Kwanini Uhuru na si CCM Kirumba?

Rai - - SPOTI - NA ABDUL MKEYENGE

HATIMAYE ule utata wa wapi pambano la watani wa jadi nchini litafanyika umepata jibu kufuatia mamlaka ya Bodi ya Ligi Kuu nchini (TPLB) kuutangaza rasmi uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kuwa ndio utakaotumika kwa mchezo huo.

Awali kulikuwa na hofu ya wapi pambano hilo litachezwa kufuatia Serikali kuufunga kwa matengenezo uwanja mkubwa wa Taifa ambao ndiyo hutumika kwa mechi baina ya watani wa jadi kwa kipindi kirefu sasa.

Hata hivyo baada ya taarifa rasmi kutolewa kwamba uwanja mkubwa hautatumika kwa mchezo wowote wa Ligi na kwamba utafunguliwa rasmi kuanzia Januari mwakani kulizuka taharuki ya wapi sasa mechi hiyo itafanyika huku kukichagizwa na hatua ya viongozi wa Yanga ambao kimsingi ndio watakaokuwa wenyeji wa mchezo huo wakitaka pambano hilo lipelekwe katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Uamuzi wa Yanga kutaka pambano hilo liende Mwanza kwanza ni kutokana imani ya kuwa na mashabiki wengi zaidi jijini humko ukilinganisha na wapinzani wao lakini pili ni dhana kwamba uwanja huo una uwezo wa kuchukua mashabiki wengi zaidi kuliko ule wa Uhuru jambo ambalo hata hivyo si la kweli.

Kufuatia hali hiyo kumekuwepo na mgongano wa mawazo na hata kimaslahi baina ya timu hizo wakati Yanga wakiamini CCM Kirumba ndio mahali sahihi kwa pambano la watani wa jadi baada ya ule wa Taifa huku Simba wao wamiamini Uwanja wa Uhuru ndio mahali salama kwa mchezo huo.

Hata hivyo toka Bodi ya Ligi Kuu iweke wazi pambano hilo kufanyika katika Uwanja wa Uhuru baadhi ya wadau wameendelea kuwa na hofu kwamba uwanja huo hauwezi kukidhi idadi ya mashabiki wanaoweza kujitokeza katika mechi hiyo ya watani kutokana na ukweli kuwa katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na idadi kubwa ya wanaohudhuria.

Lakini wakati hayo yakiendelea hebu tujiulize pambano hilo halijawahi kufanyika katika uwanja huo wa Uhuru? Ukweli ni kwamba miaka kadhaa iliyopita kabla ya kujengwa uwanja mpya pambano baina ya timu hizo lilikuwa likichezwa katika Uwanja huo tena wakati ule ukiwa na wastani wa kuingiza idadi ndogo sana ya mashabiki tofauti na sasa.

Takwimu zinaonesha kuwa Uwanja wa Uhuru una uwezo wa kuingiza mashabiki 27,000 wakati Kirumba ni 23,500 tu japo kulingana na mazingira yake ya kutokuwa na viti unaweza kufikisha hadi 25,000 kama ambavyo ilikuwa katika pambano baina ya Taifa Stars na Senegal Juni, 2007.

Kwa takwimu hizo ni dhahiri pambano hilo kuchezwea Uhuru ni sahihi kabisa.

Ni kweli kwa mahitaji ya soka la kisasa uwanja wa Uhuru ni mdogo kama utataka kuulinganisha na ule wa Taifa kwa kigezo cha idadi ya mashabiki lakini hii isiufanye mchezo huo kupelekwa sehemu nyingine.

TFF na Bodi nya Ligi kwa ujumla wanaweza kuweka utaratibu mzuri wa mashabiki kuingia uwanjani bila kuathiri usalama wao pamoja na mapato kwa ujumla.

Licha ya hivyo kuna baadhi ya mambo yanapaswa kuimarishwa uwanjani hapo kama suala zima la ulinzi kwa mashabiki na mali zao. Lakini sehemu nyingine zote Uhuru unakidhi haja ya kila anayehitaji kwenda uwanjani kuutazama mchezo husika.

Kabla ya uwanja huo kufanyiwa marekebisho ulikuwa umezungukwa na majukwaa sehemu zote, lakini matengenezo mapya yameufanya upande wa Kaskazini ukose majukwaa licha ya kwamba kitendo cha kutoweka viti baadhi ya majukwaa unaufanya uweze

kukidhi kuingiza watu zaidi ya ilivyokusudiwa.

Lakini hii haifanyi mchezo huo ushindwe kuchezewa uwanjani hapo. Kunahitajika maboresho ya ulinzi madhubhuti na kufanya kila shabiki aingie uwanjani na akae katika sehemu nzuri kwa usalama wake na usalama wa watazamaji wengine. Inawezekana!

Shida kubwa waliyonayo baadhi ya mashabiki wa soka nchini ni kuamini kuna mambo hayawezekani kwenye soka la Tanzania. Mashabiki hao wanaoupinga uwanja wa Uhuru hivi sasa ndiyo waliokuwa wakiupinga uwanja wa Azam Complex kwa timu za Simba na Yanga kwenda uwanjani hapo kucheza dhidi ya Azam.

Lakini kupitia safari ya Simba kwenda kucheza dhidi ya Azam Complex kucheza na Azam mwanzoni mwa msimu huu, kila kitu kimebadilika na sasa wadau wanaamini mipango na mikakati mikiwepo basi hakuna linaloshindikana katika suala la kudhibiti uingiaji wa mashabiki uwanjani.

Kilichofanyika uwanja wa Azam Complex ndicho kinachopaswa kufanyika hapo Uhuru utakapofanyika mchezo huo, japo pambano hilo ni kubwa zaidi ya lile la Azam na Simba pale Chamazi.

Ni aibu iliyoje kila kitu kusema haiwezekani kufanyika, bila ya kuja na suluhisho. Wacha mashabiki waende Uhuru kisha watanzania wajionee. Hizi kauli za ‘haiwezekani’ katika masuala mengi ndiyo yameufikisha hapa mpira wa Tanzania kuwa na sura ya mdororo kila siku.

Uwanja Uhuru, Dar es Salaam wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 25,000 ndio utakaotumika kwa pambano la watani wa jadi mwishoni mwa mwezi huu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.