Serikali yawasha ‘moto’ UDSM

Mtandao wa wanaohusishwa wasakwa Viongozi watakiwa kutoa maelezo ya kina

Rai - - MBELE - NA GABRIEL MUSHI

SERIKALI imewasha moto wenye nia ya kuwasulubu watu wote waliohusika na upotevu wa mamilioni ya fedha za ada za baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM).RAI linaripoti.

Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti kuwapo kwa upotevu wa mamilioni ya ada za wanafunzi wa msimu wa masomo ulioanza mwezi April, 2018, ndani ya chuo hicho na kuelezwa kuwa uchunguzi wa suala hilo unaendelea.

Fedha zinazodaiwa kupotea zililipwa kwenye benki mbalimbali nchini na wanafunzi hao, lakini taarifa za malipo hayo hazionekani kwenye mitandao halali ya chuo hicho, huku ikibainishwa kuwa wanafunzi wote walionusurika kukosa mitihani kwa madai ya kutolipa ada wanavyo vithibitisho vyote vyenye kuonesha uhalali wa malipo yao.

Kutokana na kuripotiwa kwa taarifa hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeibuka na kutaka kupatiwa maelezo ya kina juu ya sakata hilo, ambalo linatajwa kukifedhehesha chuo hicho chenye heshima ya juu ndani na nje ya nchi.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Wiliam Ole Nasha (pichani) amesema wote waliofanya mchezo huo hawatobaki salama.

Akizungumza na RAI kwa njia ya simu, Ole Nasha alisema wizara imesikia changamoto hiyo lakini pia imepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho.

Alisema kutokana na hali hiyo tayari wizara imeauagiza uongozi wa chuo hicho kuwapatia kwa maandishi kwa kina kuhusu kilichotokea hadi fedha hizo zikapotea.

Alisema wameagiza maelezo yatakayotolewa na chuo hicho yawasilishwe ndani ya wiki hii ili hatua stahiki zianze kuchukuliwa haraka.

“Kimsingi ifahamike kwamba kama kuna michezo imechezwa, aidha ubadhirifu au wizi hakuna mtu yeyote aliyefanya hayo na akabaki salama, lazima tutachukua hatua. Katika serikali ya awamu ya tano huwezi kufanya michezo ya wizi ukabaki salama.

“Nina wahakikishia wanafunzi kuwa kama kuna miongoni mwao watakuwa wamedhurika na maamuzi mabovu, ujanja au wizi wa watu wengine wao hawatadhurika, kama wapo ambao nao watakuwa wameshiriki sheria itachukua mkondo wake kwa kila mtu.

“Tunategemea kupata taarifa kabla ya mwisho wa wiki hii, katika siku hizi za karibuni, hatujawapa muda mrefu kwa sababu ni kitu ambacho kina masilahi ya umma na inaweza kuwa inawaathiri wanafunzi wengi,” alisema.

Alisema kwa kuwa wizara hiyo ndiyo yenye dhamana ya kusimamia mambo yote yanayohusiana na vyuo, kinachofuata sasa ni kupata taarifa za kina kuhusu tukio hilo kutoka kwa viongozi waliopewa dhamana ndipo hatua stahiki zianze kuchukuliwa.

“Vilevile kama nilivyosema kama kuna mtu kahusika kufanya michezo michafu wala si cha kuzungumza hatua zitafuata. Tutalinda maslahi ya umma na wanafunzi dhidi ya maamuzi mabaya ya watu,” alisema Ole Nasha.

Pamoja na kauli hiyo ya Naibu Waziri, RAI limedokezwa kuwa tayari baadhi ya hatua zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na watu wanaohusika na masuala ya fedha za ada kuanza kuhojiwa na vyombo vya dola.

Katika kuhakikisha mchezo wa namna hiyo haijurudii, imeelezwa kuwa uongozi wa chuo kwa kushirikiana na Serikali umeanza kuusaka mtandao mzima unaojihusisha na michezo hiyo.

Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita RAI liliripoti kuhusu kupotea kwa mamilioni ya fedha ambayo hayakuwekwa wazi na uongozi wa chuo hicho, ambapo pamoja na mambo mengine baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho walizungumzia kwa kina kuhusu upotevu huo.

Wakizungumza na RAI kwa nyakati tofauti kwa sharti la majina yao kutotajwa gazetini, baadhi ya wanafunzi hao ambao waliwakilisha wenzao wengi, walisema siku chache kabla ya kuanza kwa mitihani hiyo uongozi wa chuo ulitoa tangazo lililokuwa na majina ya wanafunzi ambao hawajalipa ada, kuwa hawataruhusiwa kufanya mitihani hadi hapo watakapokamilisha malipo hayo.

Mmoja wa wanafunzi hao, (jina limehifadhiwa) alisema tangazo hilo liliwashtua kutokana na idadi kubwa ya waliooredheshwa na kwamba wengi wao walikuwa wamekamilisha malipo ya ada na kuwasilisha stakabadhi za benki kwa uongozi wa chuo ambao uliwapatia vitambulisho maalumu vya kuwathibitisha kukamilisha malipo.

