TANZANIA YASAIDIA SUDAN KUONDOLEWA VIKWAZO

Rai - - MBELE - NA MOSES NTANDU

KATIKA kile ambacho Taifa la Sudan lilikuwa likikingoja kwa miaka kadhaa na kwa hamu kubwa, ni suala la kuondolewa vikwazo vya kiuchumi ambavyo taifa hilo liliwekewa na taifa la Marekani kwa takribani muongo mmoja sasa.

Moja ya sababu kubwa ya taifa hilo kuondolewa vikwazo ni kile kilichoelezwa na taifa la Marekani kuwa ni pamoja na kuimarika kwa hali ya usalama na utulivu katika Jimbo la Darfur, ambapo kwa miaka mingi Tanzania kupitia Jeshi la Wananchi (JWTZ) limekuwa likiendesha shughuli za ulinzi wa amani jimboni humo.

Licha ya kupoteza wapiganaji wetu kadhaa jimboni humo, leo Sudan inasherehekea kuondolewa vikwazo ambavyo viliwekwa na Marekani kwa nchi hiyo kufuatia kuonekana kuwa na vurugu za mwenyewe kwa wenyewe jimboni Darfur nchini humo na pia suala la ugaidi ambalo ilionekana kuwa taifa hilo lilikuwa likiunga mkono na kufadhili baadhi ya makundi ya kigaidi.

Kwa sasa hali imeimarika sana jimboni Darfur na maeneo mengi nchini humo ingawa bado kuna maeneo machache ambayo bado yanahitaji juhudi za Serikali ya taifa hilo kuikabili hali hiyo kwa baadhi ya maeneo ili kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinapatikana kila kona ya taifa hilo.

Darfur ya leo ni salama sana kila kona, huku shughuli nyingi za maendeleo kwa wananchi zikiendelea, nimefika jimboni humo mara kadhaa kufanya tathmini ya kile kinachoelezwa kuwa ni kuimarika kwa hali ya usalama na kushuhudia mabadiliko makubwa ya kiusalama huku nikishuhudia mikusanyiko mingi ya wananchi wakiwa katika shughuli za kawiada ikiwemo harusi matamasha ya michezo na kila kona kukiwa na harakati za shughuli mbalimbali za maendeleo na ujenzi wa taifa lao.

Katika hali ambayo kwa miaka ya nyuma haikuwa ni kawaida kuona kuna utulivu jimboni Darfur, kulikuwa na hofu na mapigano kila kona, lakini kwa sasa kila uzungukapo mitaani katika miji ya majimbo yote manne ya Darfur Magharibi, Darfur Kusini, Darfur ya Kati na Darfur Kaskazini hali ni shwari sana. Shughuli mbalimbali zinaendelea katika miji ya El Geneina, Nyala na Al Fasher ambayo ni miji mikukwa katika ukanda huo wa Darfur.

Nilizunguka kwa sehemu kubwa katika mitaa ya mji wa Al Fasher na kufanikiwa kukaa vijiweni na kupata vyakula vya asili kama nyama maarufu ya kuchoma iitwayo ‘Sheiya’ na kula mikate na chapati kwa mlenda. Kwa kweli hali imeimarika sana jimboni humo tofauti na nilipoweza kufika jimboni humo miaka saba iliyopita kwani kwa kipindi kile mitaa ilikuwa haina watu wengi huku kukiwa na pilikapilika za vikosi vya kulinda amani vikizunguka mitaani.

Pia kulikuwa na kambi kadhaa za wakimbizi wa ndani jimboni humo ikiwemo kambi zilizokuwepo katika mji wa Al Fasher jimboni humo, lakini kwa sasa kambi nyingi zimefungwa huku wakimbizi wale wakirejea vijijini mwao na kuendelea na kazi mbalimbali zikiwemo za kilimo, ufugaji na biashara.

Kwa upande mwingine zile kelele za kugombea mji mdogo wa Abyei zimekwisha na hali imeendelea kuimarika sana kwa sasa. Kuhusu mgogoro wa Abyei sio suala la malumbano tena muda huu ingawa sitazungumzia sana suala la mgogoro wa Abyei katika makala hii kwani mgogoro huo utahitaji uchambuzi wake pekee kwani nilifanikiwa pia kufanya utafiti na uchunguzi katika suala la mgogoro huo pia nikiwa nchini Sudan na kubaini mambo kadhaa yaliyokuwa yakichangia katika mgogoro ule. Suala la mgogoro huo wa Abyei nitauchambua katika makala nyingine zijazo.

