Djuma aiweka rehani Simba

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

AMA kweli la Kuvunda halina ubani. Kuna kila dalili sasa ya maisha ya Kocha Msaidizi wa timu ya Simba, Masoud Djuma kuhesabika ndani ya klabu hiyo.

Hali imechafuka na hakuna namna tena kwani tayari harufu imeanza kuvunda, licha ya kuwepo wa jitihada kubwa za kutaka kuzuia isitoke au isisambae nje, lakini nani awezaye kuizuia?

Siku chache tu toka kuanza kwa Ligi Kuu nya Tanzania Bara klabu ya Simba inaingia katika msukosuko mkubwa wa kutikisika kwa benchi lao la ufundi. Si kitu kipya sana kwani kwa lugha nyepesi unaweza kusema ni suala lile lile tu mabosi wa idara hiyo nyeti hawaelewani.

Ndiyo, Djuma haelewani na bosi wake, Kocha Mkuu, Mbelgiji, Patrick Aussens. Kawaida vikombe vikikaa pamoja havikosi kugongana lakini hili linaweza kuwa na ukakasi kidogo kutokana na ukweli kuwa sababu ni zile zile na mhusika mkuu ni yule yule.

Fununu za kutoelewana kwa makocha hao wawili zilianza kusikika siku chache toka kikosi cha timu hiyo kirejee nchini kutoka kambi ya Uturuki, ni kama vile wengi waliamini lingekuwa ni tatizo la mpito na mambo yangerejea katika mpangilio wake lakini imekuwa ni kinyume.

Si siri tena maelewano kati ya Patrick na Djuma si mazuri tena kufuatia mbelgiji huyo kudai msaidizi wake amekuwa akifanya ‘fitna’ za kumkwamisha ili aonekani hafai na yeye kukabidhiwa mikoba. Lakini pia kuna madai ya kuwapa wachezaji maelekezo tofauti na anayoyatoa kocha mkuu.

Madai yakaenda mbali zaidi kuwa ametengeneza makundi ndani ya timu kwa kuwagawa wachezaji hali ambayo inatia hofu ya kufanya vibaya katika mechi zake za ligi zinazoendelea.

Baada ya hayo yote Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu hiyo iliyokutana mwishoni mwa wiki iliyopita haikusita kufikia maamuzi ya kuachana na mrundi huyo ili kuweka hali shwari ndani ya klabu na timu yao hasa wakiamini kocha huyo ndiyo tatizo.

Huenda kazi ya kumaliza hesabu kwa Djuma zilikuwa rahisi sana hasa kwa kuzingatia yaliyotokea kati yake na aliyekuwa bosi wake Pierre Lechantre ambaye toka aondoke hana hata miezi mitatu.

Patrick anapaswa kufahamu kuwa kuna vitu viwili amekuwa akiishi navyo kwa sasa ambapo mbele yake kuna kioo lakini kwa nyuma yake kuna kivuli.

Ukweli ni huu, sifa kubwa ya kioo huwa hakidanganyi. Kila kilichoripotiwa kwenye kurasa za mbele za magazeti, mashabiki wa Simba wanakisubiri uwanjani.

Katika mkataba wa kocha huyo na klabu ametakiwa kuhakikisha Simba inatetea taji la Ligi Kuu na kufuzu katika hatua ya makundi katika Michuano ya Ligi ya mabingwa barani Afrika.

Hapa kwa ubingwa wala hakuna shaka. Kwa kikosi alichokabidhiwa chini ya uwekezaji wa Bilionea Mohamed Dewji ‘MO’, hata kaka yangu Julio angebeba taji bila kupoteza mchezo wowote.

Shida kubwa ipo kwenye michuano ya Afrika. Ni kweli atakwenda kufuzu hatua ya makundi? Siyo kwamba hilo haliwezekani hapana ila mazingira ndiyo yanayotia shaka hiyo japo katika mpira lolote linawezekana.

Shaka ya kwanza inakuja pale

atakapotakiwa ndani ya kipindi kifupi kuleta mafanikio hayo kwa kikosi cha wachezaji ambao kwa asilimia 95 hukuwasajili.

Waswahili husema, ‘paka huwa hatoki jikoni mpaka siku atakapoungua mkia wake’. Patrick anatakiwa kuchunga sana mkia wake na hata kioo kilichowekwa mbele yake ni kikubwa mno hasa katika mazingira kama haya ya kutofautiana na msaidizi wake.

Nyuma ya kocha huyo kuna kivuli. Unafikiri ni cha nani? Hiki ni kivuli cha Mrundi Masoud Djuma.

Jean de La Fontaine, mwandishi wa vitabu wa Kifaransa katika Karne ya 17, aliwahi kusema: ‘Kadri Jua linavyozidi kuzama ndivyo kivuli kinavyozidi kuwa kikubwa’ hapa kuna kila dalili ya mbelbiji huyo kufeli.

