Gavana mpya abebeshwa mzigo mzito

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

KUTEULIWA kwa Profesa Florens Luoga kuwa Gavana wa saba wa Benki Kuu Tanzania (BoT), kunatajwa kuwa na tija kubwa kwa nchi kutokana na uwezo wa msomi huyo aliyebobea kwenye masuala ya kodi na utafiti. RAI linachambua.

Matumaini hayo ya Watanzania wengi kwa Prof. Luoga yanasukuma dhana ya kumbebesha mzigo mzito wa matumaini kwa imani kuwa atatenda kile ambacho wananchi wengi wanakitarajia kutoka kwake.

Prof. Luoga ambaye anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Gavana wa sasa, Benno Ndulu juzi alimwagiwa sifa kedekede na Rais Dk. John Magufuli kutokana na utendaji wake uliotukuka.

Rais Magufuli alisema amemteua Prof. Luoga kutokana na kazi nzuri aliyoifanya akiwa katika kamati ya majadiliano baina ya serikali na kampuni ya Barick Gold.

“Kwa kazi nzuri iliyofanywa na kamati hii ya makinikia, nimeamua kumteua Prof. Luoga kuwa Gavana mpya wa Benki Kuu baada ya gavana aliyekuwapo kubakiza siku chache kumaliza muda wake,” alisema Rais Magufuli.

“Na kwa kuwa nimeshazungumza, gavana aliyekuwapo atafanya haraka haraka kumkabidhi majukumu gavana mpya.”

Alisema Prof. Luoga ni mtaalamu wa masuala ya sheria ya kodi, hivyo watu wanaofungua akaunti za fedha nje ya nchi mwisho wao umefika.

Alisema wakati anafanya uteuzi huo, hakumweleza Prof. Luoga kama atamteua kuwa gavana mpya, lakini kwa kuwa imeshatokea “inabidi akubaliane na uteuzi”.

Kauli hiyo ya Rais pamoja na mambo mengine imeibua matumaini makubwa kwa wananchi wakiamini sasa Benki Kuu imepata mtu sahihi wa kuisimamia.

Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dk. Abuu Mvungi juzi alinukuliwa akisema kuwa Prof. Luoga ni mchapa kazi na mtaalamu wa kodi na kwamba anaouwezo wa kufanya kazi katika misingi sahihi.

Dk. Mvungi alisema nchi ilipofikia inahitaji mtu mzalendo, mwadilifu, msafi wa kupigiwa mstari, asiye na doa na kwamba Prof. Luoga anazo siofa hizo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe ambaye pia ni mtaalamu wa Uchumi, Profesa Honest Ngowi alisema Rais Magufuli amefanya uamuzi mzuri wa kumteua Profesa Luoga.

Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja nae alimwagia sifa Prof. Luoga kwa kuweka wazi kuwa nafasi aliyopewa anaiweza kwa sababu anaouwezo mkubwa.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Humprey Moshi, nae kwa upande wake alinukuliwa akisema kuwa gavana mteule anaouwezo wa kuleta mageuzi makubwa, lakini anapaswa kuangalia utekelezaji wa Sheria ya Utakatishaji Fedha kwa kudhibiti na kusimamia maduka ya kubadilisha fedha.

Alisema maduka hayo kwa muda mrefu yamekuwa yakiendeshwa kiholela bila usimamizi mzuri wa BoT.

Alisema kinachotakiwa sasa ni kuhakikisha kila duka linakuwa sehemu ya benki ya biashara na lisiwapo hata moja linalojiendesha bila kufungamanishwa na benki.

Prof. Moshi alisema Gavana mpya wa BoT anapaswa kudhibiti matumizi ya Dola nchini, akizitolea mfano nchi zenye uchumi imara kama vile Afrika Kusini ambayo haziruhusu matumizi ya Dola nchini mwake.

Profesa Razack Lokina kwa upande wake alieleza kuwa matumizi ya Dola kwenye bei ya bidhaa madukani au kwenye nyumba za kupanga ni changamoto kubwa kwa kuwa wengi huwa na viwango vyao vya kubadili fedha na siyo vilivyopo kwenye soko.

JUKUMU LA MSINGI LA BOT

Jukumu la msingi la Benki Kuu ya Tanzania ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kujenga mfumo wa fedha ulio imara na unaofaa kwa ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.

KAZI NYINGINE

a. Kutoa sarafu ya nchi ambayo ni Shilingi ya Tanzania. b. Kusimamia mabenki na taasisi za fedha c. Kusimamia na kudhibiti mifumo ya malipo nchini d. Kuhifadhi akiba ya nchi ikiwemo fedha za kigeni e. Kutoa ushauri juu ya masuala ya uchumi na fedha kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar f. Benki ya Serikali, na g. Benki ya Mabenki.

BODI YA WAKURUGENZI

Bodi ya Wakurugenzi ni chombo chenye madaraka na mamlaka ya juu kinachotoa maamuzi ya kisera katika muundo wa Benki Kuu ya Tanzania. Kwa mujibu wa kifungu cha nane (8) cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, Bodi ya Wakurugenzi ina wajibu wa kuamua sera za Benki Kuu, kuidhinisha bajeti na mgawanyo wa faida inayotokana na shughuli zake.

Bodi ina wajumbe 10. Wanne ni wakurugenzi watendaji wanaoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; wajumbe wawili wanaoingia kutokana na nyadhifa zao na wengine wanne wanateuliwa na Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katibu wa Benki Kuu pia ni mjumbe anayeingia kwa wadhifa wake mwenye wajibu wa kutoa huduma za Sekretarieti.

MUUNDO WA BODI

Muundo wa Bodi ya Benki Kuu ni kama ifuatavyo: • Gavana (Mwenyekiti); • Manaibu Gavana watatu, Makamu Mwenyekiti, kwa mfuatano atakaoamua na Gavana wa Benki; • Mwakilishi wa Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; • Wakurugenzi wanne wasio watendaji; na • Katibu wa Bodi.

MAJUKUMU YA BODI

Katika kufanya kazi zake; Bodi ya Wakurugenzi inasaidiwa na Kamati nne, mbili miongoni mwao zimeundwa kisheria. Kamati hizo mbili ni Kamati ya Sera ya Fedha na Kamati ya Ukaguzi. Bodi ya wakurugenzi inayo mamlaka ya kuunda kamati zingine kadiri inavyoona inafaa. Zaidi ya kamati zilizoundwa kisheria, Bodi imekasimu baadhi ya majukumu yake kwa kamati nyingine mbili, ambazo ni Kamati ya Usimamizi wa Shughuli za Benki na Kamati ya Fedha na Uwekezaji.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.