Kashfa ya Trump yafuata nyayo za Nixon,Watergate

Rai - - MBELE - NA HILAL K SUED

Wahenga walipata kunena kwamba historia ina tabia ya kujirudia, na hujirudia kwa sababu kuna watu hawakutia maanani wakati ule.

Miaka 44 iliyopita wakati Kashfa ya Watergate ilipotikisa dunia na kumng’oa aliyekuwa Rais wa 37 wa Marekani Richard Nixon, chama chake cha Republican kilinusurika kupotea kutoka ulingo wa siasa nchini humo kwa sababu viongozi wake watiifu walijiweka mbali na uhalifu wa kiongozi wao.

Seneta maarufu wakati ule Barry Goldwater wa Arizona (ambaye baadaye alirithiwa na John Mccain aliyefariki mapema wiki hii) alimwambia Nixon kwamba huo msalaba ataubeba mwenyewe kwani hakuwa na wapigakura wa kumuwezesha kukwepa kushitakiwa na Bunge.

Makamu wake wa Rais Gerald Ford, mtu mtulivu na mwenye maadili alisaidia kukirudisha chama hicho kwenye reli yake na mwaka 1980 kiliweza kuinyakuwa tena Ikulu ya Marekani chini ya Ronald Reagan na baadaye wakaja akina George Bush wawili (baba na mtoto) na hivyo chama hicho kiliweza tena kujisimika kama chama kikubwa nchini humo kama ilivyo historia yake.

Lakini leo hii viongozi watiifu wa chama hicho wamejisalimisha kabisa kwenye chama cha Donald Trump, wakipoteana mbele ya kile kinachoonekana kama uharibifu mkubwa wa maadili mema ya chama hicho cha waasisi wakubwa kama vile Abraham Lincoln, Theodore Roosevelt, Dwight Eisenhower na Ronald Reagan.

Kati ya wagombea 18 kutoka chama hicho walioshindana na Trump katika kinyang’anyiro cha uteuzi wa kugombea kiti cha urais mwaka 1916, ni mmoja tu, Gavana John Kasich wa Jimbo la Ohio ndiye alibakia kupambana vilivyo na Trump pale Rais huyo alipokuwa akipotosha, akidanganya kupitia kauli zake za kampeni na za akaunti yake ya Twitter.

Wanasiasa wengine kuanzia Gavana Scott Walker wa Wisconsin, Seneta Marco Rubio wa Florida, Seneta Ted Cruz hadi Gavana wa zamani Rick Perry wa Texas, Gavana Chris Christie wa New Jersey, Seneta Rick Santorum wa Pennsylvania na Gavana wa zamani Bobby Jindal wa Louisiana, walikuwa hawajiwezi kabisa mbele ya Trump.

Mwingine ni mwanasiasa ambaye aliyekuwa anadhalilishwa sana na Trump alikuwa Gavana wa zamani wa Florida Jeb Bush, na ambaye awsali aliyekuwa mgombea na akitajwa kama ni mrithi katika kuendeleza ukoo wa akina Bush katika uongozi wa nchi hiyo.

Mwanasiasa mwingine aliyekaa kimya wa chama cha Republican alikuwa Mitt Romney, mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi wa 2012, lakini naye alibakia kugombea Useneta tu wa jimbo la Utah na kubakia kama kivuli chake tu cha ugavana wa Jimbo la Massachussetts aliokuwa nao awali.

Na ni Trump mwenyewe binafsi ndiye alijihakikishia uongozi wa chama hicho bila ya kuwa na historia yoyote katika chama, na akakibadilisha kutoka kuwa mtetezi wa kuwepo kwa serikali ndogo (small government) kama ilivyokuwa sera kuu ya chama hicho hadi kuwa na sera kali kwa nchi za nje na kuibua migongano mikubwa kutokana na sera zake za ubaguzi wa rangi na wa kidini na kujaribu kusimika ubwanyenye wa mtu mweupe (white supremacy).

Na wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, Trump alikuwa anaonyesha waziwazi ubaguzi wa kijinsia hasa kwa mpinzani wake katika kinyang’anyiro cha kuwania urais, Bi Hillary Clinton – hasa pale alipoibuka na ushindi kwa njia ya electoral college, kitu ambacho kiliwashangaza Wamarekani wengi. Kwa uwingi wa kura moja moja Clinton alimzidi Trump kwa zaidi ya kura 2.8 milioni.

Na baada ya hapo Trump kwa njia za ubabe alijisimika kukidhibiti chama cha Republican pamoja na kwamba Mabunge yote mawili ya nchi hiyo tayari yaliibuka na idadi kubwa ya wajumbe kutoka chama chake, hali ambayo wangekuwa na sauti kubwa kuliko Trump katika masuala ya kutengeneza sera na maamuzi ya kitaifa. Lakini badala yake wajumbe wake walionekana kujisalimisha kwa maamuzi mengi tata ya Trump.

Kuhusu kuhusika kwa Russia katika uchaguzi uliomuweka madarakani, suala ambalo sasa linachunguzwa na Muendesha mashitaka maalum Robert Mueller, Trump mara kwa mara alikuwa akiyakana vikali madai hayo.

Hata hivyo chama hicho cha Republican ambacho kilinusurika kupotea kutokana na Kashfa ya Watergate iliyomuondoa madarakani rais wake Richard Nixon kwa aibu kubwa, sasa hivi kimejikuta tena kimenaswa na rais mwingine ambaye utawala wake unatishiwa na tuhuma mbali mbali za utumiaji madaraka vibaya.

Jumapili iliyopita, wakili wake Michael Cohen alikiri mbele ya mahakama makosa ya kutoa fedha kwa mcheza filam za kingono Stormy Daniels na mwanamitindo Karen McDougal, wanamama ambao Trump aliwahi kufanya nao mapenzi. Malipo hayo, ambayo Cohen mwenyewe alikiri kuyatoa, alisema yalitokana na “maagizo ya mgombea urais” – yaani Trump, na yalikuwa yanakiuka sheria za matumizi ya fedha katika kampeni za uchaguzi.

Hali kadhalika Jumanne hiyo hiyo, aliyekuwa mwenyekiti wa kampeni wa Trump Paul Manafort alipatikana na hatia katika makosa manane ya udanganyifu na ulipaji kodi. Lakini tofauti na mwaka 1974 wakati wa Kashfa ya Watergate, safari hii kunaonekana hakuna wanasiasa mashuhuri kama vile Barry Goldwater (wa wakati ule) mwenye maadili ya kisiasa na ambaye yuko tayari kumwendea Trump na kumwambia “muda wako umekwisha.”

Kusema kweli, uungwaji wake mkono mkubwa nchini kote kunampa jeuri, na hadi hatua hii ya uchunguzi unaoendelea dhidi yake unaoendeshwa na Robert Mueller, amejenga matumaini ya kunusurika kisiasa hadi mwisho.

Lakini wachunguzi wa mambo wanasema hatua hii inaonekana kama ni kuzuia haki isitendeke na hivyo kuwa na sababu ya kushitakiwa Bungeni (impeachment) kama vile ilivyokuwa kwa Nixon mwaka 1974, ingawa yeye alikwepa kushitakiwa kwa kuwahi kuandika barua ya kujiuzulu urais.

Hivyo kwa vyvyote vile chama kimejikuta kinakabiliana na hali ile ile ya 1974 ya kujiangamiza, na kupona kwake hakutakuwa rahisi kwa sababu karibu wanasiasa wakuu wote wa chama hicho wanaonekana kumuunga mkono Trump.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.