Hama hama hii ya wanasiasa ni msukumo au mvuto?

Rai - - MAKALA - MUDHIHIR M. MUDHIHIR

NDANI ya mwaka huu wa 2018 medani ya siasa nchini mwetu imekumbwa na kishindo kikubwa cha hama hama ya wanasiasa kutoka kambi ya upinzani kwenda Chama Cha Mapinduzi. Tumeshuhudia viongozi wa kuchaguliwa wakiwemo wabunge, madiwani na viongozi wa serikali za vijiji na mitaa wakijiuzulu nafasi zao na kujiunga CCM.

Sisemi kuwa hama hana hii ni kadhia yeye kustaajabisha kwa sababu utamaduni huu si mgeni hapa kwetu. Hapana shaka kuwa tunakumbuka vizuri yaliyojitokeza wakati wa vuguvugu la kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Wanasiasa waandamizi kutoka CCM pamoja na maelfu ya washabiki wao walihamia kambi ya upinzani kwa kasi iliyopewa jina la “mafuriko.”

Mafuriko yale ya mwaka 2015 yaliacha mambo makubwa mawili ya kukumbukwa. Mosi, nguvu ya kasi ya mafuriko yale viliitingisha CCM hadi ikatingishika kwelikweli. Mipasuko iliyokuwa bayana ilijidhihirisha ndani ya CCM. Baadhi ya viongozi waandamizi na wanachama waliamua kufa na mtu wao badala ya kufa na chama chao. Bila ya shaka CCM na vyama vingine vilijifunza juu ya madhara ya kumtanguliza mtu mbele badala ya chama. Chama ni watu siyo mtu.

Jambo la pili kubwa lililoachwa na mafuriko yale ni muungwana kula matapishi yake. Aliyekuwa amechafuliwa vya kutosha kwa kurushiwa tope la ufisadi wa kunuka alisafishwa kwa sabuni na dodoki hadi akawa mpya kwa haiba na hulka. Wenye Kiswahili chao utawasikia wakisema kuwa msitu mpya na komba wapya. Na wazungu husema ni rahisi kumtoa dubu msituni lakini ni kazi ngumu kuutoa msitu ndani ya dubu.

Sasa kibao kimegeuka na mafuriko yamechukua mwelekeo mpya. Hivi sasa ni zamu ya wanasiasa kuhama kutoka upinzani kwenda CCM. Tukitoa “mahepe” ngoma ya wachawi, ngoma nyingine zote huwa na watazamaji. Sisi tunaitazama ngoma hii tunajiuliza maswali mengi kuhusiana na sababu ya ngoma hii na hatima yake. Wenye nyoyo za kujifariji husema kuwa ngoma ikirindima sana inakaribia kupasuka.

Tusiyoufahamu undani halisi wa ngoma hii ya hama hama tumeanza kujiuliza maswali ya kubuni na majawabu ya hisia. Baadhi yetu tumeanza kudhani na kuamini kwamba hawa wanaojiuzulu nyadhifa zao na kuhamia CCM si bure wananunuliwa. Mtusamehe bure! Na miongoni mwetu tunasema, hivyo na wale wa mafuriko ya 2015 walinunuliwa pia? Na hawa pia watusamehe bure!

Na waungwana wanaowamiliki wachezaji wa ngoma hubobokwa maneno. Wanasema kwa uchungu mkubwa kuwa watu wao wananunuliwa kwa fedha na wengine kwa ahadi ya kupewa uteuzi wa nafasi za uongozi. Ikiwa madai haya yana ukweli basi kwa hakika isiyo shaka hili ni jambo baya. Kwa kuwa ubaya hauna kwao, tuseme pia kuwa iwapo ndani ya mafuriko ya 2015 wapo ambao waliahidiwa nafasi jambo hili nalo ni baya.

Ukisimama katikati ya makundi haya mawili utagundua kuwa mafuriko ya mwaka 2015 na yanayotokea 2018 ni yale yale. Ikiwa ipo tofauti basi ni tofauti ya viwango na kasi. Husemwa kuwa kwenye mpambano kelele haziepukiki na ukimsikia mwanaume anapiga ukelele ujue ameshikwa pabaya. Ndege wote wakilia hao wanaimba, lakini akilia bundi ni uchuro.

