Mzindakaya amchambua Magufuli

»Awataka wanasiasa wasifanye makosa kulinganisha marais

Rai - - MBELE - NA GABRIEL MUSHI

Una haja gani ya kutembea na kufanya maandamano? Pia vyama vyetu vina wabunge ambao wataenda kwa niaba ya chama kuwashukuru.

WAKATI uongozi wa Rais Dk. John Magufuli ukielekea kutimiza miaka miwili tangu aingie madarakani Novemba 5, 2015 mwanasiasa mkongwe nchini, Dk. Crisant Mzindakaya ameuchambua utendaji wa kiongozi huyo wan chi. RAI linaripoti.

Mbali na kumchambua Rais Magufuli pia Dk. Mzindakaya amewalipua baadhi ya wanasiasa wanaopenda kuwaponda viongozi wa Serikali za awamu zilizopita.

Katika mahojiano maalum na RAI yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, alisema Rais Magufuli anapigania kwa dhati rasilimali na maslahi ya nchi.

Alisema kitendo cha Rais kupigania rasilimali za Taifa kama vile madini na gesi ni jambo la kupongezwa kwa sababu wanasiasa wengi wa Afrika ni waoga kupambana na wawekezaji wazungu.

“Tanzania ndio tajiri wa rasilimali Afrika, unaweza kutulinganisha na Congo (DRC) ingawa pia tumewazidi baadhi ya vitu kwa mfano hawana bahari ambayo ni chanzo cha chumvi. Kwa hiyo rasilimali iliyopo Tanzania ni kubwa na mtu wa kwanza kuilinda ni rais wa nchi anatakiwa kuwa na uchungu kwa rasilimali za nchi na kuhakikisha zinatumika kwa masilahi ya watu wake. Na ndicho anachokifanya Rais Magufuli.

“Suala la madini limekuwa mfano kwa Afrika kwani mara nyingi hata viongozi wakiwa madarakani bado wanawaogopa wazungu. Mtu ambaye yupo imara sana katika mambo haya ya kutokuwa mnyonge ni Mugabe. Kwa hiyo kitendo alichokifanya Rais ameonesha wazi kwamba kiongozi wa nchi anaweza bila uoga kutetea masilahi ya uchumi wa nchi yake.

“Watu wanapaswa kulitazama kwa namna hiyo. Pia aneonesha dhamira ya kuwa na uchumi wa viwanda, hii yote inaonesha ni namna gani analinda masilahi ya nchi kwa mfano hapa Afrika nchi ambayo inanufaika kwa madini ni Botswana.

“Nchi hiyo imekuwa mfano wa kuigwa kwani kinachofanya mwekezaji awekeze ni rasilimali yako, ukiandaa andiko likaonesha mradi ni mzuri, uwekezaji huo utatokana na rasilimali yako. Hapo ndipo tumekuwa tukikosea kwamba mwenye teknolojia anatakiwa kuwa na nguvu kuliko mwenye rasilimali. Afrika tumeneemesha nchi matajiri, tumelegeza kamba, wamechota na mwisho wamekuwa wakitupatia misaada ambayo ni zile rasilimali zetu,” alisema.

KUKANDAMIZA DEMOKRASIA

Pamoja na mambo mengine, Dk. Mzindakaya aliwakosoa wanasiasa wanaosema Serikali ya awamu ya tano inakandamiza demokrasia kwa sababu tu ya kutoruhusu mikutano ya hadhara.

Alisema anayetakiwa kutembea nchi nzima kushukuru wananchi ni Rais huku wabunge wakiwashukuru wananchi kwenye majimbo yao.

“Sasa unataka kuzunguka nchi nzima ukamshukuru nani? haina maana!. Kwa mfano Hillary Clintoni alishindwa urais Marekani mwaka jana na hadi sasa hajazungumza kushukuru waliompigia kura. Si lazima uzunguke nchi nzima, unaweza kuzungumza kwenye televisheni kwamba nashukuru kwa kunipa kura japo hazikutosha ila nawashukuru.