“Uliibuka mgogoro mkubwa kwa sababu wengi wetu tulikwishalipa ada na slip za benki tulikuwa nazo. Mbali ya kuwa na slip ambazo ni kawaida kuziwasilisha kwa uongozi, tulikuwa na vitambulisho tulivyopewa na chuo vya kuthibitisha kuwa tumelipa.

“Tulipoubana uongozi utuambie hela zetu za ada ziko wapi na tuliwahoji uhalali wa vitambulisho walivyotupa vya kuthibitsha kuwa tumekwishalipa, wakafuta tangazo lao na kuturuhusu tufanye mitihani. Mpaka sasa hatujui kinachoendelea kuhusu kupotea kwa ada zetu,” alisema mwanafunzi huyo.

Alipoulizwa Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye kuhusu madai hayo, alielekeza atafutwe Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Profesa Bonaventure Rutinwa ambaye amemwachia nafasi yake kwa sababu yeye yuko safarini.

“Mimi ninajiandaa kusafiri, ofisi nimekabidhi kwa naibu wangu Prof, Rutinwa ambaye ndiye hasa anayehusika na wanafunzi kwa sababu anasimamia taaluma. Mtafute huyo, nakupa namba yake, ndiye anayeweza kulitolea maelezo vizuri jambo hilo,” alisema Prof. Anangisye.

Alipoulizwa Prof. Rutinwa kupitia simu yake ya kiganjani, alilitaka gazeti hili kufika ofisini kwake Agosti 20, mwaka huu kwa ajili ya mahojiano ya ana kwa ana.

Katika mahojiano ya ana kwa ana na RAI, Prof. Rutinwa alikiri kutoonekana kwa fedha za ada zilizolipwa na wanafunzi ambazo hazionekana katika kumbukumbu za malipo zilizopo chuoni, hata hivyo alisema jambo hilo, halithibitishi kuwa zimeibiwa mpaka hapo uchunguzi wa mahali fedha hizo zilipo utakapokamilika.

Prof. Rutinwa alisema uongozi wa chuo ulibaini kuwepo kwa utata kuhusu malipo ya ada za wanafunzi baada ya kutoa tangazo la kuwazuia kufanya mitihani ya muhula wa mwezi wa sita wale ambao hawakuwa kwenye orodha rasmi ya chuo inayoorodhesha waliokamilisha malipo ya ada.

“Kwanza siyo kweli kwamba kuna fedha za ada za wanafunzi zilizoibiwa, nisikilize vizuri, siyo kweli. Mimi ni mwanasheria na nimesomea ‘media law’ hivyo ukiandika zimeibiwa nakushtaki ila unachoweza kusema ni kwamba kuna fedha zilizolipwa na wanafunzi lakini hazionekani hapa chuoni kwetu.

“Iko hivi, mwanafunzi akilipa ada benki yoyote ile, sisi hapa chuoni kwenye mfumo wetu wa malipo, hiyo hela aliyolipa tunaiona hivyo hatuhitaji hata aje na slip. Wote wanaolipa huwa tunawapatia vitambulisho kuwathibitisha kuwa wamekamilisha malipo yao ya ada.

“Sasa tulipotoa lile tangazo la kuwazuia kufanya mitihani wanafunzi ambaohapachuonikwetuwanaonekana hawajalipa, wengi walionyesha ushahidi wa slip na vitambulisho vyetu kuwa wamelipa, hawadaiwi. Kwa sababu uliibuka mkanganyiko tukaona tuwaruhusu wote wafanye mitihani wakati tunafanya uchunguzi wa jambo hili,” alisema Prof. Rutinwa.

Alipoulizwa ni kwanini wanafunzi ambao majina yao hayaonekani kwenye mfumo wa chuo kwa waliokamilisha malipo ya ada walipewa vitambulisho vya kuwathibitisha kukamilisha ada alisema jambo hilo ndilo linalofanyiwa uchunguzi kubaini tatizo liko wapi.

“Kuna uchunguzi unaendelea ili tujue tatizo liko wapo. Unajua hivi vitambulisho mtu anaweza kuvitengeneza tu na yapo matukio ya watu kulipa fedha benki na kupewa slip za uongo. Uchunguzi unafanyika ili kujua kama tatizo liko kwenye mabenki ya au hapa kwetu chuoni.

“Tulichobaini awali ni kwamba baadhi ya wanafunzi walijichanganya kufanya malipo. Kuna akaunti nyingi za chuo, ipo ya ada, ipo ya maradhi na ipo ya bima ya afya na nyinginezo. Sasa wapo ambao fedha za ada walizilipa kwenye akaunti ya maradhi au bima ya afya, lakini haya yote yanachunguzwa,” alisema Prof, Rutinwa.

Akizungumzia suala la wanafunzi wote kuruhusiwa kuendelea na masomo wakiwemo ambao hawajalipa ada, alisema utaratibu wa UDSM unaelekeza mwanafunzi ambaye anakosa vipindi kwa muda wa wiki nne kutoruhusiwa kufanya mitihani hivyo kwa kuzingatia ugumu wa hali ya maisha wanafunzi wanaruhusiwa kuendelea na masomo huku wakilipa ada taratibu ila wanaoshindwa kukamalisha mpaka kinapofika kipindi cha kufanya mitihani huzuiwa kuifanya.

