HERI HOZA: Viongozi chapeni kazi, acheni maigizo

Rai - - WIK UTAWALA - NA VICTOR MAKINDA, MOROGORO

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Mkoa wa Morogoro, Heri Hoza, amewaonya watendaji wa serikali kutofanya kazi kwa kutanguliza maslahi yao binafsi, bali waangalie maslahi mapana ya jamii ambayo bado inakabiliwa na changamoto nyingi.

Katika mahojiano maalumu na ‘Rai’ hapa mjini, Heri alisema kuwa wapo baadhi ya viongozi wanaofanya kazi kinyume na misingi ya uadilifu, kufuata kanuni na miongozo ya majukumu yao. Lakini wame wamekuwa mstari wa mbele kutumia vyombo vya habari kwa lengo la kujionesha kama wanafanya kazi nzuri.

“Viongozi waache blabla na maigizo, waache kutumia vyombo vya habari kutaka kuonekana kuwa wanafanya kazi, wajikite katika kutatua kero za wananchi. Nchi yetu bado ina changamoto nyingi, uimarishwaji wa huduma za afya, elimu, maji, barabara, kilimo na viwanda, ni miongoni mwa masuala tunayoyapa kipaumbele. Haya hayawezi kufanikiwa kama tutaendelea kuwa na aina ya viongozi waigizaji na wanaofanya kazi kwa staili ya kuvizia teuzi, au kulinda na nafasi zao. Tuliowapa mamlaka wanapaswa kuyasimamia mambo haya vizuri na kuwa weledi.

Ukweli ni kwamba, wapo baadhi ya viongozi utendaji kazi wao unaelekea kuonesha kutaka sifa tu, kwani wanachokionesha kwenye vyombo vya habari sio uhalisia wa hali halisi.” Alisema Hoza.

Hoza anaongeza kusema kuwa baadhi ya viongozi hutoa takwimu za uongo, ili kumfurahisha Rais. Anasema kuwa viongozi wazembe hujifungia maofisi na kuandaa takwimu za uongo. Kwa kuwa ni wazembe, hawaendi kwa wananchi kujionea hali halisi.

Alisema kuwa Rais Magufuli hapendi kufurahishwa na vitu visivyo halisi, bali anapenda kuwaona watendaji wakichapa kazi kwa juhudi na maarifa, ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanaondokana na kero zinazowakabili.

“Watanzania tuna bahati kubwa, tumepata bahati kama Taifa kuwa na Rais mchapa kazi na mpenda maendeleo. Namna nzuri ya kuziunga mkono juhudi za Rais John Magufuli, ni kuchapa kazi kwa bidii.”

Anahofia kama Tanzania itatimiza dira yake ya kuwa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, kwani kuna baadhi ya viongozi hawajitoi kufanya kazi, ili Watanzania waishi maisha bora.

Anawalinganisha viongozi wa aina hii na wahujumu— wanahujumu juhudi za Rais za kumwondolea Mtanzania kero za afya, maji, nishati, barabara na elimu.

Anawashangaa viongozi ambao hutoa matamko na maagizo mapya kila kukicha, lakini hawayafuatilii ili kujiridhisha kama yametekelezwa kwa kiasi gani.

Anawashauri wache kutoa matamko kwa kutaka sifa na kuonekana, bali watoe matamko na maagizo na kisha wayafuatilie utekelezaji wake.

“Kwa nini kutoa matamko kila siku bila kujua agizo la jana limetekelezwa ama lah?” Anauliza na kuongeza kuwa uongozi wa matamko na maagizo pasipo kufuatilia, kwa ni uongozi usio na tija. JUMUIA YA WAZAZI kuwa ya KIUCHUMI. Hoza anasema kuwa yeye anaamini kuwa siasa ni uchumi. Anasema kwa upande wake, anadhamiria kuifanya jumuiya hiyo kuwa ni ya kiuchumi zaidi, lakini pia iendelee kufanya siasa.

“Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisisitiza kuwa siasa ni Kilimo. Unaposema siasa ni kilimo, ina maana pia kuwa siasa ni uchumi, kwani zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo.”

Anasema haitakuwa na maana kama tutafanya siasa juu ya ardhi ya watu wanaokabiliwa na uchumi mbovu. Hivyo yeye amedhamiria kuifanya Jumuiya kuwa mfano wa kuigwa katika nyanja ya kiuchumi.

“Tayari nimeunda Kamati ya Uchumi ya Mkoa, pia nimeelekeza wilaya zote katika mkoa wa Morogoro, kuunda kamati za uchumi kupitia kwa makatibu wa wazazi wilaya. Lengo kubwa ni kwamba kamati hizi zianzishe shughuli za uchumi kulingana na jiografia ya wilaya husika.

Nimeelekeza kamati hizo zijikite katika kuzalisha mazao ya kilimo ambayo kimsingi, ni malighafi muhimu kwa ajili ya viwanda. Sitaishia kuagiza tu, bali nitakuwa nikufuatilia kwa umakini kuhakikisha malengo yanatimia.” Anasema

Anatoa mfano kwamba Jumuia tayari ina ekari 100 (mia moja)enelo la Mkulazi, Morogoro Vijijini ambazo wanatarajia kupanda miwa kwa ajili ya kulisha kiwanda cha sukari kinachojengwa katika eneo hilo.

Aidha, Jumuia iko mbioni kuanzisha kiwanda cha chaki kwa ajili ya shule na itakuwa inazisambaza nchi.

KUIMARISHA JUMUIYA

Hoza anasema kuwa amebaini upungufu mkubwa wa vitendea kazi na kadi za uachama na kwamba baadhi ya viongozi wa Jumuiya hiyo, hawashika itikadi ya chama na hawayajui majukumu yao.

Aliwataka viongozi wote wa Jumuiya kuanzia mkoa mpaka tawi, wanakuwa na vitendea kazi, sare na kadi za chama. Anasema atahakikisha viongozi wote wanapata mafunzo ya itikadi sambamba na uzalendo.

“Kuna uhaba mkubwa wa kadi. Kadi ndio uhai wa chama na mwanachama. Huwezi kusema kuwa una wanachama kadhaa kama huna kadi zilizo hai mikononi mwa wanachama. Nitafanya juhudi kuhakikisha suala la kadi nalimaliza, lakini pia sare za chama zinapatikana.”

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM mkoa wa Morogoro, Heri Hoza.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.