“Una haja gani ya kutembea na kufanya maandamano? Pia vyama vyetu vina wabunge ambao wataenda kwa niaba ya chama kuwashukuru. Kwa mfano mimi sasa si mbunge wa Kwera, sasa nitaenda kuitisha mkutano ili nizungumzie nini wakati anayewakilisha watu keshapatikana? Haya ni mazoea ndio maana watu wanalalamika.

“Je, haya mazoea ni ya kisheria? Kwamba watu lazima watembee nchi nzima kuhutubia? Katika Uchaguzi mkuu uliopita vyama vya upinzani vimepata viti vingi kuliko wakati wowote. Hawakuzurura… kazi waliyofanya bungeni wamefanya vizuri kuliko wabunge wa CCM. Lazima wabunge wafanye kazi ya ziada bungeni. Huwezi kusema wanasiasa kutotembea ni kugandamiza demokrasia si kweli.

WANASIASA WANAFIKI

Dk. Mzindakaya amewataka wanasiasa kuacha unafiki kwa kukosoa uongozi uliopita bila sababu.

Alisema wanasiasa hao huponda serikali zilizopita pindi wanapotakiwa kutoa maoni yao kuhusu serikali ya sasa na serikali zilizotangulia.

Dk. Mzindakaya ambaye alihudumu kwenye nafasi ya ubunge kwa miaka 44, alisema mara nyingi wanasiasa hufanya makosa kulinganisha serikali iliyopita na ya sasa.

“Si sawa, kila serikali iliyokuwa madarakani imeingia kwa wakati wake na kufanya majukumu yake. Mambo ya uongozi na mabadiliko katika serikali ni kama kijiti, utapata shida kuanza kulinganisha kwani unatakiwa kuanzia pale Rais alipoanza.

“Ila niseme wazi kuwa kuna baadhi ya wanasiasa ni wanafiki, kwa sababu baadhi yao wamefanya kazi na marais wa awamu ya tatu au ya nne, wanapotoa maoni yao wanaponda serikali zilizotangulia, huo ni unafiki, kwa sababu ukimponda aliyetangalia wakati alifanya kazi kwa muda wake ni jambo ambalo halina maana.

“Kila kiongozi apewe sifa yake kulingana na kazi alizozifanya. Kwa mfano mimi nimefanya kazi na Rais wa awamu ya kwanza na ya pili, awamu ya tatu na ya nne nilikuwa mbunge tu. Siwezi kuanza kuponda awamu hizo nilizofanya nazo kazi,” alisema.

Aidha, alisema licha ya Rais John Magufuli kuanza vizuri tangu alipoingia madarakani, lakini hatakiwi kupimwa kwa matukio.

“Tunapaswa tumpime kwa dhamira na uzalendo. Hicho ndicho kipimo cha kwanza kwamba kweli rais huyu amedhamiria na ana uzalendo na anapenda kuona mafanikio ya maendeleo kwa taifa lake. Dhamira na nia ya dhati anayo katika kuhakikisha Taifa linasonga mbele,” alisema.

TUKUBALI MABADILIKO

Aidha, mwanasiasa huyo alisema ni vizuri kila mwanasiasa kukubali mabadiliko kwa sababu kila uongozi hauwezi kuwa sawa na uongozi uliopita.

“Naona wananchi wameshakubali lakini wanasiasa bado tunafikiria kulinganisha, hiyo ndio kasoro, lazima tukubali kwamba kwa sasa Rais wa Tanzania ni Magufuli. Lazima watu waanze kuzoea mabadiliko.”

CCM HAIENDESHWA KWA MATAMKO

Licha ya kufurahia mabadiliko ya kimfumo na kiuongozi yaliyofanywa ndani ya CCM, Dk. Mzindakaya alisema hakubaliani na kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa wa chama hicho, Humphrey Polepole kwamba wabunge na madiwani watakaopitishwa kuwania nafasi hizo katika Uchaguzi Mkuu 2020 ni wale ambao ni wakaazi wa maeneo wanayogombea.

