Kibiti ni uchumi sio siasa kinzani kimaendeleo

Rai - - MAKALA - NA SHERMARX NGAHEMERA

USEMI kuwa mchezea mwiba huota tende ndio hali halisi ya utata wa tatizo la Kibiti na wilaya zote za Mkuranga na Rufiji na tukifanya ajizi mambo yanaweza kuwa kombo zaidi.

Ninachofanya hapa ni kufikiri kwa sauti kubwa kuwa mtu mwenye njaa mara nyingi huwa ana hasira sana na iliyopitiliza kwani akizinduka hujisikia anaonewa na kila mtu na bila sababu. Ndio mchecheto ulioko Rufiji yote hadi Kilwa kwa maelezo ya Wanarufiji walioko Dar es Salaam ambao utawapata Mbagala, Tandika na Yombo Dovya.

Historia ya nchi yetu haijaandikwa kikamilifu na tumependa sana kutumia ile kauli funika kombe mwanaharamu apite tukisahau kuwa kwa kufanya hivyo tunakalia kuti kavu na upepo ukizidi tutaanguka nalo.

Chombo kimerudi ngamani na hakuna wa kutoa simile kwani jini subiani limetoka kwenye chupa kulirudisha ni kazi kubwa inayotaka chano na uvumilivu mkubwa kwani twapigana na kivuli chetu wenyewe.

Mganga au fundi anasema tujichunguze na kujisahihisha kwani adui ya mtu ni mtu nasi Wapogoro twalonga ‘Mlungu Chibidu’ yaani ogopa watu kwanza Mungu yuko mbali’.

Watu wanadai Tanzania haikupigana vita kupata uhuru wake na hivyo kuona Vita ya Majimaji, Vita ya Mtemi Bushiri na ile ya Mtemi Mkwawa kuwa ni vurugu tu na sijui wafe watu wangapi ionekane kuwa ni vita ya ukombozi. Watawala wa kikoloni hawakutaka kupigana kwani walikwisha onja ukali wake katika mapambano ya Majimaji na kwenye makabila mengine.

Uhuru wa Tanzania ulipiganwa Pwani au Jimbo la Mashariki kukiwa na mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Tanga na Pwani yenyewe ikiwa na maana ya Kisarawe, Bagamoyo, Kibaha, Kilwa, Mafia, Rufiji, Ulanga na Lindi.

Lakini cha maana zaidi ni kuwa nini kilitokea baada ya ‘rabsha’ hizo ndio kinasikitisha zaidi kwani wajanja waligeuza vibao na kuvutia kwao maendeleo na kusahau wapiganaji wao halali.

Ninapata tabu kidogo na kupata ukakasi mwingi kuzungumzia siasa uchumi za nchi hii kwani ni rahisi sana kuitwa mchochezi na kutoeleweka kwani zimekaa tenge kwa kupendelea upande wa Kaskazini mwa nchi yetu na kutelekeza eneo la Kusini mwa nchi. Ni pale tu aliposhika madaraka ya urais kwenye awamu ya tatu ndio Kusini kukakumbukwa kidogo. Mipango ya gesi ilipopamba moto ikaongeza umuhimu wa eneo hilo kwa uchumi wa nchi.

Haya ni maono tu kwani sote tuko sawa na hakuna wa pande hizo wa kulalamika kwani kama watu tumeingiliana sana bila ubaguzi wowote. Hayo si mageni ni wazi kabisa hata Mwalimu Nyerere aliyajua alipokuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kusini (South-South Commission) alipouona mgawanyo wa Kaskazini na Kusini na ule wa Mashariki na Magharibi ambao uko dunia nzima.

Kwani Vita ya Majimaji ilianza na ilipiganwa sana Rufiji, Kisarawe na Kilwa (Mkoa wa Pwani), Lukuledi (Nachingea) na Masasi (mkoani Lindi na Mtwara), Mahenge (Mkoa wa Morogoro), Njombe na Iringa (Mkoa wa Iringa, Mbeya na Songea (Mkoa wa Ruvuma) ambapo majenerali wa vita 8 wa Kingoni walinyongwa hadharani.

Mangi Sina wa Kibosho naye alinyongwa akipinga kutawaliwa na wakoloni kule Uchagani, Mkoa wa Kilimanjaro na vivyo kwa Mwinyi Bushiri wa Pangani.

Ni vema kukumbuka kuwa Julius Nyerere ambaye ni Baba wa Taifa alikuwa Mbunge wa Kwanza wa Jimbo la Pwani kwa maana ya Jimbo Mashariki (Eastern Province) mwaka 1958 katika Baraza la Kutunga Sheria (LEGICO). Tokea hapo moto wa kudai Uhuru ulipamba kila upande chini ya Nyerere na watu wa Pwani wakiwa vinara wa moto huo. Ulipopatikana Uhuru walisahauliwa vibaya na nafasi yao kuchukuliwa na wasomi waliotoka maeneo ambayo hayakupambana.

