Uchaguzi Kenya giza tupu

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

WAKENYA wanatarajia kufanya uchaguzi wa marudio wa kumchagua Rais wao leo baada ya ule wa awali uliofanyika Agosti 8, mwaka huu kufutwa na Mahakama ya juu kwa kile kilichodaiwa ni kukiukwa kwa baadhi ya taratibu.

Uchaguzi wa leo unatarajiwa kufanyika huku kukiwa na sintofahamu kutokana na mpinzani mkuu kwenye mbio za urais, Raila Odinga kujiengua kwenye mbio hizo kwa madai ya kutokubaliana na baadhi ya mambo ndani ya Tume huru ya uchaguzi nchini humo pamoja na udhaifu wa demokrasia.

Inaelezwa kuwa mfumo dhaifu wa demokrasia nchini Kenya unaendelea kujionyesha katika rangi mbalimbali ingawa kuna wakati ulileta matumaini kutokana na muafaka hata hivyo hali hiyo ilibadilika ghafla.

Haya yote yamejiri katika kipindi cha miezi miwili tu iliyopita, hata hivyo matumaini makubwa yalifikiwa miaka saba iliyopita baada kupatikana kwa Katiba mpya ambayo ilisifiwa kuwa ni miongoni mwa katiba bora kabisa barani Afrika na hivyo kuweza hata kuigwa na nchi nyingine.

Wadadisi wa mambo wanasema hakuna mahali Afrika panapokosa siasa chafu, jambo linalosukumwa kwa kiasi kikubwa na ile hali ya kutoaminiana miongoni mwao.

Aidha, wanasema siku hizi katika Bara la Afrika, na katika nchi nyingi za ulimwengu wa tatu, hasa katika masuala ya siasa zinazidi kuwa kivutio kwa wanasiasa wengi – walio madarakani hupenda kung’ang’ania walipo na wale walio nje wakitumia kila njia kuingia.

Kenya ukweli unabakia kwamba nchi inaweza kutumbukia katika ghasia kubwa iwapo wanasiasa wataendelea kushikilia misimamo yao mikali.

Rais Uhuru Kenyatta aliye madarakani anayegombea kipindi chake cha pili anakazania kufanyika kwa uchaguzi kama ilivyoelekezwa katika hukumu ya Mahakama ya Juu (Supreme Court) baada ya kubatilisha uchaguzi wa Agosti 8 ambao ilisema Katiba, sheria na kanuni zilikiukwa katika uendeshaji wake.

Kwa upande wake mgombea mkuu wa muungano wa upinzani wa NASA, Raila Odinga amejitoa katika uchaguzi huo akitaja kwamba uchaguzi huo wa marudio hautakuwa wa kuaminika kutokana na kusimamiwa na tume ile ile ya IEBC ambayo ilivuruga uchaguzi awali.

Raila alitaka kwanza kuweko mabadiliko katika tume hiyo ndiyo uchaguzi ufanyike.

Kutokana na msukumo wa nchi za Magharibi Rais Uhuru Kenyatta hatimaye alikubali maamuzi ya Mahakama ya Juu ya kubatilisha uchaguzi wa Agosti 8, lakini baadaye alionekana kuchukua hatua kadha yaliyobeba ishara ya kuyazunguka maamuzi hayo.

Chini ya hati ya dharura, utawala wake ulipeleka muswada wa marekebisho bungeni wa Sheria ya Uchaguzi ya kuweka ugumu kwa mahakama kubatilisha uchaguzi. Marekebisho hayo yalitaka iwapo mgombea urais hana mpinzani basi atangazwe moja kwa moja kuwa mshindi.

Hali kadhalika Kenyatta alishindwa kutoa msukumo wa kuifumua Tume ya Uchaguzi kama wanavyodai NASA na hivyo kuzidisha hali ya mkwamo.

Wadadisi wa mambo wanasema iwapo Kenya itafanya uchaguzi leo itakuwa inafanya makosa makubwa, ushauri wa busara ni kwa Tume kuahirisha uchaguzi huo.

Wanasema kisheria ni IEBC pekee ndiyo ina uwezo wa kufanya hivyo iwapo itaona kwamba kufanyika uchaguzi kunaweza kuleta vurugu kubwa hadi kutishia uhalali wa matokeo.

Tayari nchi hiyo imetawaliwa na maandamano na matishio katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, hasa yale yanayomuunga mkono Odinga.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.