RAILA ODINGA AIBUKA NA MADAI MAPYA

Rai - - MBELE -

ALIYEKUWA mgombea urais kwa tiketi ya Muungano wa NASA nchini Kenya, Raila Odinga ameibuka na madai mapya kwa kutaka upande wa Magharibi mwa Kenya uwe Taifa huru.

Mwanasiasa huyo ameeleza kuwa anaona haja ya kusimamia hoja hiyo kutokana na mwenendo wa uongozi wa kikabila unaondelea nchini humu kwa miongo zaidi ya minne sasa.

Odinga aliyasema hayo katika mahojiano maalum aliyoyafanya jijini London nchini Uingereza na gazeti la Financial Times.

Alisema hakuwa akiunga mkono madai ya kujitenga kwa eneo la Magharibi mwa Kenya ambako ana wafuasi wengi wanaotoka katika makabila Luo na Luhya, lakini sasa hivi anaona kuna haja ya kuwapo kwa mjadala wa kudai mamlaka huru ya maeneo hayo.

“Watu wanapofikia hali ya kukata tamaa, huweza pia kuchukua hatua za kukata tamaa kwa muda mrefu utawala wan chi hii umekuwa unashikiliwa na watu wa makabila mawili ya Wakikuyu na Wakalenjini, makabila ambayo yamekuwa yakitoa rais tangu uhuru mwaka 1963.”

Rais wa sasa wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta ni Mkikuyu na Naibu wake ni William Ruto ambaye ni Mkalenjin.

Mgogoro wa kisiasa unaoendelea sasa nchini humo uliibuka baada ya Kenyatta kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa Agosti 8, mwaka huu akimshinda Odinga.

Raila, ambaye ni Mluo alifanikiwa kutengua ushindi wa Uhuru kupitia Mahakama ya Juu (Supreme Court), lakini amekataa kushiriki katika uchaguzi wa marudio hadi kufanyike marekebisho katika utaratibu wa kufanya uchaguzi, na kufumuliwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliyomtangaza Uhuru kuwa rais.

Aidha Raila amepuuzia maamuzi yote yaliyojiri katika Mahakama Kuu na ndani ya Bunge juu ya uchaguzi huo wa marudio kwa kudai kuwa hayana maana yoyote.

Amesema iwapo uchaguzi huo utafanyika bila ya yeye kushiriki, itakuwa ni ukiukwaji mkubwa wa katiba na kuufanya uchaguzi huo kuwa batili.

Wakati mkwamo wa kisiasa unaendelea, maandamano ya wafuasi wa Raila nayo yanazidi kufanyika sehemu mbali mbali nchini humo na waandamanaji wamekuwa wakidai kufumuliwa kwa IEBC, pamoja na nguvu ya mamlaka ya kipolisi kutumika katika kuyazuia tayari watu kadhaa wameripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi.

Aidha maeneo kadha ambayo ni ngome za Raila zimeiambia IEBC isithubutu kupeleka maafisa wala vifaa vya kupigia kura katika maeneo hayo siku ya uchaguzi huo wa marudio iwapo haitafanyiwa marekebisho.

Maeneo yaliyotishia kufanya hivyo ni ya majimbo ya Kitui, Siaya na Migori na inatarajiwa majimbo mengine yatafuata.

John Githongo, mwanaharakati maarufu wa mapambano dhidi ya ufisadi nchini Kenya amesema ingawa kumekuwa hakuna vuguvugu la kujitenga nchini humo, mkwamo huu wa kisiasa umeibua mjadala mzito kuhusu suala hilo.

“Kama ni mjadala, basi mjadala huo una “miguu” kwani baadhi ya mabango ya waandamanaji yamekuwa yakibeba ujumbe huo na hali inatisha.”

Mwishoni mwa mwezi uliopita wakazi wawili wa maeneo ya Magharibi ya Kenya walipeleka ombi Mahakama Kuu ya Kenya wakitaka kufanyike kura ya maoni kuhusu haki ya kujiamulia mambo yao wenyewe.

David Ndii, mshauri mwandamizi wa Raila Odinga ambaye mwezi Agosti alizungumzia hoja ya kujitenga, wiki iliyopita alisema sasa haiungi mkono.

Hata hivyo aliongeza wako katika mazingira ya kisiasa ambayo wakati wowote yanaweza yakaanza kutetereka kutoka mlimani na yanaweza kuelekea upande wowote kwani hakuna anayejua.

“Nchi imegawanyika kwa kiwango kikubwa ambacho hakijapata kutokea.”

Wakati hayo yakijiri, Umoja wa Ulaya (EU) umekitaka chama tawala cha Jubilee na umoja wa NASA kuacha misimamo yao mikali na badala yake waruhusu kuwepo kwa uchaguzi wa marudio unaokubalika.

Mwanzoni mwa wiki hii timu ya watazamaji ya EU ilisema kuwa kunahitajika mazungumzo na ushirikiano ili kuwepo kwa mchakato halali na wa uwazi wa uchaguzi ili Wakenya wapate rais wanaemtaka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.