaonekana kwa sasa ni uwepo wa barabara zinazofikika eneo hilo kwa urahisi, lakini pia hata wakazi wake kuonekana wakiwa katika shughuli za ujenzi wa nyumba za kisasa hali inayoashiria uwepo wa mabadiliko ya kiuchumi kwa wakzi hao.

Spen Mwalimu yeye ni mkazi wa chongoleani anaeleza namna ambavyo uwepo wa mradi huo katika eneo la kata yao unavyowanufaisha.

Anasema maisha yamebadilika kwa wakazi hao kutokana na wengi wao kulipwa fidia nay a kupisha eneo la mradi japo fedha hizo zimeweza kuwasaidia kujenga nyumba za kisasa tofauti na awali walikuwa wakiishi katika nyumba za udongo.

“Mwandishi kama unavyoona kwa sasa Chongoleani sio ile unayoijua wewe, hata ukitazama nyumba unaona bati zinang’ara tofauti na hapo awali tulikuwa tukilala mbavu za mbwa kwa hili hakika tunaishukuru serikali ya magufuli,” alibainisha Mzee Mwalimu

Anasema kwamba mbali ya kufanikiwa kujenga nyumba bora na za kisasa bado wanajivunia kupata kazi katika eneo la mradi na kwamba malipo wanayolipwa yanawasaidia kuendesha familia zao.

Uwepo wa mradi katika eneo hilo haukuwaacha nyuma vijana ambao nao wanaelezea namna walivyoachana na kukaa maskani , ambapo kwa sasa wengine wanajishughulisha na shughuli za kusafirisha abiria kwa kutumia usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda.

Mohamedi Mwinchamvi kijana anaejishughulisha na kusafirisha abiria maarufu bodaboda anasema yeye alikuwa na shamba la wazazi wake ambapo mara baada ya kulipwa fidia amejenga nyumba ya kisasa na kununua pikipiki ambayo kwa sasa inamuingizia kipato.

Wapo vijana ambao wengine wameajiriwa katika mradi wanafanya shughuli mbalimbali na wanatoka kijijini kwetu hapa, hakika hili tunajivunia na ni neema.

Mwinchamvi anasema hapo awali vijana wengi hawakuwa na shughuli za kufanya ambapo waliishia kukaa vijiweni maarufu maskani jambo amablo kwa sasa anasema huwezi kuwakuta vijana wanakaa vijiweni kwa maana wamepata shughuli za kufanya.

Wanawake nao wanajishughulisha na uuzaji wa chakula katika eneo la mradi ,hali ambayo imefanya Chongoleani kuchangamka na kuonekana mpya kwakuwa sasa inajengeka upya na watu wanajishulisha kila mmoja katika eneo lake.

Kwa sasa ukifika Chongolea utajionea wakazi wake wakiwa katika harakati mbalimbali za kujiingizia kipato wengine wakiboresha makazi yao huku wageni nao wakiingia katika eneo hilo kutazama fursa zilizopo.

Wakazi wa Tanga wamepewa kipaumbele katika mradi huo mkubwa ambao umeshaanza kuwaneemesha watanzania katika nyanja mbalimbali.

0767 414 185

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.