Mjadala hukumu ya kifo moto - 3

Rai - - MBELE -

Nimekuwa nikishawishi Watanzania kusanifu na kujenga utamaduni wa kujadiliana kwa uwazi, kwa upendo, kwa staha, kwa ujasiri masuala yenye masilahikwaTaifanikiamini kuwa jamii inayojadiliana na kushindanisha hoja ni jamii hai maana katika msuguano wa ushindani wa hoja ndipo huchipuka

cheche za maendeleo. Jamii isiyojadiliana mambo yao ni mfu wasioweza kutofautishwa na wanyama hayawani ambao huendeshwa kwa hisia-silika maana hawakujaliwa uwezo wa kufikiri kama binadamu. Je, tujiruhusu kuwa wanyama hayawani? Hapana, maana asili inakataa na hata uumbaji unagoma. Endelea.

Kaiza Musa (70) anatetea hukumu ya kifo lakini ukisoma jumbe zake (ambazo sikuona sababu za kuziandika hapa kuheshimu miiko ya taaluma) akijificha chini ya mbawa za sheria za Kiislamu, Sharia katika aya ya 108 Surat Bakara inayoelekeza hukumu ya kifo. Hii ni katika kujibu hoja yangu kuwa hakuna dini inayoshadadia mtu kuua maana hata wale vijana waliolipua mabomu na kuua watu nchini Uingereza wakidai kutetea Uislamu na Waislamu bado viongozi waandamizi wa Uislamu waliwakana na kueleza dunia kuwa maana ya Uislamu ni Amani na kwamba wanaotumia jina la Uislamu kuua watu wanakwenda kinyume na Imani ya dini hiyo.

Lakini pia tulikuwa tukijadili kauli ya Jeshi la Polisi inapokuwa imeua watuhumiwa wa ujambazi ambapo utasikia, “tumefanikiwa kuua majambazi watatu…na wengine kutoroka.” Kwamba kwa kuua watu ni mafanikio. Nani anayewahukumu/ anayethibitisha watu hawa kuwa ni majambazi tofauti na mahakama? Kwa nini jambazi auawe tu? Hoja hapa ni kutetea uhai wa watu wawe ni wema au wahalifu ili kutafuta adhabu inayoweza kuwafanya wahalifu nao kuwa raia wema waendelee kuishi ili ile dhana ya “ni Mungu pekee mwenye kuamua nani afe na lini” iweze kuwa na mashiko. Kwa muktadha huu Polisi anavaa madaraka ya Mungu?

Dk. Kasala wa TEC akijitosa katika mjadala huu kutetea hoja na kampeni ya Papa Francis ambapo anaanza kwa kulalamika; “tatizo mijadala kama hii mara nyingi huishia sakafuni tu, haiendelei, huishia magazetini na hasa katika kipindi kama hiki sidhani kama unaweza kusikilizwa na watunga sera ambao ajenda yao kwa sasa si kujadili mambo kama haya.”

Dk. Kasala ambaye amemkosoa mwandishi katika baadhi ya maneno kutoka Waraka wa Kwaresma 2018 kimantiki anaendelea, “kwangu sidhani kama mjadala ungekuwa ni kufutwa kwa sheria ya hukumu ya kifo au la maana unaweza kufuta sheria hiyo lakini vitendo vya mauaji vikaendelea tu kwa hiyo nadhani kama ni mjadala basi ungejikita nini hasa kinachopelekea watu kuua na hivyo kukutana na hukumu ya kifo?” Dk. Kasala anaamini kuwa kama jamii tukizuia vitendo vya mauaji basi hata hukumu ya kifo haitokuwa na maana tena kwa sababu hakutakuwa na wakosaji na uuaji watakaohukumiwa kunyongwa.

Dk. Kasala anarejea andiko la Mwanzo 4:9 (Biblia) lililotolewa katika Waraka wa TEC wa Kwaresma mwaka huu ikitaka kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake kuzuia vifo. Katika andiko hilo tunasoma habari ya Kaini kumuua nduguye Habili kabla ya Mungu kumuuliza yuko wapi ndugu yako? Naye Kaini kujibu kwa kiburi, “Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” Dk. Kasala anataka kila mtu kumlinda mwenzake ili kuepusha vifo. Hata hivyo Dk. Kasala hajaeleza “mwenzangu” ana alama gani usoni ya kumtofautisha na watu wengine?.