Ni ukweli unaouma kuona kuwa wale wanaochelewa kuingia kwenye mapambano mara nyingi ndio wanaofaidi matokeo ya mapambano hayo.

Kwa hasira wakoloni waliamua kutelekeza maeneo hayo yaliyokuwa mahasimu kwao na utawala baada ya uhuru ilifuata mwenendo ule ule wa kikoloni na kufanya maeneo hayo kutengwa na kufikika kwa tabu.

Lakini siku hizi kwa yaliyo mengi mambo yamebadilika kwani Serikali imefanikiwa kuunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za lami.

Hali imeanza kubadilika sana baada ya ugunduzi ya vikoleza pesa yaani kuweko kwa shughuli zakuzungusha fedha kwa wingi na hivyo kutamanika na wawekezaji na hivyo kugeuza meza kwa wa juu kuwa wa chini na wa chini wakawa juu.

Kwa maneno mengine mambo yamegeuka sana kwani wa mbele amerudi nyuma na wa nyuma sasa amekuwa mbele katika mstari ule wa maendeleo. Kijeshi tunasema ‘about turn’ yaani nyuma geuka! Ndio hali yetu sasa.

Kimitazamo ya kiuchumi Pwani, Mtwara na Lindi kuna uhai wa kiuchumi mkubwa kwa siku za usoni kuliko Kilimanjaro kutokana na kupatikana na kuchimbwa kwa gesi asilia ambayo imeshaanza kusababisha kuchanua kwa uchumi wa Tanzania. Hapo baadaye uchumi huo utaning’inizwa kwenye madini hayo na kwa mbali madini ya Kinywe ambayo yataanza kuchimbwa mwakani na yako kwa wingi, Lindi, Mtwara na Ulanga.

Warufiji na Mganga au Jenerali Kinjekitile kwao ni pale Muhoro Wajerumani walishindwa kumnyonga Kinjekitile kwani mara tatu aliponing’inizwa kamba ilikatika na hivyo kuachiwa huru kwani hukumu ilikuwa ni kunyongwa hadi kifo na si kuuawa na kwa vile majaribio matatu yalifanyika bila kufanikiwa ni kuwa hakustahili kufanyiwa hayo. Ni ukweli ambao Wazungu hawakutaka kuuzungumza kwani ulikua Kioja, nacho huwa hakizungumzwi kwani ni uchuro!

Hizo ndizo hekaya za Rufiji na zimekaa mioyoni mwa watu kuwa Wazungu walishindwa kuitawala Rufiji kwani watu wanaamini kuwa ipo mizimu ya Rufiji inayowatetea watu wake na hivyo hukubalika kutumia ndumba kwani inaonekana ina nguvu kuliko ukweli wowote utakaopelekwa hapo. Imani hiyo potofu ndio iliyoanzisha purukushani hizo na kuchochewa kwa mbali ushindi wa CCM juu ya Chama cha CUF ambao wengi wanafikiria wanafaa kushinda eneo hilo na kuingiza mtimanyongo kwenye siasa za Rufiji. Mitazamo ibadilike Matatizo makubwa ya kiutawala kwa wakoloni yalikuwa kusini ya nchi na huko ndiko kulikuwa motozaidi. Kwa muda mrefu Rufiji imekuwa kama daraja kwa wale watokao kaskazini na kusini na kama kilivyo kiuno hakina cha kwake ila kutegemea kinachohitaji kichwa au miguu ndio inakuwa ajenda yake.

Rufiji ina matatizo ya kiuchumi zaidi kuliko mambo mengine kwani njia za asili ya uchumi huo zimezingirwa na serikali na kufanya watu wa hapo kukosa kupumua.

Mbaya zaidi hakuna anayewajali wakati wao waliaminishwa na Baba wa Taifa kupitia marehemu mbunge wao Profesa Bakari Mikidadi aka Mbonde kuwa wao ni watu muhimu kwa ukombozi wan chi lakini mabadiliko ya uongozi yaliyofanyika hayatambui hali hiyo leo ila walionacho kwani uzalendo ni bidhaa adimu siku hizi ambapo fedha ni kila kitu.