Baada ya kuudurusu muhtasari wa yanayojiri na yanayozunguka ndani ya vichwa vyetu kuhusiana na hama hama ya wanasiasa wetu baina ya chama tawala na kambi ya upinzani, pengine tungependa kwenda mbele zaidi kufahamu kiini cha kadhia hii. Hatua hii ni muhimu kwani tatizo ni kama kufuli na kulitambua tatizo ni kama kuupata ufunguo wa kufuli hiyo.

Mwanadamu kuhama kutoka eneo moja kwenda eneo jingine ni jambo la kawaida. Katika mazingira ya kawaida zipo sababu kuu mbili zinazoweza kusababisha mtu kuhama. Sababu hizi zinaweza kuwa msukumo unaokuondosha ulipo au mvuto unaokuvutia unakohamia. Yaani yanaweza kuwepo yanayokukera hapo ulipo yanayokusukuma utoke, au yapo yanayokuvutia eneo lingine yakakuvutia uyaendee.

Nguvu ya msukumo na mvuto zinafahamika na vyama vyote. Kambi ya upinzani chini ya mwavuli wa UKAWA katika kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015 ilijinadi kwa kauli mbiu ya MABADILIKO. Kaulimbiu hii ilitarajiwa kuleta mvuto kwao, lakini watani wao wakawazidi kete kwa kuwageuzia kibao kuwa vyama visivyokuwa na utamaduni wa mabadiliko havina uwezo wa kuunda serikali yenye kuleta mabadiliko.

Nimeanza na suala la mabadiliko kwa kuamini kwamba mabadiliko ya uongozi na ya kisera ni msingi muhimu wa kujenga na kuimarisha chama chochote cha siasa. Anayewania uongozi anaweza kujiunga na chama chochote cha siasa ilimradi anaona ndoto zake zitatimia. Na vivyo hivyo anaweza akaondoka muda wowote akiona matarajio yake yamo hatarini. Bali wapiga kura daima wataungana na chama chenye matumaini na matokeo.

Chama chochote cha siasa chenye dalili hata zisizo bayana za kukumbatia ujimbo, ukabila au udini hakitakuwa na nguvu ya kitaifa. Chama chochote cha kisiasa ambacho nguvu yake ni mtu mmoja au kikundi cha wateule hakitakuwa na wanachama wenye nidhamu ya kweli ya chama. Chama cha aina hii hakiwezi kuhimili misukosuko ya ndani wala ya nje.

Hivi ni baadhi ya viashiria ambavyo hutegeneza nguvu za msukumo zinazoweza kumhamisha mwanachama wa kawaida au kiongozi kutoka kwenye chama chake. Na hivi ni viashiria ambavyo kidogo huitafuna nguvu ya chama cha siasa hadi zikapoteza haiba yake. Haya tumeyashuhudia kuanzia uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini mwetu mwaka 1995. Vyama vilivyokuwa tishio leo ni wasindikizaji.

Mvuto ndani ya chama cha siasa unatengenezwa na muundo wa uongozi, mfumo wa uamuzi, kusoma nyakati, sera na matokeo. Lazima kuwepo na utaratibu wa viogozi kupokezana vijiti vya uongozi. Lazima uamuzi wa chama utokane na vikao vya chama. Lazima chama kisome alama za nyakati ili kujua matakwa ya wananchi. Lazima chama kiwe na sera zenye kuleta matokeo.

Waliyohamia CCM wanadai kuwa wanakunwa mno na juhudi za serikali ya CCM ya awamu ya tano. Wanadai kuwa huko watokako maneno na vitendo havioani. Kwa namna yoyote iwayo tunaihitaji demokrasia ya vyama vingi hivyo wanasiasa nyote na hasa viongozi wakuu jengeni vyama imara.

Mvuto ndani ya chama cha siasa unatengenezwa na muundo wa uongozi, mfumo wa uamuzi, kusoma nyakati, sera na matokeo. Lazima kuwepo na utaratibu wa viogozi kupokezana vijiti vya uongozi. Lazima uamuzi wa chama utokane na vikao vya chama. Lazima chama kisome alama za nyakati ili kujua matakwa ya wananchi. Lazima chama kiwe na sera zenye kuleta matokeo.

0784-307271.

Mwita Waitara (kushoto) akifurahia jambo na Humphrey Polepole

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.