Dk. Kasala amepanua mjadala zaidi anapotaka tujadili nini kinachofanya mtu amuue nduguye na kisha kukutana na adhabu ya kifo. Lakini mimi nimwongezee Dk. Kasala katika hoja yake kwamba wauaji/muuaji ni nani hasa? Kuna tofauti gani kati ya waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua Bilionea Msuya kwa kummiminia risasi na yule Afisa wa Serikali anayechukua fedha za mradi wa kuzuia vifo vya mama na mtoto na hivyo mama na mtoto kupoteza maisha kwa kukosa chandarua chenye dawa?

Kwa nini uchunguzi wa chanzo cha kifo cha aliyepigwa risasi uoneshe ni aliyefyatua risasi na hivyo anastahili kunyongwa lakini chanzo cha mtoto aliyekufa kwa malaria usioneshe ni yule Afisa wa Serikali aliyepindisha matumizi ya fedha za kununulia kinga ya kifo ambayo ni chandarua chenye dawa ya kumkinga mtoto na mjamzito dhidi mbu aina ya “anofelesi?”

Hivi tunaposema aliyeua kwa kumkatakata mapanga yule mtu mwenye ualbino kule Shinyanga alidhamiria hivyo anastahili hukumu ya kifo kwani fisadi anayepindisha matumizi ya fedha za umma hajui kwa wanakijiji kukosa maji wataugua magonjwa ya tumbo na mwisho watakufa? Anatofauti gani na muuaji wa kutia sumu ndani ya mto wa maji ya wanakijiji?

Hata hivyo Dk. Kasala anashangaza anapotaka tujikite kutafuta kwa nini watu waue wenzao hadi kutungiwa sheria ya kifo! Kama kiongozi wa kiroho Dk. Kasala hajui asili ya kifo ni laana? Je, Dk. Kasala hajui jukumu lake (viongozi wa dini) ni kuhubiri na kuwafundisha watu wote kuacha kuua wenzao ili sheria ya kunyongwa isiwepo tena?

Lakini Dk. Kasala anapohubiri waumini wake juu ya amri ya Mungu ya “usiue” je, amri hii inalenga watu gani hasa? Je, kanisa Katoliki litabariki muumini wake ambaye pia ni Rais kutia saini mtu kuuliwa? Mwenyewe amewahi kusema, “ninyi majaji kazi yenu ni kutoa hukumu lakini ikifika huku kwetu wanasiasa ni ngumu kweli.” Kauli inayoonesha uzito wa Rais Magufuli kutia saini waliohukumiwa kunyongwa na hivyo kutoa taswira kuwa anaweza kumaliza muda wake wa uongozi bila watu kunyongwa. Kama kuna ugumu huo kwa nini basi sheria hii isiondolewe tu?

Adhabu ya kuiba kuku ni kufungwa jela ili mwizi akiwa jela afanyishwe kazi za suruba kwa kipindi fulani ili atakaporudi uraiani basi awe mtu mwema, aogope kuiba na atumie nguvu zake katika ujenzi wa Taifa. Unajiuliza, tunapotoa adhabu ya kifo ni kwa namna gani adhabu hii inamsaidia muuaji kujirudi ilhali hatunaye tena? Lakini je, kama lengo ni kumuogopesha mwingine ambaye hajaua asiue kuogopa hukumu ya kifo ni kwa namna gani limefanikiwa? Mbona bado wauaji wamejaa tele vijijini na mitaani? Mbona matukio ya mauaji hayaishi? Kwa nini tusione adhabu hii imeshindwa kukidhi matakwa-lengwa? Je, muuaji akiambiwa arudie kuua anaweza kurudia? Kwa nini wahukumiwe kunyongwa?

Bado ninaamini kuwa Rais Magufuli ni kiongozi mwenye uwezo wa kuthubutu hata mambo magumu. Amethubutu kutoa elimu bure ameweza, amethubutu kufufua mradi wa ujenzi wa ufuaji umeme kwa kutumia maji ya mto Rufiji ameweza, amethubutu kujenga reli ya kati ameweza, amethubutu kuanzisha mahakama ya mafisadi ameweza, amethubutu kufufua shirika letu la ndege ameweza. Wito wetu ni kuthubutu pia kutamatishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya ambayo ndani yake kutakuwa na Ibara inayoondoa hukumu ya kifo. Safari ya Kaanani inaendelea! Karibu kwa mjadala.

Dk. Kasala ambaye amemkosoa mwandishi katika baadhi ya maneno kutoka Waraka wa Kwaresma 2018 kimantiki anaendelea, “kwangu sidhani kama mjadala ungekuwa ni kufutwa kwa sheria ya hukumu ya kifo au la maana unaweza kufuta sheria hiyo lakini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.