Mienendo hii ya walimu vijana ikomeshwe

Rai - - HABARI - NA HASSAN DAUDI

MWANADAMU ni zao la jamii yake. Wanasaikolojia wanaamini kuwa namna anavyotembea, anavyokula, anavyoamini, anavyovaa, anavyowasiliana, ni matokeo ya watu waliomzunguka.

Kwamba ukiacha sababu za kibaolojia, mazingira yana mchango mkubwa katika kuumba tabia tulizonazo. Mfano; asilimia kubwa ya waliozaliwa katika familia za Kiislamu au Kikiristo, huwa hawana sababu za moja kwa moja zilizowavuta katika imani hizo.

Wengi walijikuta wakiingia huko kwa sababu tu walipozaliwa waliwakuta wazazi au ndugu zao wengine wakiwa waumini wa dini hizo.

Kama hiyo haitoshi, hebu fikiria juu ya mtoto aliyezaliwa katika familia ya wafanyabiashara wa ‘gongo’ (pombe haramu ya kienyeji). Ukichunguza, utabaibini kuwa baada ya miaka kadhaa, wengi wao huingia katika ulevi au uuzaji wa pombe hiyo ni wachache sana humudu kukiepuka kikombe hicho.

Hivyo, ni wazi madai ya wanasaikolojia kuwa sehemu kubwa ya mienendo ya mwanadamu hutokana na watu waliomzunguka hayana shaka. Tabia ya mtu fulani unaweza kuitafisiri kutokana na jamii aliyotokea.

Ukiacha familia, shule ni moja kati ya taasisi muhimu katika kazi hiyo ya kumjenga mwanadamu. Hebu nikuulize, ni tabia ngapi ulizonazo leo hii ulijifunza shuleni? Walimu na wanafunzi wenzako walikuwa na mchango mkubwa kuumba baadhi ya mienendo uliyonayo sasa.

Nitakupa mfano katika hilo. Mwanafunzi anayevutiwa na kazi ya ualimu, ghafla anaweza kujikuta akijaribu kutembea na kuzungumza kama mwalimu wake wa Hisabati kwa sababu tu anakoshwa na ufundishaji wake, akitamani siku moja naye afikie uwezo alionao.

Isishangaze pia kusikia hata asilimia kubwa ya waandishi wa habari, waandisi, madaktari au wanasheria tunaowaona sasa walijikuta wameingia huko kutokana na ushawishi wa marafiki waliokutana nao shule.

Kwa maana hiyo, baada ya familia, jamii haina ujanja wa kukataa kwamba shule ni chombo kisichopaswa kupuuzwa katika kumtengeneza mwanadamu.

Hapa nchini, Serikali imekuwa ikilitambua hilo kwa kujaribu kuipa kipaumbele taalamu ya ualimu licha ya changamoto za hapa na pale. Walau juhudi zinaonekana.

Moja ya mapinduzi ya kuvutia katika taaluma hiyo ni uwepo wa walimu wengi wenye umri mdogo. Binafsi nimekuwa nikipendezwa na hilo, japo bado nautambua na kuuthamini mchango wa walimu wakongwe.

Nina sababu za kisaikolojia inayonifanya nivutiwe na uwepo wa walimu vijana katika shule zetu. Ukweli ni kwamba inaongeza hamasa (motivation) kwa wanafunzi wanaotamani kufikia mafanikio wakiwa katika umri mdogo.

Nikirejea katika kuyapa nafasi macho yangu kuona, nikiri wazi kuwa licha ya mvuto walio nao kwangu, lakini zipo aina za mavazi na mitindo ya nywele kwa walimu vijana katika shule nyingi, hasa za sekondari, ni changamoto kubwa isiyopaswa kufumbiwa macho.

Nikianza na walimu wa kike, wamekuwa kichefuchefu mbele ya jamii kwa mavazi mafupi au yanayobana, ambayo kwa kiasi kikubwa huyaanika maungo yao. Je, mwanafunzi wa kike anayevutiwa na mwalimu huyo anaandaliwa kuwa mtu wa aina gani katika jamii?

Hebu tujiulize, ikiwa tunapeleka watoto shule ili kuwaepusha na uhuni uliojaa mitaani, halafu anakutana na mwalimu wa aina hiyo, nini tofauti?

Walimu wa kiume nao ni tatizo linapokuja suala hilo la mavazi. Achana na suruali zao za kubana miguuni ‘model’, ambazo licha ya sasa kuonekana kuwa mtindo mpya, ukweli ni kwamba miaka michache iliyopita zilikuwa zikivaliwa na wanawake tu.

Lipo hili la kuingia darasani wakiwa wamevaa mlegezo (suruali chini ya makalio). Nimelishuhudia hilo mara nyingi na sina shaka kuwa hata wazazi wanaofika shuleni mara kwa mara kufuatilia maendeleo ya watoto wao wanaweza kukiri kama si kuniunga mkono kukemea upuuzi huo.

Aidha, walimu hao wamekuwa kituko zaidi katika mitindo yao ya nywele. Kama wafanyavyo vijana wenzao wa mitaani, nao wamekuwa wakinyoa staili za ajabu kana kwamba si watumishi wa umma, tena katika taaluma nyeti.

Mwisho, niulize, ni kweli kamati za shule haioni au zinafurahia uchafu huo? Kama jibu ni hapana, nini kimefanyika kukabiliana nao?

Niulize pia, kama kuna hatua wanazochukuliwa waalimu hao kwanini tatizo linaendelea na kuchafua taswira na maana halisi ya shule?

Mbali na mitindo ya mavazi, nywele na namna ya kujiremba kwao, lakini pia lipo suala la utoaji wa adhabu, kundi hili la waalimu vijana wao hawana maumivu ya uzazi nah ii huenda inasukumwa na wengi wao kutokuwa na familia.

Ukiwakuta wanachapa mwanafunzi, kamwe hawaangalii mahali sahihi na salama pa kuchapa, wanachapa kama wanaponda nyoka.

Nalisema hili kwa uhakika kwa sababu macho yangu yamepata kuyaona matukio ya namna hii mara kadhaa kwenye shule za msingi na Sekondari.

Na tukio la hivi karibuni ni kwenye shule ya Sekondari Maendeleo, iliyopo Nyakasangwe kata ya Wazo, wilaya ya Kinondoni, kwenye shule hii kuna baadhi ya waalimu vijana ni hatari zaidi ya magaidi. Wanachapa mwanafunzi bila huruma wala hofu ya Mungu. Ipo haja kwa Serikali na wasimamizi wa suala hili kulitazama jambo hili kwa umakini zaidi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.