Pongezi Dk. Mpango kwa kusimamia sheria

Rai - - MAONI/KATUNI -

NI nadra sana kutokea. Hivi ndivyo unavyoweza kusema kuhusiana na mzozo wa makontena yanayoshikiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam, almaarufu ‘Makontena ya Makonda’ — kwamba viongozi wawili wa Serikali wametofautiana katika uamuzi tena hadharani.

Awali iliarifiwa kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alizuia kwa kulihusisha jina la Mwenyezi Mungu — kwamba yeyote atakayenunua makontena hayo, atalaaniwa yeye na kizazi chake. Haya hayakuwa maneno mazuri kutoka kwa kiongozi huyo na alikuwa anawatisha watu waliokuwa na nia ya kuyanunua makontena hayo. Matokeo yake, hayakununuliwa na hivyo kuikosesha Serikali mapato.

Baadaye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akaenda bandarini na kuagiza kwamba makontena hayo 20, ambayo yanadaiwa kodi takriban, Sh bilioni 1.2 yapigwe mnada ili kukomboa mapato ya serikali.

Suala hapa sio nani ni sahihi, bali ni suala la sheria na taratibu za kuingiza bidhaa nchini zinajulikana. Tunajua kwamba shehen samani ulioagizwa kutoka nje ya nchi haina msamaha wa kodi, na haijalishi unaagizwa na serikali, taasisi za umma au mtu binafsi, na kwamba aliyeagiza anapaswa kulipa kodi stahiki.

Tunajua pia kwamba Makonda aliomba msaada kwa wafadhili wa diaspora nchini Marekani, kwa nia nzuri ya kusaidia kuinua hali ya miundombinu ya elimu mkoani Dar es Salaam. Na baadaye aliomba msamaha wa kodi kwa maelezo kwamba bidhaa hizo zitatumika katika shule za mkoa wake.

Lakini pamoja na kwamba nyaraka za usafirishaji makontena hayo zimeandikwa jina binafsi la Makonda yalipaswa kulipiwa ushuru kwa vyovyote vile kufuatana na sheria.

Hivyo jitihada za Makonda za kuomba msamaha wa kodi, hazikuzaa matunda na alijulishwa hivyo. Na muagizaji mali, kwa mujibu wa sheria akishindwa kulipa kodi, mali hiyo inatakiwa iuzwe kwa njia ya mnada. Lakini kwa kuwa Dk Mpango na Makonda, wote wanaitumikia Serikali moja — ambayo ina lengo la kuboresha elimu na kuinua hali ya walimu, tunashauri kwamba fedha zitafutwe kutoka serikalini au hata kwa Wasamaria wema za kulipia ushuru sitahiki na yaondolewe bandarini. Kuendelea kuyahifadhi makontena hayo bandarini, ni kuipa Serikali hasara zaidi.

Tunamuunga mkono Waziri wa Fedha Dk Mpango kwa kusimamia sheria za nchi na kuwashauri watendaji wengine kufanya hivyo, kwani utawala unaofuata sheria za nchi ndiyo utawala uliotukuka, na huepusha mmambo mengi hasi yanayoweza kulikumba taifa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.