“Jambo la msingi ni kwamba wanafunzi wote walifanya mitihani. Hapa kwetu mwanafunzi akikosa vipindi kwa wiki nne mfululizo, huyo hata akija kulipa ada baadaye na kuingia darasani, kama ameingia baada ya wiki nne wakati wenzake wakiwa wanaendelea na masomo haruhusiwi kufanya mitihani.

“Kwa hali ya sasa, ni vigumu kwa kila mmoja kukamilisha malipo ya ada anapoingia tu chuoni ingawa utaratibu unataka hivyo, lakini sisi tunalichukulia kibinadamu zaidi ndiyo maana tunawaruhusu kuendelea na masomo bila kujali nani anapata mkopo wa Serikali na yupi hapati.

“Na nataka ieleweke kuwa ingawa tuliruhusu wanafunzi wote kufanya mitihani lakini baada ya uchunguzi, ikibainika kuwa wapo wanafunzi ambao walifanya mitihani wakiwa wanadaiwa ada hao hatutawapa matokeo yao,” alisema Prof. Rutinwa.

KUFUNGWA KWA UCC

Akizungumzia uamuzi wa bodi wa chuo hicho kufunga baadhi ya vituo vya mafunzo ya Kompyuta yaliyokuwa yakiendeshwa na chuo hicho (UCC), Ole Nasha alisema licha ya vyuo kuwa chini ya wizara ila vina mamlaka ya kufanya mambo yao kulingana na taratibu za ndani kanuni na sheria zinazowaongoza wao.

“Kwa hiyo kama Bodi yao itakuwa imeridhia na kuona ni kwa masilahi mapana ya chuo kulingana na hali halisi watakayokuwa wameona, sisi hatuna shida lakini mara nyingi katika hatua ya maamuzi bodi wanaweza kuwa na namna ya kujiendesha ila kila kitu wanachokifanya wanatupa taarifa pia kama wizara,” alisema.

Aidha, akizungumzia kufungwa kwa kituo cha mafunzo ya Kompyuta yaliyokuwa yakiendeshwa na chuo hicho, Prof. Rutinwa amesema Bodi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kituo cha Mafunzo ya Kompyuta (UCC) imeridhia kufungwa kwa baadhi ya matawi ya chuo hicho.

Alisema hatua hiyo ni moja ya utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli lililoelekeza taasisi zote za Serikali kufanya shughuli zake katika majengo ya Serikali badala ya kupanga kwa watu binafsi.

Prof. Rutinwa alisema uamuzi huo wa bodi pia umezingatia ubora wa mafunzo yanayotolewa na chuo hicho ambayo sasa yamepitwa na wakati hivyo kuwapo kwa hitaji la lazima la kutoa mafunzo ya taaluma nyingine ambayo ni muhimu zaidi kwa wakati wa sasa.

Kauli hiyo ya Prof. Rutinwa ilikuwa ikijibu madai yaliyoibuliwa na baadhi ya wafanyakazi wa UCC kuwa baadhi ya matawi yake yamefungwa kwa sababu ya ukata na uongozi mbovu.

Katika madai hayo, UCC kilidaiwa kufunga matawi yake ya Mbeya na lile lililopo Mbezi Beach, Dar es Salaam na kwamba tawi la Arusha nalo liko mbioni kufungwa.

Aidha, katika mlolongo wa madai hayo, ilidaiwa pia kuwa vifaa vilivyokuwa kwenye vituo vilivyofungwa vimeharibika baada ya kutelekezwa nje kisha vikanyeshewa na mvua.

Katika majibu yake, Prof. Rutinwa alisema mafunzo ya kompyuta yaliyokuwa yakitolewa na UCC yalikuwa ya msingi ambayo sasa yanatolewa na vyuo vingi na hata kwenye shule za msingi na sekondari hivyo chuo hicho hakina sababu ya kuendelea nayo.

“Mafunzo ya kompyuta yanayotolewa na UCC hivi sasa yanatolewa mpaka kwenye shule za msingi na sekondari, huko mitaani kuna vyuo vingi tu vinatoa mafunzo kama hayo. Sasa sisi kama Chuo Kikuu hatuoni sababu ya kuendelea na kozi hizo,

“Na matawi ya Mbeya na Mbezi yalifungwa baada ya agizo la Rais lililozitaka taasisi zote za Serikali kuondoka kwenye majengo ya watu binafsi na kurudi kwenye majengo ya Serikali. Agizo la Rais na ubora wa mafunzo zote ni sababu za msingi za kufungwa kwa matawi hayo na hata Arusha ndiyo tutafunga.

“Tunaangalia kozi gani ya kutoa kwa wanafunzi wa Tanzania baada kuachana na hiyo. Mbeya yale majengo ni yetu hapo tutabadilisha kozi, ninakwenda huko karibuni kukamilisha mipango hiyo,” alisema Prof. Rutinwa.

Naibu Waziri, Wiliam Ole Nasha

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.