Selous Game Reserve ni Rufiji na Rufiji ni Selous Game Reserve kwa urefu na mapana na jina lake mahsusi la ‘Shamba la Bibi’ kutamalaki mioyo ya watu nchi nzima. Ni kweli shamba la bibi kwani Mheshimiwa Makunganya na Mkwepu ni ushuhuda wa matokeo ya uwindaji huo kihalalai na walikuwa ni watu waliofanikiwa katika masuala ya uwindaji halali.

Kutoka Selous watu waliwawinda na kuua tembo, chui, simba, pundamilia na nyati na kuchukua nyama na nyara zao na kuzifikisha Dar es Salaam kwa wajanja waliwamo wawindaji wa haja wa enzi hizo akina Mkwepu na Makunganya na Bwana Peter, Mwingereza aliyekuwa mwindaji wa wanyama kibiashara na sio kitoweo.

Makunganya na Mkwepu kutokana na utajiri wao walitambuliwa kwa kupata mitaa Uhindini ambayo wanayo Mitaa mizima Jijini Dar es Salaam imeitwa kwa majina yao. Simile, kazi ya uwindaji ikaharamishwa na hivyo kuwaacha wengi masikini walio halali na wale wakibudu. Kuna haja ya kupima ukweli huu.

Kama ilivyo kawaida aliyezoea vya kunyonga vya kuchinja hawezi. Katika kutafuta cha mkono uende kinywani wengi wakawa majangili na operesheni zote za Serikali zilifyeka watu wa Rufiji na ushahidi ni kuwa nyumba za huko nyingi zimefikia ‘linta na kukwama’ na kubaki kuwa mapagale. Sio wao tu bali hata watu wa Ifakara, Mahenge, Tunduru na Liwale wote ni wahanga wa kukosa Vibali vya kuvuna mazao ya misitu na wanyama lakini waliendelea kushuhudia uwindaji wa kitaalamu na (Professional hunting ) na kibiashara ukifanyika kwa wageni na wale wenye navyo “kutoka Shamba la Bibi”; huku wenyeji wakizuiwa kwa mbinde za operesheni za mali asili ambazo zilijaa mateso na uvunjaji wa haki za binadamu. Ni kwa misingi hiyo zilisimamishwa.

Operesheni hizo mbili za vita ya Ujangili vya Uhai na Tokomeza ziliwafanya wananchi wawe na chuki dhidi ya serikali yao kwa kuwanyang’anya matonge mdomoni na kuachwa barabarani bila mpango mbadala.

Wachunguzi wa mambo wanadai ni makosa makubwa kuwa na mipango ya kukatisha tamaa kwenye operesheni ambazo sio shirikishi na zilizojaa uzandiki ambapo watu wabaya wamezitumia kuwamaliza washindani wao kibiashara. Inafaa tukumbuke mpaka hivi karibuni tu kuwinda tembo na wanyama pori ilikuwa shughuli halali na yenye heshima katika nchi hii ili kupunguza idadi ya wanyama hao kulingana na uwezo wa ikolojia husika (culling). Sasa vilio vimeanza kila mahala kuwa wanyama pori wanakula mazao ya wakulima tufanyeje? Mgongano wa mawazo Huku wakiambiwa wao walinde wanyama hao wengine waliruhusiwa kuwinda kwa vibali maalumu na hivyo kutoa taswira isiyoeleweka kwa wengi na kudai kuwa mbuga hiyo imekuwa mradi wa wakubwa tu na watu wa kawaida wasichume utajiri ambao kwa miaka mingi ulinufaisha jamii hiyo ya Wanarufiji na hata Wana Ulanga wanaouzunguka shamba la bibi.

Kadiri siku zilivyopita kamba ilikuwa inakazwa kiasi cha kukatisha tamaa na kuonekana kuwa ni uonevu na sio uhalali wa kutunza rasilimali za taifa. Hakuna haja ya kurudia yanafahamika kwa uma kwani yalifanyika nchi nzima.

Mlundikano wa mawazo hasi na misononeko kwa maisha yao ndio chimbuko la matatizo yote kwani vijana wao walionekana kukosa subira kwani hata shule hawakusoma, hawakutaka kusoma kwani wao walitaka sana madrasa kuliko elimu dunia na hivyo kugongana mawazo na mwelekeo wa taifa zima kwenye elimu.

Viongozi wao kisiasa walionekana kuwa wanafanyakazi na maadui wa tija yao kiuchumi na hivyo kuingia lawamani na kuangamizwa. Walionekana kama ni wasaliti.

Masuala ya uchumi yameleta tafrani za kisiasa eneo hilo na kupotosha mwelekeo wa suala zima kwa kufanya wakazi wa Rufiji wakate tamaa ya maisha na kuwa viruu kama mbogo waliojeruhiwa kwa uchungu na kutishiwa maisha. shermarxn@ gmail.com

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.