Mwanambu na kitumbo cha duara

Rai - - MBELE -

Ni kawaida mtu anaponena au kutenda jambo la kupendeza hadhira yake humpigia makofi ikiwa ni ishara ya kumpongeza. Huu ni uungwana unaomtia mtu shime ya kuendelea

Ni kawaida mtu anaponena au kutenda jambo la kupendeza hadhira yake humpigia makofi ikiwa ni ishara ya kumpongeza. Huu ni uungwana unaomtia mtu shime ya kuendelea kufanya vizuri zaidi. Lakini hutokea kwa baadhi ya watu hasa wasio na umakini pongezi za aina hii zikawalevya na kuwavimbisha kichwa. Sifa humjengea kedi akajivika matao ya juu ambayo kwa pamoja humpotezea mwelekeo wake akawa hafai kwa kutowea wala kwa asusa.

Kwa watu wenye umakini pongezi huzipokea kwa hadhari kubwa ajabu. Hapana neno au tendo duniani litalomfurahisha kila mtu. Kanuni ya maisha ni kuwa furaha kwa aliyeshinda, huzuni kwa aliyeshindwa. Hivyo siku moja ukitamani kuamini kuwa utafanikiwa kumfurahisha kila mtu basi utambue kuwa unajiandalia jakamoyo. Ni muhimu kufahamu na kuamini kuwa hata mafanikio yako yanayokupa ustahiki wa kupongezwa nayo ni uadui kwako.

Mti huandamwa na bughudha ya kupopolewa kwa mawe na vigongo kwa sababu ya matunda yake. Na mja huandamwa na bughudha ya jicho la hasidi kwa sababu ya neema yake. Undumilakuwili wa mwanadamu unaelezwa kwa namna nyingi. Hujasikia watu wakisema kuwa akumulikaye mchana usiku anakuunguza, au akuchekeaye usoni moyoni anakununia! Haya ni maneno ya dhana na wasiwasi, bali huo wasiwasi nao ni akili kwani asiye nadhari ng’ombe.

Wapo wanaodiriki kusema kuwa kwa watu wema kuishi na wasiwasi ni woga usio na sababu. Masalale! Hebu jaribu kuwaambia kuwa kwa sababu nyinyi ni watu wema basi msijisumbue kukomelea milango na madirisha ya nyumba zenu kwa komeo na kufuli. Watu wema ndio windo la waovu kama walivyo wanyonge kuwa windo la wenye nguvu. Ingekuwa chini ya jua la Mwenyezi Mungu hawapo watu wema basi na waovu wasingekuwepo. Hapana! Hadhari dhidi ya uovu haiepukiki.

Nakubaliana nao wanaosema kuwa wapo wanaopiga makofi kupongeza kwa dhati ya nafsi zao neno au tendo lenye kupendeza. Hawa ni watu wema. Na ndio hawa ambao ukinena au kutenda lenye kuchefua watakusifia kwa manukato yako ya gharama ambayo umejifukiza nayo hadi nzi wanakuzunguka. Na halafu uchunge sana. Ukiwaona adui zako au wapenzi wako wanashangilia jambo lako na kukupongeza, jambo hilo ni hatari kwako liache mara moja.

Siku moja mwanambu alionywa na mama yake kuwa mbu hawana chuchu za kunyonyesha watoto hivyo aende kwa wanadamu akapambane na hali yake. Mwanambu alirejea na kitumbo cha duara kwa shibe ya damu ya wanadamu huku akijisifu kuwa amewanywa damu hadi wakawa wanampigia makofi. Hakutambua mwanambu kuwa makofi yale yalikuwa yanamkosa kosa yeye. Hivyo uwaumize watu halafu wakushangilie kwa kukupigia makofi!

Inakupasa kuuepuka utoto wa mwanambu kwa hatua elfu nyingi. Nena ya kupendeza na tenda yaliyo mema ili kutimiza uungwana wako kwa wanadamu wenzako. Usinene au kutenda kwa kutarajia kupongezwa. Sifa kutoka kwa wanadamu hazina manufaa kwako kwani sifa nyingine ni kilemba cha ukoka. Na baadhi ya sifa ni makofi yaliyomkosa kosa mwanambu.

Kalamu ya muungwana ina bahati ya kuwa na wino usio na udi wala uturi hivyo kuwa mbali na hatari ya kusifiwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.