“Sikubaliani naye kabisa, lakini niseme haifai watendaji wa chama wakaendesha chama kwa matamko. CCM haiendeshwi kwa matamko, inaendeshwa kwa vikao. Lazima mambo yote yanayohusu sera na maamuzi ya kikatiba yatokane na vikao. Haiwezekani mtu anasimama mwenyewe anasema ooh lazima mgombea ubunge awe anatoka hapohapo. Sio sawa lakini kama chama kimekutana ni uamuzi wa chama ni sawa. Kwamba watu kuendesha chama kwa matamko si sawa kwa sababu kinatokana na watu lazima mambo yanayotokana na watu ndio yatoke hadharani.

“Pili ubunge si uenyekiti wa kijiji, watu wa Kagera wanakaa, Mwanza au Dar es Salaam wamekwenda kule kujifunza, sasa ukisema wagombea lazima watokane hapohapo, mnalocalize leadership. Tunataka kupanua mawazo, yaani tunataka watu wote wa kuongoza nchi hii, warudi kijijini Sumbawanga kwenye jimbo? mtawapata wapi hawa! Tuna wasomi wametoka Rukwa wapo mikoa mingine, wengine wapo masomoni Uingereza wamekwenda kujifunza eti wakirudi ooh wewe hukai hapa! Hii ni kasoro. Lazima tukubali kutumia watoto wetu waliotoka katika maeneo yetu kwa sababu wamesoma hivyo wana haki ya kurudi katika maeneo yao,” alisema.

Alisema mabadiliko ambayo yamefanywa ndani ya chama hicho ni moja ya mambo ambayo tangu zamani alikuwa akiyaamini.

“Tulifika mahali viongozi wetu wanaccm au watu ndani ya chama, wanakuwa na tamaa sana. Mtu mmoja anataka kujilimbikizia vyeo viwili, vitatu, vine. Hivi hakuna watu! Sisi wakati huo tulipoingia bungeni mwaka 1965 watu waliosoma chuo kikuu wakati huo Makerere, walikuwa wanne tu mkoa wote wa Rukwa, leo Rukwa ina madaktari, maprofesa sasa kwanini watu wachache wanataka kuendelea kukumbatia vyeo ndani ya chama?

“Pili nilikuwa mjumbe wa Halmashauri kuu kwa miaka 15 nikiwakilisha mkoa, hapo katikati ikaamuliwa kuwa kila wilaya ya chama iwe na mjumbe wa halmashauri. Kwa hiyo maana ya mjumbe wa halmashauri kuu ikapotea.

“Alafu kuwa na wajumbe halmashauri zaidi 300 mnazungumza nini! Ndio maana siri za chama hazikuweza kulindwa tena. Wakati wetu sisi tulikuwa tukienda kwenye kikao kujadili majina ya watu au mambo ambayo ni siri inakuwa siri kweli. Kwa sababu tulikuwa wajumbe wa mikoa tu na wale wanaochaguliwa kitaifa, wanaoteliwa na rais.

“Sasa ilifika wakati halmashauri kuu ya taifa ni bunge lingine kwa sababu mbunge anakuwa mjumbe tena wa halmashauri kuu. Katika wilaya ambaye yeye ni mbunge wa jimbo anakuwa mjumbe wa halmashauri kuu, maana yake nini? Kwa hiyo chama kilishaanza kupoteza hadhi ya vikao. Hadhi ya vikao ni kulinda siri,” alisema.

NAMWOMBEA LISSU APONE

Licha ya makada wengi wa CCM kukwepa kuzungumzia tukio la kujeruhiwa kwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kwa upande wake Dk. Mzindakaya alisema anamuombea mwanasheria huyo wa Chadema apone haraka.

“Suala la uhalifu sio kwa wabunge tu, ni kwamba Tanzania imekuwa nchi ya amani kwa muda hivyo serikali yetu inatakiwa iendee kuhakikisha amani na utulivu kwa raia wote.

“Lissu ni mbunge lakini pia ni raia wa nchi. Kinachotakiwa ni juhudi za serikali kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi ya mfano. Pili kitendo cha kumshambulia Lissu hakiwezi kuungwa mkono na mtu yeyote mwenye akili timamu, ni kitendo kibaya na mimi miongoni mwa wanaomuombea apone na ninafurahi kama Lissu anaendelea vizuri,” alisema.

Mwandishi wa RAI, Gabriel Mushi (kushoto) akifanya mahojiano na Dk. Mzindakaya

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.