Tanzania mpya – vikwazo na changamoto

Rai - - MAKALA - NA MUDHIHIR M. MUDHIHIR

TUMEAZIMIA kuijenga Tanzania mpya. Ni dhamira njema itakayotujengea uhuru wenye nguvu ya kujiamulia matakwa yetu na kutujengea heshima ya nchi yetu na ya utu wetu ndani ya dunia ambayo nguvu ya taifa lolote, inatokana na uimara wa uchumi wake. Tumeianza safari hii kwa kishindo kikubwa na dalili zinaonyesha matumaini ya kufikia azma yetu. Hatuna budi kufahamu na kukubali kuwa mbele yetu tunavyo vikwazo na changamoto.

Lengo kuu la kuijenga Tanzania mpya ni kuiwezesha nchi yetu kumiliki uchumi wa kati. Hatupaswi kuitazama dhamira yetu kuwa ni njozi za mchana kwani jambo hili linawezekana kutimia ikiwa kila mmoja wetu ataliafiki na kutimiza wajibu wake. Mbegu ya fikra ya aina hii ilipandwa katika mataifa tuliyokuwa tunalingana nayo kiuchumi hasa katika mataifa ya mashariki ya mbali, na leo tunayaona yanavyonawiri kiuchumi.

Tunaihitaji Tanzania mpya yenye kumiliki uchumi wa kati ili kuukuza ustawi wa taifa letu litakalohimili kuhudumia mahitaji ya watu wake mmoja mmoja na mahitaji ya nchi kwa ujumla wake. Tunahitaji Tanzania mpya yenye fursa za kuwawezesha raia wake kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wa uchumi wetu, kumudu maisha yao na kuchangia mapato ya nchi yetu.

Katika safari yetu hii ya kuelekea uchumi wa kati tumeamua kuchagua Tanzania ya viwanda kama masurufu muhimu ya safari yetu. Hatuna budi kutambua na kukiri kuwa hatuwezi kuanza kupaua na kuezeka kabla ya kujenga msingi na boma. Na hii ndio sababu ya kuanza na viwanda vidogo viogo vya kuchakata mazao ghafi na viwanda vya ukubwa wa kati. Safari huanza na hatua moja.

Tunaijenga vipi Tanzania ya viwanda ni suala linalohitaji tafakuri ya kina kinadharia na kisayansi. Tumechagua viwanda na Waswahili husema kuwa kupanga ni kuchagua. Hatuhitaji kupoteza muda wa kutafuta kinachoanza kati ya kuchagua na kupanga. Lisilo na mjadala ni ukweli kuwa tukishindw akupanga basi tutambue kuwa tumepanga kushindwa. Mwenza wa lengo daima ni mpango. Tunahitaji mipango thabiti.

Tanzania ya viwanda inahitaji mwega unaojumuisha sekta za huduma, uzalishaji wa malighafi, mazingira rafiki katika kilimo, mifugo, uvuvi, madini na biashara, na mipango iliyo thabiti katika kuratibu na kusimamia uchumi. Mwega huu unahitaji kuumiza kichwa ili kufikia ubunifu, uyakinifu na umakinifu ndani ya serikali katika jitihada zake za kuijenga Tanzania ya viwanda. Mipango ndio pango linalohifadhi mizungu ya mafanikio.

Vikwazo na changamoto

Mabonde na milima katika safari ya nchi kavu sioshani kama ilivyo kwa safari ya baharini, pepo za mbisho na mawimbi kuwa ndio safari ya jahazi. Husemwa kuwa hata wanaosafiri kwa ndege hukutana na misukosuko ya tufani na mawingu yenye radi. Hapana shaka kuwa safari yetu ya Tanzania ya viwanda ina misukosuko yake ya vikwazo na changamoto. Safari si matembezi. Safari ina harubu zake.

Dunia ya viwanda imesheheni ushindani wa thamani ya bidhaa, teknolojia na mitaji. Pamoja na ushindani huu tukiwa na malighafi ya kutosha na yenye viwango inatosha kuwa chambo cha kuvutia uwezekaji katika viwanda vya kuongeza thamani malighafi zetu. Jambo la msingi ni kuendelea na azma yetu basi mvua au jua tutatafuta mwavuli au kivuli mbele ya safari. Maadamu tumeyavulia nguo hatuna budi kuyaoga.