Pongezi za kipekee zinapaswa kupelekwa kwa jeshi letu JWTZ kwani limeweza kufanya kazi kubwa sana jimboni Darfur kwa kipindi chote cha mgogoro uliokuwepo jimboni Darfur nchini Sudan, majeshi yetu yameweza kufanya kazi kubwa kwa ushirikiano na majeshi ya nchi nyingine kwa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani jimboni Darfur kikosi cha UNAMID na sasa ukanda huo umetulia na hali ni shwari kabisa.

Hivi leo serikali ya Marekani imeiondolea vikwazo Sudan ikisema taifa hilo kwa kiwango kikubwa limefanikiwa kukabiliana na mgogoro wa Darfur na limeweza kukabiliana kwa kiwango kikubwa sana na masuala ugaidi pamoja na ukiukaji wa haki za kibinaadamu dhidi ya raia wanaoishi katika jimbo la Darfur na sehemu nyingine nchini humo Sudan.

Uamuzi wa kuiondolea Sudan vikwazo na kusitisha vikwazo vya kiuchumi umekuja baaya ya serikali ya Marekani kupitia rais wa nchi hiyo Donald Trump mwezi uliopita kuliondoa taifa hilo katika orodha ya mataifa ambayo raia wake wamewekewa vikwazo vya kiuchumi, na kulifanya taifa la Siudani kuwa huru kutoka katika vikwazo hivyo vya kiuchumi.

Suala hili la kuondolewa vikwazo limefanyika kwa taifa moja tu la barani Afrika, taifa la Sudan katika kipindi hiki cha utawala wa rais Trump na kufanya kuwa Sudan ndio taifa pekee ambalo limeondolewa katika orodha hiyo duniani huku mataifa mengine yaliyowekewa vikwazo na Marekani yakiendelea kusalia katika orodha ya mataifa yaliyowekewa vikwazo.

Kuondolewa kwa vikwazo hivi kwa taifa la Sudan unagusa mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa taifa huku uamuzi huo ukiviacha vikwazo vingine kuendelea kwa sasa ikiwemo vile dhidi ya watu binafsi walio na agizo la kukamtwa kufuatia unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanyika katika eneo la Darfur.

Hii maana yake ni kwamba Serikali ya Sudan inakuwa huru sasa kufanya biashara moja kwa moja na taifa la marekani hali ambayo itaweza kuimarisha uchumi wa taifa hilo, uchumi uliokuwa umedorora sana na kusababisha wananchi wa taifa hilo kuishi katika hali mbaya sana kutokana na kukosna huduma bora za afya, elimu na hata miundombinu ya usafiri wa anga pia kudorora kwa kilimo ambacho ni sehemu kubwa ya uchumi wa taifa hilo.

Katika kuonesha kuwa taifa hilo limedhamiria kubadilika na kuanza kukabiliana na ugaidi, majuma mawili yaliyopita taifa hilo liliweza kuwa mwenyeji wa Mkutano wa wakuu wa taasisi za usalaama barani Afrika maarufu kama CISSA huku mada kuu ikiwa ni kujadili na kupeana uzoefu wa kukabiliana na masuala ya ugaidi barani Afrika.

Kwa michakato hiyo Taifa la Sudan limefanikiwa kuondolewa vikwazo na taifa la Marekani huku Tanzania ikichangia kwa kiwango kikubwa sana kulisaidia taifa hilo kuimarisha na kuboresha hali ya usalama jimboni Darfur, hali ambayo imechangia na kusaidia taifa hilo kuondolewa vikwazo na taifa la Marekani

Tanzania imekuwa ikishiriki katika mchakato wa kulinda amani nchini Sudani toka kuanza kwa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha UNAMID kulinda amani katika jimbo hilo la Darfur nchini Sudan toka mwaka 2007.

Taarifa zilizotolewa na Umoja wa Mataifa kutoka katika kikosi hicho ni kwamba, kimepoteza wapiganaji wapatao 50 toka walipoanza operesheni hiyo ya kulinda amani jimboni humo to mwaka 2007 hadi kufikia mwaka 2013, huku Tanzania ikipoteza takribani askari kumi waliokuwa katika shughuli hiyo ya kulinda amani jimboni humo.

Mwandishi wa Makala hii ni Mwandishi na Mtafiti katika Kituo cha kutoa Taarifa kwa Umma Tanzania (TCIB) anapatikana kwa namba 0714 840656 na Baruapepe mosesjohn08@yahoo.com

Rais wa Sudan, Omar

Hassan Al Bashir

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.