Vijana ni mti unaokua, tuchunge ndimi zetu

Rai - - MAKALA - NA GORDON KALULUNGA

VIONGOZI wa kisiasa, hasa vijana, ni sawa na matunda ambayo hayajakomaa, hivyo hayajulikani kama ni matamu au machugu.

Katika nchi iitwayo ‘Mzurikwao’, Katiba yao iliruhusu kuwa na

demokrasia ya vyama vingi. Mbali na demokrasia kuendelea kukua, lakini kuna viashiria ambavyo vilionyesha kuwa waumini wa chama tawala, hawakuwa tayari kuipokea hali hiyo.

Nchi ikaendelea na viongozi wakaedelea kuiishi demokrasia hiyo, huku upinzani ukionesha kuendelea kujijenga.

Vijana wengi wakaonekana kuvutiwa sana na vyama vya upinzani, hivyo wakalazimika kujiunga huko na kuibua mambo kadhaa ya kimantiki katika nchi hiyo ya Mzurikwao.

Baadaye, wengi wa vijana hao, wakaanza kukitukana sana chama tawala cha nchi hiyo, na kuwasema vibaya vijana wenzao walio chama tawala—yakiwemo maneno yaliyokuwa yakiashiria kuwa vijana walioko chama tawala, ni kama akili zao zilikuwa zimepungua.

Kuna wakati hali ilibadilika, vijana hao wa upinzani, baada ya

kugundua kuwa sehemu waliyokuwepo hakukuwa na uwezekano wa kupata ajira za kuteuliwa na watawala, wakaanza kurejea katika chama tawala.

Kila kijana kutoka upinzani aliyetangaza kujiunga na chama tawala hakuwa na hoja ya msingi, zaidi ya kusema wanaunga juhudi za uongozi wa mfalme wa nchi ile, huku wakifumba mdomo kabisa kuwa wanakubaliana na mfumo wa chama husika.

Kila walipojiunga wakawa wanateuliwa kuingia kupata ajira serikalini huku wakiendelea kuwacheka sana vijana wenzao waliokuwa wakikipigania chama tawala.

Walipokuwa wanarejea, wakawa wanatoa siri za wakubwa chama wanakotoka, bila kusema wao walishiriki vipi dhambi hizo, ili wapimwe kuwa ni wasafi kiasi gani.

Vijana waliokuwa wakiendelea kutumikia chama chao, wakawa wanaugulia maumivu, maana baadhi yao, kwa mapenzi mema, wamewahi hata kupona kufa katika kampeni, lakini hawakuwa na namna kwa sababu walikuwa wanamuogopa sana mfalme wa nchi ya Mzurikwao.

Wakawa wamevunjika mioyo sana, lakini kwa sababu ya uwoga, wakawa wananung’unika mioyoni na mitaani na kumwachia Mungu mambo yote—huku wakisema kuwa endapo kutakuwa na uchaguzi halali mwingine, watampumzisha mfalme huyo, baada ya kipindi cha miaka mitano tu, badala ya 10 kama Katiba ya nchi yao inavyotaka.

Ilipofika miaka mitano, wakafanya kila waliloweza kuwaunga mkono viongozi wengine ndani ya chama hicho hicho, kuwa wanastahili kuchukua fomu za kurithi ufalme wa mfalme aliyekuwepo—huku wale vijana waliotoka upinzani na kupewa vyeo, wakiwa upande wa mfalme aliyewapa kazi na wakaanza tena kuwatusi viongozi waandamizi wa chama hicho waliowakuta kwa sababu wao walikuwa wanamheshimu aliyewapa kazi tu.

Hali hiyo ambayo ilikuwepo na kutokea katika nchi ya Mzurikwao haiwezi kutokea Tanzania.

Ila nakumbuka rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia kuwa, sisi viongozi vijana, ni sawa na mti wenye matunda ambayo hayajulikani utamu wake na uchumgu wake.

Hayajulikani yanaweza kuwa ni afya kwa walaji au sumu.

Mambo makubwa ya kuzingatia, ni kuwa tunahitaji subira na hekima kwa matamshi na matendo yetu.

Hakuacha kunisihi kuwa siyo busara wala afya, kumwambia mwanasiasa, au mtu mwenye haiba ya siasa, siri yeyote au mipango yeyote, kwani wanasiasa wapo wa aina mbili.

Wapo wasaka vyeo na wapo wapambania vyeo, na wote hutegemea taarifa zako.

FUNZO

Kutukana au kutoa siri za mwanasiasa mwenzako, sio ukomavu wa siasa ni kipimo cha kutokuaminika na kutokuwa na sifa za kuwa mwaminifu kabisa.

Namaliza kwa kusema wanasiasa vijana ni mti unaokuwa, hivyo ni vema sana tukachunga ndimi zetu kama akina Lembeli.

Hii ni sauti kutoka hapa Nyikani.

Patrobas Katambi

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.