Kuna vyombo vingi vya habari, waandishi wa habari wachache

Rai - - MAKALA - VICTOR MAKINDA

Fani ya uandishi wa habari ni miongoni mwa fani muhimu katika jamii. Dhima ya vyombo vya habari kwa muktadha wa maendeleo ni jambo lisiloepukika. Vyombo vya habari vina mchango mkubwa sana katika kuchochea na kukuza maendeleo ya jamii yoyote iwayo.

Ukweli ulivyo vyombo vya habari ni muhimili mkubwa katika kueneza habari, taarifa na masuala yafananayo. Vyombo vya habari ni muhimili wa nne wa serikali, ikitanguliwa na Dola, Bunge na Mahakama.

Vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kutoa elimu ya masuala anuani ya kisekta na kisera. Masuala kama ya afya, taadhari ya majanga na mengine mengi kwa kiasi kikubwa hutegemea taarifa sahihi kupitia vyombo vya habari. Pia vyombo vya habari hutumika katika kusambaza kampeni zenye lengo mahususi la ama kuipa uelewa jamii au kutaadharisha jamii.

Kazi, sifa na umuhimu wa vyombo vya habari ni nyingi. Itoshe tu kusema kuwa jamii zetu zinahitaji vyombo vya habari mahiri kwa lengo la kuchochea maendeleo na ustaarabu wa jamii.

Ikumbukwe kuwa vyombo hivi vya habari vinaweza kutumika ndivyo sivyo. Yaani kinyume chake. Ukweli ulivyo yapo maeneo duniani vyombo vya habari vimewahi kutumika kusambaza chuki kati ya jamii moja dhidi ya jamii nyingine na kuleta matokeo mabaya kabisa. Vita na uhasama wa kijamii ni miongoni mwa madhira yaliyochochewa na vyombo vya habari baadhi ya maeneo jirani.

Hapa kwetu Afrika Mashariki tunao mfano hai juu ya madhara na madhira yaliyosababishwa na vyombo vya habari pale vyombo hivyo vilipotumika kinyume chake.

Yaani vilipotumika kwa mintaarafu ya kusambaza chuki, husuda na kuchochea hamasa ya kufanya vurugu na mauaji. Nchini Rwanda yalipotoea mauaji ya Kimbari mwaka 1994, mchango wa vyombo vya habari unatajwa kama miongoni vya vichocheo vikubwa vya mauaji hayo.

Ukweli ulivyo hatuwezi kuzungumzia vyombo vya habari pasipo kuwataja waaandishi wa habari ambao ndio wenye dhima kubwa ya kufuata miiko na maadili ya taaluma ya uandinshi wa habari na hatimae kutumia vizuri vyombo vya habari kwa malengo yenye tija kwa jamii.

Kichwa cha makala hii nimeeleza kuwa kuna vyombo vingi vya habari, lakini kinyume chake kuna waandishi wa habari wachache sana. Mpishano na utofauti huowa uwianao kati ya vyombo na wanataaluma hauna siha njema kwa fani ya uandishi wa habari.

Ninaposema kuna waandishi wachache wa habari nina maana mbili. Maana ya kwanza ni idadi ya waandishi mahiri wana taaluma kulinganisha na idadi ya vyombo vya habari vilivyopo. Kwenda mbali zaidi hapa nina maana kuwa hivi sasa kuna ongezeko kubwa la namna ya kupata kukusanya na kutoa taarifa. Hii inatokana na kukua kwa tenkolojia ya vifaa vinavyoweza kukusanya taarifa na kuzisambaza.

Tofauti na yalivyo matakwa ya kitaaluma ya habari, taarifa hukusanywa na kuchujwa na wana taaluma ya habari kwa lengo la kujiridhisha juu ya ukweli na maudhui yake kwa hadhira na hatimae kutangazwa kupitia vyombo rasmi vya habari.

Hivi sasa hali ilivyo ni kinyume chake. Ukweli ulivyo ongezeko la matumizi ya simu za mkononi maarufu kama SmartPhone, limeongeza idadi ya watoa taarifa za habari wasio na weredi wa kutoa taarifa hizo. Hali ilivyo kwa sasa kila mtu ni mpiga picha na mwandishi wa habari, mamladi anamiliki simu yenye uwezo wa kupiga picha na kusambaza habari. Matokeo yake kila kukicha tunakumbana na habari za uongo na picha dhariri.

