Klopp, Mourinho jino kwa jino

Rai - - SPOTI - MWANDISHI WETU NA MITANDAO

BAADA ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa, uhondo wa michezo ya kuliwania taji la Ligi Kuu England unatarajiwa kurejea mwishoni mwa wiki hii. Mbali na michezo mingine, utakaovuta hisia za mashabiki wengi ni ule utakaozikutanisha liverpool na Manchester United.

Mtanange huo wa nane kwa kila timu kwa msimu huu utapigwa kwenye Uwanja wa Anfield wenye uwezo wa kupokea mashabiki wapatao 54,074.

Kikosi cha Man United kinachonolewa na kocha mwenye mbwembwe nyingi Jose Mourinho kitaingia kwenye mchezo huo kikiwa kinashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, kikilingana pointi na Manchester City waliojichimbia kileleni.

Mashetani Wekundu hao wameshinda mechi sita kati ya saba, wakiwa wamefunga mabao 21, lakini haijakutana na timu kubwa, hivyo Liver itakuwa kipimo chao cha kwanza tangu kuanza kwa msimu huu.

Liver, watakaokuwa mbele ya mashabiki wao, watapambana kufa na kupona kujinasua katika nafasi ya saba waliyopo sasa, baada ya kujikusanyia pointi na kufunga mabao 13. Ni wazi kocha Jurgen Klopp na vijana wake watataka matokeo ili kujisogeza kwenye nafasi za juu.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, timu hizo zimeshakutana mara 226,ambapo Man United inaongoza kwa kuibuka na ushindi (87), Liver wakishinda mara 75 tu, huku matokeo ya sare yakichomoza katika michezo 64. Lakini, katika mechi tano zilizopita kati yao, kila timu imeshinda mara moja huku michezo mitatu iliyobaki ikimalizika kwa sare.

Takwimu nyingine inayoufanya mchezo huo kuwa na msisimko mkubwa na kusubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Ligi Kuu England ni ile inayoonesha kuwa tangu kuanza kwa msimu huu, Liver hawajafungwa kwenye uwanja wao wa nyumbani kwani wameshinda mechi mbili na kutoa sare moja, huku Man United nao wakiwa hajafungwa ugenini, wakishinda mechi mbili na kutoa sare moja.

Katika hatua nyingine, kocha wa Liver raia wa Ujerumani, Klopp, atawavaa Man United akijua wazi kuwa safu yake ya ulinzi imekuwa ikifanya makosa ya kizembe yaliyosababisha kikosi hicho kuruhusu jumla ya mabao 12 hadi sasa.

Lakini, habari njema kwa mashabiki wa Liver ni kurejea kwa staa wao Sadio Mane ambaye amemaliza adhabu yake ya kutocheza mechi tatu. Msenegal huyo alikuwa uwanjani katika mchezo dhidi ya Newcastle licha ya Liver kutoibuka na ushindi.

Katika mtanange huo uliochezwa kwenye Uwanja wa St James’ Park, Klopp hakumtumia nyota wa kimataifa wa Brazil, Roberto Firmino, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kumpa nafasi Jumamosi dhidi ya Man United.

Liver wataendelea kuikosa huduma ya kiungo Adam Lallana ambaye bado anaendelea kusumbuliwa na majeraha yake ya paja na pia beki wa pembeni, Nathaniel Clyne, hatakuwa uwanjani siku hiyo kutokana na majeraha yake ya mgongo.

Mourinho naye atamkosa mchezaji wake wa bei kali, kiungo Paul Pogba, ambaye anatazamiwa kuwa nje kwa muda mrefu, hivyo kukosekana kwake kunaendelea kumpa nafasi Marouane Fellaini.

Huku mabeki wa Liver wakipaswa kuwa makini na Romelu Lukaku ambaye anaongoza orodha ya wafungaji kwa sasa akiwa na mabao saba, safu ya ulinzi ya Man United itakuwa macho kwa muda wote wa mchezo kumlinda Mohamed Salah, ambaye ameshazifumania nyavu mara nne. Kama alivyo Lukaku, mwanasoka huyo raia wa Misri amehusika kwa asilimia 33 katika mabao yote ya Liver msimu huu.

Pia, mashabiki wa Anfiled watakuwa wakimtegemea staa wao, Philippe Coutinho, ambaye amefunga katika michezo yote miwili iliyopita dhidi ya Leicester na Newcastle.

Lakini je,itakuwa rahisi kwa David de Gea ambaye tangu kuanza kwa mwaka huu ndiye kipa aliyecheza mechi nyingi (14) bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa? Bila shaka utakuwa ni mtihani mzito kwa safu ya ushambuliaji ya Liver,ikizinagatiwa kuwa kipa huyo wa kimataifa wa Hispania amefungwa mabao mawili pekee katika mechi saba za Ligi Kuu England.

Klopp Mourinho

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.