WAANGALIZI WA KIMATAIFA NI WAVURUGAJI WA CHAGUZI NYINGI AFRIKA

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI MAALUM

TANGU zilipojipatia uhuru nchi za Bara la Afrika, zimekuwa zikilazimishwa kukubali kwamba uhalali wa chaguzi zao zitatafsiriwa kuwa huru na haki iwapo tu zitaonekana kuangaliwa na kupigiwa mhuri na watazamaji wa nje ambao huchaguliwa kwa njia zisizokuwa wazi.

Wajumbe wa makundi haya ya watazamaji mara nyingi huwa hawana uelewa kuhusu hali ya idadi ya watu nchini na ya kisiasa kuhusiana na chaguzi hizo.

Hata hivyo, tafiti zinaonyesha kwamba uelewa huu si kitu muhimu sana. Na ni nadra sana kwa nchi husika kuwapinga iwapo watawala watatuhumiwa kwa kukiuka misingi ya demokrasia na/au kuficha kasoro na hujuma zinazokuwapo wakati wa uchaguzi.

Nchi ambazo huwakubali watazamaji hawa kwa uchangamfu mkubwa, hufanya hivyo kwa kufahamu kabla matokeo ya ripoti zao ambazo watayatangaza. Mara nyingi huwa hawatilii maanani habari zozote kuhusu kipi hasa kilichotokea kwa undani katika chaguzi hizo.

Na ripoti zao huwa za kupotosha na mara nyingi huunga mkono matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa na yanayopendelea maswahiba zao ambao hutangazwa kuwa washindi. Aidha, baadhi ya ripoti hizo huwa chanzo cha mifarakano ndani ya nchi husika.

Sababu ya hali hii inajulikana wazi. Inafahamika wazi kwamba hakuna kundi la watazamaji kutoka nje wanaoruhusiwa kuingia nchini na kufanya kazi na kutayarisha ripoti zao bila ya mamlaka za nchi husika kwanza kuwakubali na hasa namna walivyoteuliwa na kufahamu imani zao za kisiasa.

Chukua kwa mfano uchaguzi wa Kenya wa hivi karibuni. Kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo, mtaalamu bingwa wa masuala ya kompyuta katika Tume ya Uchaguzi (IEBC) aliuawa kikatili.

Wahusika wa mauaji hayo bado hawajajulikana, achilia mbali kutiwa mbaroni, ingawa wengi wanashuku ni mawakala wa kundi moja la siasa ambalo lilitarajiwa kunufaika na matokeo ya uchaguzi huo.

Na baada ya kutangazwa kwa matokeo, watazamaji kutoka nje ambao walitarajiwa kuchunguza kwa undani mchakato mzima wa uchaguzi, walitangaza maoni yao kwamba uchaguzi ule ulifanyika kwa uhuru na haki na hivyo matokeo yanapaswa kukubaliwa.

Ripoti zao zilishindwa kutilia maanani mapungufu mengi ya zoezi zima la uchaguzi kama yalivyoripotiwa na vyama vya upinzani pamoja na wale watazamaji huru wa ndani.

Hata hivyo, Mahakama ya Juu (Supreme Court) ilitofautiana sana na ripoti za makundi ya watazamaji kutoka nje.

Majaji wa Mahakama hiyo walifahamu vyema namna ya mifumo ya kutangaza matokeo ilivyokuwa na kwamba ilikuwa rahisi sana kuiingilia.

Kutokana na hali hii, hakuna shaka kwamba majaji wa Mahakama ya Juu ambao kutopendelea kwao na ujasiri walioonyesha umechukuliwa kuwa ni nadra sana kutokea barani Afrika na hivyo uamuzi wao ni halali zaidi kuliko ule wa watazamaji wa kutoka nje.

Udhaifu unaotokana katika kutegemea sana watu wa nje katika ‘kuhukumu’ chaguzi za Afrika unathibitishwa baada ya kujulikana kiongozi mmoja wa kundi la watazamaji kutoka nje alikuwa ni swahiba wa rais Uhuru Kenyatta.

Na mtu akiweza kuangalia nyuma, hili lisingeshangaza wengi ambao wanayafahamu mambo haya. Hivi karibuni, jarida moja la Uingereza la Private Eye Septemba 8 liliandika:

“Uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Kenya wiki iliyopita kwamba uchaguzi wa urais haukuwa halali kutokana ma ukiukwaji wa kanuni ni tukio moja miongoni mwa matukio kadhaa hivi karibuni yaliyomwaibisha Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth), Baroness Scotland.

Baroness Scotland alimteua Rais wa zamani wa Ghana, John Mahama, kuongoza kundi la watazamaji kutoka Jumuiya hiyo kwenda Kenya na kwa niaba ya Jumuiya hiyo alitangaza kwamba uchaguzi ulikuwa halali, huru na haki.

Mahama hakuwa chaguo sahihi kutokana na uswahiba wake wa karibu ma mmoja wa wagombea urais, Uhuru Kenyatta. Ni mwaka jana tu ambapo Uhuru alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za uhuru wa Ghana.

Na ndiyo maana bila shaka Kenyatta alipata mshtuko mkubwa pale Mahakama ya Juu ilipoonekana kutupilia mbali ripoti za watazamaji wa nje.

Yeye na wafuasi wake walitegemea ripoti za watazamaji kuwa nguzo ambazo zingewaongoza Majaji kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa mbele yao na upinzani ya kupinga matokeo ya uchaguzi.

Udhaifu unaotokana katika kutegemea sana watu wa nje katika ‘kuhukumu’ chaguzi za Afrika unathibitishwa baada ya kujulikana kiongozi mmoja wa kundi la watazamaji kutoka nje alikuwa ni swahiba wa rais Uhuru Kenyatta.

Kiongozi wa Kundi la Watazamaji wa uchaguzi wa Kenya kutoka Jumuiya ya Madola na Rais wa zamani wa Ghana, John Mahama.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.