Djuma ni kivuli cha jioni nyuma ya Patrick. Awali alianza kukiona kama ni kidogo, lakini sasa ukubwa wake ameanza kuubaini na jua litakapoanza kuzama atagundua mengi zaidi ya haya. Hapa maamuzi magumu yanahitajika.

Alikuwepo Mfaransa Pierre Lechantre. Huyu ndiye aliyekuwa kocha mkuu kabla ya ujio wa Patrick na kufanikiwa kudumu kwa takribani miezi mitano tu.

Ujio wa Lechantre ulikuwa kama mbelgiji huyo alivyotua kwa mbwembwe nyingi tu achilia mbali matarajio lukuki toka kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo. Alitamba kama anavyofanya huyu na hata kutoa mikakati na mipango.

Lakini unajua kilichofuata? Miezi sita baada ya ahadi yake ya kutaka kuifanya Simba kuwa timu tishio Afrika, alibeba mabegi yake na kurudi kwao.

Huyo ni Lechantre. Kwa akili ya kawaida kabisa, wasifu wake ni mkubwa mara mbili kuliko Patrick Aussems.

Ukimzungumzia Lechantre unamtazama mtu aliyewahi kuwa kocha bora Afrika mwaka 2000. Tunamzungumzia kocha aliyebeba taji la AFCON akiwa na Cameroon.

Huyu alichemka hapa Simba! Sina nia ya kutabiri mwisho mbaya utakavyokuwa kwa mbelgiji huyo ila lengo hapa ni kutaka kumtahadharisha mbelgiji huyo juu ya kivuli cha Djuma ambaye tayari ana kundi kubwa la mashabiki wa Simba wanaomkubali.

Changamoto kubwa anazoweza kukutana nazo kocha huyu mpya ni kukubalika kwa Djuma na mashabiki wa klabu hiyo. Ukiondoa Haji Manara, mrundi huyo ndiye mwanadamu anayependwa sana na mashabiki wa Simba, kifupi naweza kusema anakubalika mno.

Na hili halikutokea kwa bahati mbaya. Alifanya kazi kubwa mno. Ni yeye aliyeichukua Simba ya ‘ hovyo’ chini ya Joseph Omog na kuirejesha Simba ya burudani.

Nieleweke. Tofauti ya Simba ya Omog na Djuma ilikuwa si kwenye kupata ushindi, bali mbinu za kuutafuta huo ushindi. Mpaka leo mashabiki wa Simba wanaikumbuka Simba iliyoichapa Singida United ya Mdachi Hans van der Pluijm mabao 4-0. Simba bora kabisa.

Bahati mbaya ya Masoud haaminiki na viongozi wake. Ndio ukweli huu. Akiwa njiani kuijenga zaidi Simba, akashushwa Lechantre na msaidizi wake na masiha yakaendelea.

Kwa picha ya haraka, Lechantre hakumtazama Djuma kama tatizo. Na hakumtazama kwa sababu hakujua misingi iliyojengwa na Djuma kabla.

Akaichukua timu na kuanza kuweka mipango yake. Bahati mbaya, Simba ikaendelea kushinda, lakini ikarudi kulekule kwa Omog. Ushindi wa ‘Mungu saidia saidia’.

Jua lilipoanza kuondoka kwa Lechantre, Djuma akawa mkubwa tena. akaibuka na kuwapa kiburi viongozi kumkabidhi timu, ikiwa katikati ya mashindano kule Nakuru, Kenya.

Djuma akarudi kuwa bosi mkuu. Bosi mwenye sauti ya nani acheze na nini kifanyike. Uliona kilichotokea? Akiwa na kikosi kilichowakosa Okwi na Bocco, aliipeleka timu mpaka fainali. Wakapoteza kwa Gor Mahia.

Wiki chache baadaye, akiwa na kikosi kilichowakosa zaidi ya wachezaji nane wa kikosi cha kwanza, Djuma akaipelekea Simba kucheza fainali ya Kombe la Kagame. Huyu ndiye Masoud Djuma na ukubwa wake nyuma ya kivuli cha Patrick Aussems.

Vyovyote atakavyofanya Patrick Aussems mbele ya kioo chake, kama hatafanikiwa kukifunika kivuli cha Djuma, tutakutana naye Uwanja wa Ndege kumsindikiza kwao.

Yote kwa yote kwa upande wa viongozi Simba kama kweli wana dhamira ya timu yao kufika mbali katika mashindano yote inayoshiriki msimu huu inapaswa kuliangalia suala la mgogoro wa makocha wake kwa jicho la tatu kwani ni sawa na kusema kwasasa Djuma ameiweka rehani timu hiyo.

Djuma

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.