Tunalo tatizo la usingizi wa kubweteka bwetebwete kwamba hatuwezi. Hili ni tatizo linalotatulika kwa kuwaamini na kuwasomesha zaidi wasomi wetu hapa ndani na huko ng’ambo. Hayupo aliyekuja hapa duniani na elimu yake kibindoni. Tunahitaji kuwa na mfumo wa elimu itakayokidhi mahitaji yetu, itakayoukabili mwenendo na mabadiliko ya dunia ya leo, na elimu inayotafsiri nadharia katika vitendo.

Kasuku ni ndege anayeweza kuimba nyimbo anazofundishwa na bwana anayemfuga. Wakati wa kusujudia mfumo na mitaala ya elimu tuliyoachiwa na mabwana umepita. Tunahitaji sasa mitaala itakayotuwezesha kuleta matokeo yenye tija katika kilimo, uvuvi, ufugaji, ufundi na taaluma nyinginezo kwa shabaha ya kutuletea elimu yenye manufaa. Kwa mwelekeo huu Tanzania mpya inawezekana.

Zipo changamoto katika safari yetu ambazo kimsingi zinatuhitaji kufanya uamuzi wa mabadiliko ya makusudi katika dhamira, utashi na fikra, ili kutuwezesha kuzikabili changamoto na kutuongezea ari ya kusonga mbele. Tukichagua moyo wa kujiamini na ujasiri wa fikra, changamoto si vikwazo bali ni fursa. Hapa tulipo hatukuwekwa na nguvu za kufikirika bali haya ni matokeo ya shubiri ya ukoloni inayoendelezwa na asali ya ukoloni mamboleo.

Kimaumbile hawa wapo kama sisi. Hewa tunayoivuta mapafuni ni ile ile. Sote tunafikwa na njaa na kiu, na sote tunazaliwa na kufa. Ikiwa ipo tofauti basi ni ya rangi zetu na pengine lugha zetu. Lakini kwani tunafikiri kupitia rangi zetu? Zipo baadhi ya nyakati natamani kuamini kuwa asali ya ukoloni mamboleo imepakazwa katika kidonge cha lugha za mabwana.

Hebu twendeni tukawatazame mafundi wa magari wa gereji za mitaani wasiojua “yes yes” mzungu kala fenesi. Wanaimudu kazi yao utasema walisoma kwenye viwanda vya magari. Halafu tuwatazame wahandisi katika fani hiyo wanapozimikiwa na gari barabarani. Sikusudii kushusha hadhi ya yeyote bali natilia mkazo mfumo wa elimu yetu na lugha inayotumiwa katika kufundishia na kujifunzia.

Unapozama katika tafakuri unawaza kwa Kiswahili. Unapoota ndoto ukiwa usingizini unaota kwa Kiswahili. Unapougulia maumivu kitandani ni “Mungu wangu wee, mama yangu wee”. Lakini ukiwa darasani lugha ni kimombo ni “aam aam” nyingi. Wachina, Wakorea Kusini na Waturuki wanatumia Kiingereza katika mifumo yao ya elimu? Wajapani wanatumia Kiingereza?

Leo Wachina, Wajapani, Wakorea Kusini, Wajerumani, Wafaransa, Warusi ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwakiteknolojia nakiuchumi. Bila ya shaka matumizi ya lugha zao za asili katika mfumo wa elimu, huchangia vya kutosha ufahamu kwa wepesi na uyakini. Wanajifunza Kiingereza kama somo tu na wanakizungumza vizuri tu kama wasomi wetu.

Serikali inapaswa kuiangalia changamoto ya elimu kwa mfumo wake, mitaala yake na lugha ya kufundishia ikiwa tunaitaka kasi ya kupaa kuelekea Tanzania mpya. Idadi kubwa ya wajenzi wa uchumi wa nchi yetu hatujui kimombo. Hebu tupeni elimu kwa kutumia Kiswahili muone. Uchumi wetu tunaujenga humu nchini sio Ulaya.

Kasuku ni ndege anayeweza kuimba nyimbo anazofundishwa na bwana anayemfuga. Wakati wa kusujudia mfumo na mitaala ya elimu tuliyoachiwa na mabwana umepita. Tunahitaji sasa mitaala itakayotuwezesha kuleta matokeo yenye tija katika kilimo, uvuvi, ufugaji, ufundi na taaluma nyinginezo kwa shabaha ya kutuletea elimu yenye manufaa. Kwa mwelekeo huu Tanzania mpya inawezekana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.