Kana kwamba hilo halitoshi wana habari wasio na taaluma ya habari wamekuwa chanzo cha uzushi na udhalilishaji.

Pamoja na uwepo wa sheria inayosimamia mitandao ya kijamii (Social Media), bado kadhia hiyo ipo. Hapa msisitizo ni sheria kuongeza makali yake ili jamii ya kitanzania isitumbukie katika uwanja wa uzushi, kashfa ni kuchochewa kuingia kwenye hali ya sintofahamu na hatimae vurugu.

Maana ya pili ya vyombo vya habari kuzidi idadi ya waandishi ni kwamba, ijapokuwa kuna waandishi wengi wa habari, waliosomea fani ya uandishi wa habari kwa ngazi mbali mbali za kitaaluma, waandhishi mahiri, jasiri wenye uweledi wa taaluma na wanao simamia misingi ya taaluma ni wachache sana.

Hii ndiyo sababu ikiwa kuna kituo cha radio, luninga au gazeti linaanzishwa basi mmiliki atafanya kila namna kumnasa mwandishi A kutoka kituo B kana kwamba hakuna wana taaluma wa fani hiyo walio nje ya soko la ajira. Ukweli Ulivyo wapo waandishi wengi nje ya ajira lakini ama hawana uwezo mzuri au hawako tayari kulamba miguu ya wamiliki na wanasiasa.

Ukweli Ulivyo wapo waandishi wana taaluma ya habari wabobezi ambao ni ni bendera fuata upepo. Ni weledi wanao fahamu vyema misingi ya taaluma, lakini kinyume chake wanaangukia katika mikono ya ama wanasiasa au wamiliki wa vyombo vya habari na mwishowe hugeuka makusuku wakiimba kwa kufuatisha na kukariri nyimbo za ama wanasiasa au wamiliki wa vyombo hivyo ambao wamiliki hao walio wengi wamejiegemeza kwa wanasiasa.

Katika muktadha huo kinachotokea ni vyombo vya habari kuwa na agenda tofauti. Utofauti wa agenda hutokana na nani anamshabikia nani na nani anashabikia nini.

Kubaini hayo rejea kipindi kabla na wakati wa chaguzi kuu. Agenda za baadhi ya vyombo vya habari huwa ni kuchafuana na kuandika habari za uzushi zenye lengo la kusambaza propaganda za uongo zidi ya kundi fulani ama mgombea fulani.

Badala ya vyombo vya habari kuwa daraja kati ya wapiga kura na wagombea huku vikisambaza kwa usawa sera za wagombea kwa wapiga kura, vyombo hugeuka kusambaza proganda za uongo kwa wapiga kura huku vikiwa vimejibanza kishabiki kwa baadhi ya wagombea. Ukweli ulivyo ni hatari sana chombo cha habari kujigeuza shabiki na kutotoa habari kwa usawa.

Jamii ingetaraji kuona kuwa vyombo vya habari nyakati za uchaguzi vinatoa taarifa sahihi na kwa usawa huku vikichambua sera na kutoa ufafanuzi wa kina wa sera za wagombea kwa lengo la kuleta uwelewa sawia kwa wapiga kura. WAPO WAPI WAANDISHI JASIRI?

Najiuliza swali hili pasipo majibu. Wapo wapi waandishi jasiri wanaoweza kuhoji watawala? Wpo wapi waandishi wasio tayari kulamba miguu ya wamiliki na wanasiasa? Kipo wapi kile kizazi cha waandishi wenye uthubutu wa kukataa kukandamizwa misingi na taaluma ya uandishi wa habari? Wapo wapi waandishi wanaoweza kuthubutu kuandika na kuchambua habari za kweli iliyo kweli pasipo kuogopa kuusema ukweli?

Ukweli ulivyo waandishi wa habari wa karba hiyo kana kwamba hawapo? Kama wapo wako wapi, wanachambua wapi? Namaliza kwa kusema tunavyo vyombo vingi vya habari, tuna waandishi wachache sana wa habari. Tuupanue mjadala.

Waandishi wakiwa kazini

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.