Vurugu FDL zinakimbiza wadhamini

Rai - - MICHEZO - ABDUL MKEYENGE

VURUGU viwanjani kwenye michezo ya Ligi Daraja la Kwanza Nchini (FDL) ni kama imekuwa jadi sasa katika soka la Tanzania katika miaka ya karibuni. Hali ya vurugu imekithiri kwa kiwango kikubwa mno.

Mashabiki wanapigwa, waamuzi wanapigwa, wachezaji wanapigwa, makocha wanapigwa. Hii ndiyo FDL inayotoa timu za kuja kushiriki mikikimikiki ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Hali imeshakuwa mbaya viwanjani.

Kila mmoja amekuwa na hofu na mwenzie. Wakati kwenye michezo ya Ligi Kuu viwanja vikiwa sehemu ya vivutio, hali ni tofauti siku kukichezwa michezo ya FDL ambako viwanja hivyo vinageuzwa ulingo wa masumbwi kwa watu kupigana bila woga. FDL ndiyo imefikia hapa kwa sasa.

Tangu kuanza kwa msimu huu wa ligi hiyo kumeshatokea vurugu kwenye michezo minne tofauti, ajabu iliyoje ndani ya vurugu hizo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekaa kimya, kama halioni au halijui yanayotokea kwenye michezo ya ligi hiyo huku wao wakiwa ndio wasimamizi wakuu.

Vurugu hizi zilizoota magugu kwenye soka letu, haziwezi kuisha kwa ukimya huu wa TFF ambao kama wameitenga ligi yenyewe. FDL kuna uozo mwingi unaopaswa kuondolewa ili kuwepo na usawa kwa timu zinazopanda Ligi Kuu Bara na maendeleo ya soka la Tanzania kiujumla wake.

Muda mrefu sasa kuna timu zinapanda Ligi Kuu Bara zikitokea FDL bila kuwa na uwezo. Timu nyingi zinajipanga zaidi nje ya uwanja ambako kunafanyika mipango mingi kinyume na kanuni zinazosimamia mchezo huo. Ina maana TFF hawayajui matatizo haya?

Muda huu ambao TFF imepata viongozi wapya madarakani tulipaswa kuona makali yao kwenye matatizo ya namna hii ili heshima ya FDL irudi haraka, lakini ukimya wao unatishia kuturudisha kule tulikotoka.

TFF kama inashindwa kutoa taarifa au onyo kwenye FDL ni ligi gani nyingine inayoweza kwenda kukemea na ikaeleweka? FDL iko karibu na Ligi Kuu Bara, hivyo hapa kulihitajika umakini wao kwa timu zinazokuja juu, sio kufumbia macho madudu haya yanayoendelea.

Bodi ya Ligi (TPLB) haina mamlaka makubwa na FDL kutokana na bodi hiyo iko kwa ajili ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara. Hivyo zigo la FDL ni la TFF kwa namna yeyote ile, japo viongozi wa timu za FDL wanaingia kwenye upigaji wa kura kuwapata viongozi wa TPLB.

Kalamu yangu haiamini kama TFF inashindwa kumaliza matatizo haya ya FDL yanayolipaka matope shirikisho hilo na mpira ukachezwa kwenye mizani ya usawa bila timu kudhulumiana, lakini wanaonekana hawako tayari kumaliza matatizo haya yanayotokea kila msimu sasa.

Inawezekana vipi vurugu za namna hii zisionekane Ligi Kuu Bara ziishie kuonekana FDL na madaraja mengine ya chini? TFF hawako tayari kufuta kero hizi za FDL na siku wakiwa tayari kuondoa uhuni huu,tutashuhudia soka murua linalochezwa na vijana wenye vipaji.

TFF iko makini na Ligi Kuu Bara ndiyo maana tunayoyaona kwenye FDL hatuyaoni Ligi Kuu Bara. Mapigano ya mwisho kutokea FDL ni ile ya mchezo wa Yanga dhidi ya Azam, Uwanja mkuu wa Taifa.

Lakini tangu kutoka kwa vurugu hizo zilizofanywa na wachezaji wa Yanga, Jerson Tegete, Stephano Mwasika na kufanya wafungiwe kwa miezi kadhaa baada ya kumpa kichapo mwamuzi Israel Mujuni Nkongo, na kufuatia ile ya mashabiki wa Simba kung’oa viti mmsimu uliopita katika mechi ya watani hakuna vurugu nyingine kubwa iliyotishia maisha ya mtu katika michezo ya Ligi Kuu Bara.

TFF kama taasisi iamke na ianze kukomesha masuala haya yanayotokea uwanjani. Ukimya wao ndiyo unaofanya hao wanaoleta fujo wajione kama watu salama, kumbe ni watu wanaoharibu sura nzima ya soka.

Vurugu hizi zinatupa maana ya kwanini FDL haina mdhamini wa kudumu. Hakuna mdhamini anayeweza kuwekeza fedha zake au rasilimali zake kwenye vurugu ambako hakuna heshima. Mdhamini anataka unyenyekevu. Kwa hali hii ya FDL mdhamini anayeweza kuja?

Kando ya ubora wa soka na ushawishi kutoka kwa timu kwenda kwa wawekezaji, wawekezaji hawapendi vurugu, si kitu kingine, lakini aina hii ya uendeshaji ulioko FDL ni ngumu kumpata hata mdhamini wa kutoa vifaa kwa timu zote shiriki. Ni ngumu kujitokeza. FDL haina heshima.

TFF ilipaswa kuisimamia vyema ligi yake ili iwavutie watu wengi, kisha baadae iwachie majukumu ya kutafuta wadhamini watu wa masoko wa timu hizo, lakini kwa uendeshaji huu uliokosa heshima FDL itaendelea kubaki hivi kwa miaka mingi, bila TFF kuingilia kati.

Kama hali hii itaendelea kuwepo tena na tena, kisha TFF ikashindwa kuchukua hatua stahiki, muda si mrefu tutatoka nje na kuwauliza wanaiona FDL au wanaisikia? Si dhambi kuwauliza hivi!

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.